The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 18

0


MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:

Hakukuwa na muda wa kupoteza, mwenye nyumba alipigiwa simu, akaja na kuandikishiana mkataba ambao sasa pale kwenye jina la mpangaji, liliandikwa jina langu na hata sahihi niliweka ya kwangu, yule mwenye nyumba akawa ananitazama kwa macho ya chinichini, nadhani akiwa haamini kama mimi ndiyo mhusika mwenyewe kwa sababu nilikuwa sifanani kabisa na ‘fujo’ zile za fedha.

SASA ENDELEA…
Baada ya kukamilisha kila kitu, Bonta alitoa fedha, wakahesabiana pale kisha tukakabishiwa funguo, mwenye nyumba akaondoka zake akiwa anachekacheka tu mwenyewe.

Kwa kuwa nyumba ilikuwa safi sana, hakukuwa na haja ya kufanya usafi, Bonta akamuagiza dalali atafute watu wa kutusaidia kushusha vyombo, tukatoka mpaka barabarani kumchukua yule dereva wa ‘Canter.

Tuliporudi naye mpaka pale kwenye ile nyumba, tayari vijana wenye nguvu kama sita hivi walikuwa wameshajipanga, wanasubiri kushusha mizigo. Kazi ikaanza ambapo Bonta alinisaidia kupanga namna vitu hivyo vitakavyopangiliwa mle ndani.

Kazi ikafanyika haraka na mpaka inafika saa kumi na moja, kila kitu kilikuwa kimeshakamilika, akaniambia twende tukajipongeze kidogo kwenye baa iliyopo jirani, tukafunga vizuri milango na kutoka naye mpaka barabarani, tukaingia kwenye Bajaj na kumuelekeza dereva atupeleke sehemu aliyomtajia ambayo sikuwa naijua.

“Maisha yenyewe mafupi haya, jiachie mdogo wangu, kula bata!” alisema wakati tukiondoka na Bajaj, nikaishia kucheka tu. Moyoni nilijiona kuwa na deni kubwa kwa Bonta mwenyewe na kubwa zaidi kwa Bosi Mute, nikajiapiza kwamba nitafanya chochote atakachoniagiza, hata kama kitakuwa ni cha hatari kiasi gani.

Safari yetu iliishia kwenye Baa ya Cheers, iliyopo Sinza Mori, tukateremka kwenye Bajaj, akamlipa dereva fedha zake kisha tukaingia ndani ya baa hiyo iliyokuwa imechangamka kwelikweli. Tulienda mpaka kwenye moja ya meza zilizokuwa ndani kabisa, kwenye kona.

Tulipokaa tu, wahudumu wa kike kama wanne hivi walitufuata na wote wakawa wanamkumbatia na kumbusu Bonta. Ilionesha ni kama wanamfahamu vizuri, basi naye akawa anawachangamkia.
“Huyu ni mdogo wako nini?”

“Mdogo wangu ndiyo, muacheni bado anasoma,” alisema, wakacheka sana na kugosheana mikono, mmoja akanisogelea na katika hali ambayo sikuitarajia, alinikalia kwenye mapaja yangu, akanibusu mdomoni halafu akaninong’oneza:

“Usiogope, hata kama unasoma mimi sitakupokonya madaftari yako.”
Nilijikuta nikiishia kucheka tu, basi akainuka na kuanza kusikiliza oda iliyokuwa inatolewa na Bonta. Wawilikati yao, walivuta viti na kukaa na sisi, wale wengine wawili wakaenda kutuletea oda zetu kama Bonta alivyoagiza.

Muda mfupi baadaye, meza yetu ilikuwa imejaa vyakula na vinywaji. Bonta akawa ananihimiza nile, kunywa, kucheza muziki na hata kama nitataka mwanamke wa kwenda kulala naye mpaka asubuhi, hakuna tatizo. Kiukweli hayakuwa mazingira niliyoyazoea lakini nilijilazimisha kwenda naye sawa ili nisije kuonekana mshamba.

