The House of Favourite Newspapers

Simulizi: Nilivyokutana na Mzimu wa Kifo Oman-3

Ally Katalambula   +255 653428197

Ilipoishia wiki iliyopita.

Saa 48 baadaye, mimi na Mariamu tulikuwa kwenye teksi tukielekea sehemu moja iitwayo Suwaiq kilometa 50 kutoka mjini Muscat, huko ndipo mahali nilipotakiwa kwenda kufanya kazi ni huko ambapo kulikuwa na familia ya tajiri aliyeitwa  Abdallah Mustapha ambaye ndiye niliyetakiwa kwenda kuanza kazi nyumbani kwake.

“Karatasi za majibu yako ya vipimo  vya hosptali unazo?” Mariamu aliniuliza wakati gari likikunja kushoto na kuiacha barabara kubwa ya lami na kuingia kwenye barabara iliyokuwa na changarawe nyingi.

“Karatasi zipo kwenye begi, kwani majibu ya vipimo bado yanahitajika hadi huku?”

 “Ndiyo” alinijibu kwa ufupi. Nilijiuliza moyoni ina maana huko niendako, wao waajiri hawajui kuwa siwezi kuwa kwenye nchi hiyo pasipo kupima, vipi tena wahitaji majibu ya vipimo.

Wakati nikiwa bado najiuliza, gari lilikata kona na kuiacha ile njia yenye changarawe na kuingia kwenye njia nyembamba iliyokuwa na marumaru, pembeni ya njia hiyo kukiwa na miti mingi iliyopandwa kwa mpangilio mzuri.

Gari lilikwenda kwa mwendo wa taratibu, mita kama ishirini tukawa mbele ya nyumba kubwa iliyokuwa na sifa zote za kuitwa nyumba ya kifahari.

Baada ya dereva teksi kulipwa ujira wake na kuondoka, tukasogea kwenye geti la jumba lile, Mariamu alibonyeza swichi ya kengele iliyokuwa pale getini na muda mfupi baadaye, alikuja mvulana wa kisomali kufungua, nilipogonganisha macho na yule mvulana kitu fulani kisichoelezeka kilipita kichwani mwangu. Macho yangu yalinata kwa yule mvulana kwa nukta kadhaa.

Alizungumza na Mariamu kama watu wenye kufahamiana kwa muda mrefu, kilichonishangaza zaidi aliongea kwa Kiswahili, alikuwa ni mtu mcheshi na mkarimu, Kiswahili chake kilikuwa na lafudhi ya Kimombasa, kwa kweli alionekana ni mtu mwenye kufurahia maisha wakati wote, baada ya maongezi ya hapa na pale, alitufungulia geti na kuingia ndani.

Ndani ya lile jumba la kifahari kulikuwa na eneo kubwa la wazi ambalo lilipandwa bustani ya maua na nyasi fupi za kijani kibichi, upande wa kaskazini kulikuwa na bwawa dogo la kuogelea sanjari na viti vichache vya kukalia vilivyokuwa chini ya miavuli midogo mahususi kwa kivuli, mbele ya nyumba hiyo kulikuwa na magari ya bei mbaya yaliyoegeshwa sehemu maalum kwa ustadi mkubwa.

“Hapa ndipo utakapofanya kazi,” hatimaye Mariamu aliniambia.

 “Pazuri sana”

“Ndiyo ni pazuri, hata mshahara utakaolipwa utakuwa mnono, mradi uwe tayari kukabiliana na changamoto zitakazokukabili” aliposema hayo taswira ya kubakwa, ikanijia.

Wakati huohuo alitokea mwanamke mmoja wa Kiarabu  aliyekuwa na sifa zote za kuitwa mrembo, pamoja na uzuri wake lakini midomo na macho yake yalinijulisha kuwa mtu yule alikuwa ni wa aina gani. Majivuno na dharau.

  “Asalam aleykum” alitusalimia

  “Waleykum salam”

 “Huyu ndiye yule mtu mweusi kutoka Tanzania?” alisema. Kauli ile ilinifanya niendelee kuamini kuhusu fikra zangu juu ya tabia ya yule mwanamke wa Kiarabu.

  “Ndiye” Mariamu alimjibu.

  “Mmepima na mmeona hana Ukimwi”

   “Hana?”

   “Ebola na Tb je?”

  “Hana pia”

 “Piteni ndani” alisema yule msichana.

 “Huyu anaitwa Zakia Almajidi mke wa Abadallah Mustapha, ndiye bosi wako mtakayekuwa naye muda wote hapa nyumbani” Mariamu alininong’oneza tukiwa tunaingia ndani.

Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia kisa hiki cha kusisimua katika toleo lijalo.

 

 

 

Sanchoka: ‘Nilimuokota’ Idris Sultan Kwenye Apartment Sauzi, Amfungukia Gigy Money

 

Comments are closed.