The House of Favourite Newspapers

Simu feki kuzimwa; vilio nchi nzima

0

Simu fekiMwandishi wetu, Amani

DAR ES SALAAM: Vilio vimetawala nchi nzima kufuatia serikali kuamua kutekeleza agizo lake la kuzima simu zote feki zilizokuwa kwenye mzunguko wa watumiaji.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti mara baada ya kuona muda uliotolewa na serikali unaelekea ukingoni, wananchi mbalimbali wameeleza masikitiko yao kwa kusema wanaumia serikali kufanya hivyo pasipo kuwafikiria hali zao ngumu.

“Wewe niangalie mimi, maisha yenyewe ni ya kuungaunga, ndugu zangu nao ni hohehahe, nitapata wapi fedha za kununua simu mpya? Walipaswa kutufidia kwanza,” alisema John Tindye, mkazi wa Tanga.

Kitundu Marwa, mkazi wa Tarime, alisema licha ya serikali kutoa muda wa miezi sita lakini ilipaswa kugharamia simu hizo kwani wao ndiyo walioziruhusu ziingie nchini.

“Sisi wanatutesa bure. Wewe unafikiri mimi nilijinyima kiasi gani hadi nikanunua simu? Hali yenyewe tete hii tena kama mimi simu ya mke wangu nilinunua kwa gharama kubwa kweli, nimeipeleka kwa fundi lakini nimeona bora hata niitelekeze huko.

“Bora ile hela iliyokuwa nimlipe yeye nitafute hata simu nyingine ndogo ambayo itakuwa ni orijino,” alisema Kitundu.

Akizungumza na gazeti hili, fundi mmoja wa simu aliyejitambulisha kwa jina la Dulla, mkazi wa Kariakoo jijini Dar, alisema wamekasirishwa na vitendo vya wateja ambao tayari walishapatana nao bei ya kutengeneza simu zao kuingia mitini.

“Wametutelekezea simu zao. Sasa tunashindwa kuelewa wana maana gani wakati kama  ni malipo tulishapatana na hata hawajaja kuzihakiki na kujua kama ni feki,” alisema Dulla.

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano  Tanzania (TCRA), ilitoa muda wa takriban miezi sita kwa Watanzania kuhakiki simu zao kabla ya kufanya zoezi la kuzima simu hizo linalotarajiwa kufanyika Juni 16, mwaka huu (leo).

Mamlaka hiyo ilisema imeamua kuchukua hatua hiyo kutokana na kushindwa kuzidhibiti simu hizo kwani mtumiaji kutoka mtandao mmoja akifanya uhalifu na akibadilisha laini kwa simu ileile, anashindwa kupatikana kirahisi.

Leave A Reply