Nilikula kwanza maana nilikuwa na njaa, nikamfakamia kuku wa kuchoma na chipsi mpaka nikashiba kisawasawa, chupa mbili za bia zikafunguliwa kwa mpigo na kusogezwa mbele yangu. Nilianza kunywa lakini kwa tahadhari kubwa ili nisije nikalewa, stori za hapa na pale zikawa zinaendelea.

Mara kwa mara Bonta alikuwa akigusanisha ndimi na yule mhudumu aliyekaa pembeni yake, wakati mwingine akiingiza mkono wake kwenye sketi yake bila hofu. Yalikuwa ni mambo mageni sana kwangu lakini kama nilivyosema, nilijitahidi kutoshangaa sana, nikawa najifanya kama ni mambo ya kawaida kwangu.

Yule mhudumu mwingine aliyekuwa amekaa pembeni yangu, naye alikuwa akinifanyia vituko vya kila aina, lakini nikawa najitahidi kuvishinda vishawishi kwa sababu ukweli ni kwamba sikuwa namjua mwanamke mpaka katika umri huo.

Nilijikaza na kumaliza chupa ya kwanza, nikaanza kuhisi kichwa kinazunguka. Nikaianza ile chupa ya pili na muda mfupi baadaye, tripu za kwenda chooni zilianza, wanywaji wa pombe watakuwa wanajua vizuri ninachomaanisha. Kadiri nilivyokuwa nikiendelea kunywa, ndivyo kichwa kilivyokuwa kikizidi kuzunguka na ndivyo safari za kuelekea chooni zilivyoongezeka.

Nilikuwa nikibanwa na haja ndogo mara kwa mara. Nilimaliza chupa ya pili, zikafunguliwa nyingine mbili, nikaendelea kunywa huku nikijitahidi nisitapike kwani kuna hali isiyo ya kawaida niliianza kuisikia. Ilifikia mahali, nikisimama kwenda chooni napepesuka kwelikweli, yule mhudumu mmoja akawa ananisaidia.

Muda ulizidi kuyoyoma, watu wakazidi kuongezeka kwenye ile baa, muziki nao ukawa unapigwa kwa sauti ya juu huku Bonta akifakamia pombe kama hana akili nzuri. Nilipomaliza chupa nne, tayari nilikuwa ‘nime-flot’, nikaanza kusikia usingizi mzito na haukupita muda, nikalala kwenye meza.

Bonta akawa anacheka sana huku akiniambia kwamba nisijali, nitazoea taratibu. Baadaye sikuelewa tena kilichoendelea, nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nikiwa juu ya kitanda, pale kweye makazi yangu mapya. Nilikuwa nimelala na nguo zangu zote vilevile, na kibaya zaidi, nilikuwa pia nimelala na viatu.

Nilikurupuka kitandani na kusimama, bado nilikuwa na pombe kichwani kwa hiyo nikawa napepesuka. Nilijaribu kuvuta kumbukumbu nimefikaje pale? Kumbukumbu zangu ziliishia pale tulipokuwa kule baa, nikiwa nimelewa sana.

Nilisogea dirishani na kuchungulia nje, kulishaanza kupambazuka! Nikatingisha kichwa na kujisikitikia. Nilitoka mpaka sebuleni, nikakuta kuna hotpot limewekwa mezani huku chini yake kukiwa na kikaratasi kilichokuwa na ujumbe.

“Ukiamka kunywa hii supu, kuna soda za kupunguza pombe kwenye friji na maji, kunywa vyote utajisikia vizuri. Pumzika mpaka nitakapokuja kukuchukua,” ulikuwa ni ujumbe ulioandikwa na Bonta kwani chini kabisa aliandika jina lake.

Nilifanya kama alivyoniambia, nilifunua lile hotpot kubwa na kukuta kuna supu imejaa, ikiwa na nyama kibao. Nikafakamia harakaharaka na baadaye nilienda kwenye friji. Japokuwa lilikuwa jipya, lakini lilishaunganishwa kwenye umeme na kuwashwa.

