The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya JB: filamu zake Jerusalem

0

JB1.gif“Ngoja nikwambie kitu kimoja. Kuna vijana wengi siku hizi wanaweza kukufuata na kukwambia kwamba wanataka kuigiza, sawa, ila ukiwauliza kwa nini wanataka kuigiza, wanakwambia ni kwa sababu wanataka kuwa maarufu, basi,” anasema JB kisha anakunja sura kidogo hali iliyonifanya nishtuke, nikajiweka vizuri kitini. Akaendelea:

“Huwa sipendi kufanya kazi na watu wanaotaka umaarufu halafu iwe basi. Uigizaji kwa sasa ni ajira, tunahitaji waigizaji ambao vichwa vyao vinawaza kutoka kimaisha na si kuwa maarufu halafu basi.”

Wakati amesema maneno hayo, mara simu yake inaanza kuita, anachokifanya ni kuichukua kutoka pale mezani alipoiweka na kuanza kukiangalia kioo kisha kuirudisha mezani pasipo kuzungumza chochote.

“Unapoamua kumwambia mtu ukweli kwamba hatakiwi kuhitaji umaarufu, anatakiwa kuangalia fedha, umaarufu utakuja tu endapo utafanya vitu vizuri, yaani uigizaji wako ukishakuwa mzuri, umaarufu haukwepeki, mbona Gabo amekuwa maarufu, aliigiza filamu moja, akatoka, cha kwanza ni kupiga kazi,” anasema JB na kuendelea:

“Baadaye mimi na kampuni yangu ya Jerusalemu tukaendelea kufanya kazi, katika kipindi hicho ndipo nikaamua kuwavuta wasanii wengine ili kuongeza nguvu katika kampuni ile, mtu wa kwanza ambaye alinijia kichwani alikuwa marehemu Adam Kuambiana.

“Nilikuwa namwamini sana jamaa, alikuwa anajua, kumuacha hivihivi lilikuwa jambo gumu, ni sawa na kuacha kipande cha dhahabu jangwani. Mbali na yeye, nikamchukua Shamsa Ford pia nikataka nimtoe msanii asiyekuwa na jina, hivyo karata yangu ikaangukia kwa huyu Gabo,” anasema JB kisha kutoa tabasamu pana kama mtu aliyefurahishwa na jambo fulani.

“Uigizaji ni kazi nyepesi kama utaigiza na watu wanaojua, nilipomchukua Gabo, nikaigiza naye katika filamu ya Bado Natafuta. Ninaposema jamaa anajua, ieleweke tu kwamba anajua. Alipatia sana na ndiyo filamu ambayo ilimtangaza, ikawafanya wadau wajue Gabo ni nani na anafanya nini.

“Unajua katika maisha yetu, unapoamua kumfanyia kitu kizuri mfanyakazi wako basi jua kwamba hata kazi zako atazifanya zinavyotakiwa. Nilichokifanya ni kuanza kuwalipa mishahara waigizaji waliokuwa hapo Jerusalem. Haikujalisha kama waliigiza filamu au la, nilichokifanya ni kuwalipa mishahara, yote hayo ni kuwaonyeshea kwamba niliwajali,” anasema JB. Anabaki kimya kwa sekunde kadhaa, anachukua simu yake na kuanza kuandika meseji huku nikibaki kimya nikimwangalia.

“Unajua kuna kipindi kilifika, nikabadili kabisa maisha yangu katika uigizaji, kampuni yangu ilianza kuwa kubwa, hivyo nilichokifanya ni kuzigawa filamu zangu kwenye makundi mawili, kundi la kwanza lilikuwa ni ‘low budget’ yaani bajeti ya chini na kundi jingine ni ‘high budget’ yaani bajeti ya juu.

“Kwenye zile filamu za bajeti ya juu ni zile ambazo mimi mwenyewe naigiza kama Mzee wa Swaga na Shikamoo Mzee. Hizi ndizo ambazo natumia fedha nyingi kwani ni lazima niigize na staa yeyote mkubwa.

“Katika kundi la bajeti ya chini kuna filamu kama Bado Natafuta na Chausiku, filamu hizo huwa ninabaki na kuwa muongozaji tu. Huwa ninajipanga sana mpaka ninatoa filamu mtaani na ndiyo maana watu wengi wanapongeza ubora wa filamu zangu,” anasema huku tabasamu likiongezeka usoni mwake.

“Watu wengi walitarajia kwamba ungekuwa mrithi wa marehemu Steven Kanumba kwa kuigiza filamu nyingi na waigizaji wa nchi nyingine lakini watu wakaona kimya, kwa nini? Unaogopa au?” nikamuuliza swali hilo kama kumtega, nilitaka kusikia jibu lake lingekuwa lipi. Cha kushangaza, akaongeza tabasamu lake usoni na kuniambia:

“Swali zuri sana,” anasema.

Itaendelea wiki ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply