Simorix The General Aiunganisha Australia na Bongo kwa Kolabo ya Remix ya Vaccine na Weusi
MBONGO aishie nchini Australia anayefanya vizuri kwenye muziki wa kizazi kipya, Saimoni Masanja a.k.a Simorix The General, ametua hapa nchini Tanzania kwa ajili ya kufanya remix ya ngoma yake ya Vaccine na Kundi wa Weusi lenye ngome yake Arusha hapa nchini.
Akizungumza na paparazzi wetu, Simorix The General, amesema ameamua kufanya hivyo ikiwa ni mwendelezo wa mpango wake wa kuliteka soko la Bongo Fleva nje na ndani ya Tanzania na kuipaisha lugha ya Kiswahili nchini Australia anakoishi kupitia muziki.
“Nimeamua kuja kufanyia remix ya ngoma yangu hii hapa nyumbani baada ya kubamba sana ndani na nje Australia ambapo na kila kitu nimeshakamilisha na muda wowote kuanzia sasa audio na video yake zitakuwa hewani.
“Nimefurahi sana kuona audio imepokewa vizuri na mashabiki kutoka kwenye mitandao yote ya kusikiliza na kupakua muziki hivyo, naamini hii ni hatua kubwa kwenye muziki wangu baada ya kufanya kazi na kundi bora la Hiphop Weusi,” amesema Simorix.
Wasanii aliowashirikisha kutoka kwenye kundi hilo ni pamoja na G Nako, Joh Makini na Lord Eyez.
Ngoma hiyo kwa mara ya kwanza iliruka hewani February 14 mwaka huu ambayo ilikuwa siku ya Wapendanao ndipo sasa amekuja na remix hiyo.
Akizungumzia sababu ya kufanya kazi hiyo na Weusi jamaa amesema alikuwa na uwezo wa kupiga kazi na msanii au kundi lolote lakini ameamua kupiga kazi na Weusi kwenye remix hiyo baada ya kupata ushauri kutoka kwa mashabiki wake” alimaliza kusema Simorix.