Nililifungua, nikakuta kuna chupa mbili za zile soda nyeupe na chupa nyingine mbili za maji makubwa. Nilifungua soda moja na kuanza kuinywa. Kwa wale waliowahi kunywa zile soda za kupunguza uchovu wa pombe (club soda) watakuwa wanaeleza jinsi zilivyo na ladha mbaya mdomoni.

Nilijilazimisha tu kwa sababu bado nilikuwa nimelewa. Nikanywa ya kwanza na kushushia na chupa nzima ya maji. Angalau sasa nilikuwa najisikia vizuri, nilirudi chumbanim nikavua nguo na kuingia bafuni, nikafungulia ‘bomba la mvua’ na kuanza kujimwagia maji.

Kiukweli nilijisikia raha sana kwa sababu hayo ndiyo maisha niliyokuwa nayaota siku zote. Baada ya kuoga, angalau sasa nilikuwa najisikia vizuri, nikatoka na kuanza kuzungukia nyumba yangu kukagua vitu vilivyonunuliwa kwa ajili yangu.

Kila nilichokuwa nakitazama, nilikuwa nikiishia kuchekacheka tu mwenyewe, nikaenda kukaa kwenye masofa mapya pale sebuleni. Haukupita muda, nikapitiwa tena na usingizi kwani bado nilikuwa na uchovu.

Kilichonizindua, ilikuwa ni mlango wa geti uliokuwa ukifunguliwa, nikafunua pazia na kuchungulia nje, nikamuona Bonta akiingia. Hata sikuwa najua kwamba naye alikuwa na funguo, akaingia na kufungua mlango wa ndani, nikampokea kwa uchangamfu.

“Daah! Mdogo wangu ukilewa unakuwa mkorofi sana,” alisema huku akicheka, akakaa na kuanza kunisimulia vituko vyote nilivyokuwa navifanya jana yake. Niliishia kucheka tu kwa sababu mambo mengine yalikuwa ya aibu.
Aliniambia kwamba bosi amesema siku hiyo nipumzike na kuweka vizuri nyumba yangu.

“Nitakuja kukuchukua kesho asubuhi, funguo zako hizo hapo, ilibidi niondoke nazo kwa sababu za kiusalama,” aliniambia huku akinikabidhi funguo alizozitumia kuingilia mle ndani.

Hakukaa sana, akaniaga na kuinuka huku akinisisitiza kwamba natakiwa kwenda kununua nguo nzuri pamoja na simu. Aliniachia bunda la hela pale mezani, basi nikamshukuru sana na kumsindikiza, alipotoka, nilifunga geti kwa ndani na kurudi tena ndani.

Nilianza kwa kuunganisha TV na redio kwa sababu nilikuwa nahitaji kitu cha kuchangamsha nyumba. Sikupata taabu sana kwa sababu kabla baba hajapatwa na haya matatizo, nyumbani tulikuwa na kila kitu. Baada ya kumaliza kuunganisha, ilibakia kazi ya kumtafuta fundi wa kuja kufunga ‘dish’ na vitu vingine vidogo.

Niliendelea kuweka vitu vizuri, nikahakikisha kila kitu kipo kwenye mpangilio safi, kisha nikaoga tena na kutoka kwa ajili ya kwenda kununua simu na nguo kama Bonta alivyoniambia.

Sikuwa mwenyeji wa mitaa ya Sinza kwa hiyo nilitakiwa kuwa makini. Nilitoka mpaka barabarani na uzuri wake ni kwamba kulikuwa na maduka mengi na kila kitu kilikuwa kinapatikana hapohapo.

Baada ya ‘shopping’ ya nguo kadhaa na viatu, nilimalizia na simu, kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikanunua simu ya kisasa (smartphone), nikasajili laini na kununua vocha, kisha nikapitia chakula na kurudi nyumbani.

Ilikuwa ni siku ya furaha mno kwangu, yaani nilijiona kama maisha nimeshayapatia. Niliweka laini kwenye simu, nikawa naisetiseti pale wakati fundi akiendelea kuniunganishia ‘dish’ ili nianze kufaidi utamu wa runinga kubwa (flat screen) na baada ya muda, tayari nilikuwa hewani.

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply