The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA FAMILIA HII INAUMA!

FAMILIA nyingi nchini huwa zinapata shida mbalimbali lakini simulizi ya familia hii ukiisikia, inauma sana. Ni kwamba msichana Hadija Abduli (21), mkazi wa Kirumba jijini Mwanza yuko katika wakati mgumu kutokana na kuumwa uvimbe kwenye tumbo tatizo alilonalo yapata miaka miwili sasa huku akiwa hawezi kufanya kitu chochote.

Mbaya zaidi ni kwamba watu aliokuwa wakiwategemea wamhudumie ambao ni mama yake mzazi na kaka yake nao wapo kitandani wamelazwa wanaumwa.

 

Akizungumza na UWAZI hivi karibuni, mama wa msichana huyo, Hawa Salehe ambaye amelazwa katika Hospitali ya Gamba mkoani Mwanza akisumbuliwa na maradhi ya moyo pamoja na vidonda vya tumbo alisema kuwa mtoto wake Hadija

alianza kuugua ugonjwa huo yapata miaka miwili iliyopita ambapo alikuwa akilalamika kujisikia maumivu ya tumbo kila siku.

 

Akisimulia zaidi mama huyo alikuwa na haya ya kusema:

“Mwanangu alikuwa akisoma katika Shule ya Sekondari Abuolo, lakini alishindwa kuendelea kutokana na ugonjwa huo kwani tulimpeleka katika Hospitali ya Sekou Toure lakini baada ya vipimo waligundua kuwa utumbo mpana umevimba hivyo walituambia kuwa tumpeleke Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Hatukwenda Muhimbili kutokana na ugumu wa maisha tulionao, hatuna fedha, ilitubidi turudi nyumbani tujifungie ndani maana hutuna kabisa uwezo wowote, maana hata kula yetu ni shida.

 

“Mbaya zaidi baada ya muda mfupi nami nikaanza kuumwa, siku chache baadaye mwanangu wa kiume naye amepata ugonjwa wa kisukari, hivyo sasa hivi wote tumelala kitandani tukiwa wagonjwa.

“Kusema kweli ugonjwa kwa mwanangu Hadija umeongezeka kutokana na kukosa chakula kwani maisha yetu ni shida mno, tunategemea kusaidiwa na watu kwa sababu baba wa watoto hawa alishafariki muda mrefu.

 

“Hakika tumekuwa tukiishi kwa matatizo maana hata sehemu tunayolala haifai kabisa, Hadija ana afya mbaya, nimshukuru dada Flora ambaye ametupigania na kuokoa maisha yetu.

“Mimi bado naumwa na wanangu pia na tumelazwa Hospitali ya Gamba kwa msaada wa huyu dada Flora, bado tunahitaji msaada kwani gharama ya tiba ikiwa pamoja ya kufanyiwa upasuaji ni mamilioni ya shilingi, tutapata wapi fedha hizo sisi masikini?” alisema mama huyo huku akifuta machozi kwa khanga.

 

Kwa yeyote aliyeguswa na simulizi ya mama huyu anaweza kumsaidia chochote ulichonacho kwa kutumia namba ya simu 0759 665 555.

STORI: IMELDA MTEMA, UWAZI

Comments are closed.