The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Al shabaab: Watu watano hatari wasakwa!

0

AlShabaabfighters014.jpgILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Katika mfululizo wa simulizi hii nimeeleza ni kwa jinsi gani kundi korofi na haramu la kigaidi la Al-Shabaab lenye mizizi yake nchini Somalia linavyosumbua Afrika Mashariki na Kati likiwa limeua mamia ya watu hasa Kaskazini mwa Kenya.

Wiki iliyopita tuliona jinsi ambavyo kundi hilo limekuwa likishambuliwa na vikundi mbalimbali vya kijeshi vikiwemo Jeshi la Umoja wa Mataifa (UN), Jeshi la Umoja wa Afrika (AU) vikosi mbalimbali vya Jeshi la Kenya na Somalia. SASA ENDELEA…

Kufuatia mashambulizi ya Al-Shabaab, zaidi ya wakimbizi elfu 7 kutoka Somalia walikimbilia kwenye hifadhi nchini Yemen ambako hata hivyo baadaye walirejeshwa nyumbani wakati bado hali ya amani ikiwa ni tete.

Nicholas Kay, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Somalia alikaririwa akisema kuwa wakati raia hao wakirudi nyumbani, juhudi kubwa zilistahili kuchukuliwa kuhakikisha kuwa Wanamgambo wa Al-Shabaab hawapati uungwaji mkono kutoka kwa waasi nchini Yemen.

Raia hao wa Somalia walirejeshwa nyumbani kuungana na wenzao zaidi ya milioni tatu waliokuwa wakikabiliwa na njaa na vitisho vya Al-Shabaab.

Kay alieleza ni kiasi gani alikuwa na hofu kuwa huenda mashambulizi ya Al-Shabab yangeongezeka ikiwa hatua ya kuondoa majeshi ya Burundi ingechukuliwa nchini Somalia.

Kwa upande wake, Marekani nao walitangaza kupunguza kiasi cha fedha walichokuwa wakitoa kwa majeshi ya Burundi baada ya shutuma kuwa jeshi hilo lilijihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kay aliendelea kusema kuwa majeshi ya Umoja wa Afrika yalihitaji msaada kuweza kupambana na Al-Shabaab.

Wakati hayo yakiendelea, kuliibuka makabiliano makali kati ya vyombo vya usalama na Wanamgambo wa Al-Shabaab yaliyotokea Kaskazini-Magharibi mwa Kenya kwenye Kijiji cha Yumbis na maeneo mengine yaliyopembezoni katika Kaunti ya Garissa ambayo yalikuwa yakilengwa mara kwa mara na wanamgambo hao wa Al-Shabaab.

Shambulio hilo lilifanywa usiku wa manane katika Kijiji cha Yumbis, umbali wa kilomita zaidi ya hamsini Kaskazini-Mashariki mwa Kaunti ya Garissa. Yalikuwa ni mashambulizi mawili yaliyofanyika kwa wakati mmoja.

Gari la polisi lililokuwa likipiga doria lilikanyaga bomu lililotengenezwa kienyeji na baadaye kulifuatiwa na urushianaji wa risasi. Muda mfupi baadaye msafara wa magari ya polisi yaliyotumwa kusaidia ili kuzima shambulio hilo, ulishambuliwa na magari kadhaa yaliharibiwa na Al-Shabaab.

Taaifa kutoka kwa viongozi wa Kenya zilikuwa zikitofautiana ambapo msemaji wake wa polisi, George Kinoti alikaririwa akisema kuwa makumi ya askari walitoweka katika shambulio la kuvizia lililoendeshwa huku akibainisha kwamba oparesheni ya kuwatafuta ilikuwa imeanza kwa kasi.

Lakini tangazo la Mkuu wa Polisi, Joseph Boinett lilithibitisha kwamba kulikuwa na majeruhi na magari matano ya polisi yaliteketezwa kwa moto.

Katika tukio hilo, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alituma rambirambi zake kwa familia zilizowakosa ndugu zao.Hata hivyo, baadaye, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya alitangaza kuwa askari polisi mmoja alikuwa ameuawa na wengine wanne kujeruhiwa vibaya.

Waziri huyo alitaja idadi ya askari ishirini waliouawa iliyokuwa ikitolewa na Al-Shabaab kuwa ilikuwa propaganda ya kundi hilo. Polisi nchini Kenya walitoa picha za watu watano hatari waliokuwa wakitafutwa kwa tuhuma za kupanga mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Ripoti za kiinteljensia zilisema kuwa watu hao ambao walikuwa ni raia wa Kenya baadhi yao ni Shamim Wanjiru Hussein mwenye umri wa miaka 26, Omar Patroba Juma, mchezaji wa zamani wa Klabu ya Soka ya Matahre United, Anwar Yogan Mwok ni miongoni mwa washukiwa waliokuwa wakisakwa.

Akilihutubia taifa, Rais Uhuru Kenyatta aliwaomba Wakenya kuendelea kushirikiana kupambana katika vita ya ugaidi na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuhakikisha kuwa magaidi wanakabiliwa.

Kundi la Kigaidi la Al-Shabaab kutoka nchini Somalia limeendelea kutishia kuishambulia Kenya baada ya Nairobi kutuma jeshi lake nchini humo katika oparesheni iliyopewa jina ‘linda nchi’.

Baada ya hapo kundi hilo la Wanamgambo wa Al-Shabaab limeendelea kuwa tishio kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki hivyo jitihada za kupambana nalo zinaendelea.
MWISHO

Leave A Reply