The House of Favourite Newspapers
gunners X

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 19

0


MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:
Baada ya ‘shopping’ ya nguo kadhaa na viatu, nilimalizia na simu, kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikanunua simu ya kisasa (smartphone), nikasajili laini na kununua vocha, kisha nikapitia chakula na kurudi nyumbani.

Ilikuwa ni siku ya furaha mno kwangu, yaani nilijiona kama maisha nimeshayapatia. Niliweka laini kwenye simu, nikawa naisetiseti pale wakati fundi akiendelea kuniunganishia ‘dish’ ili nianze kufaidi utamu wa runinga kubwa (flat screen) na baada ya muda, tayari nilikuwa hewani.

SASA ENDELEA…
Nikawa naperuzi simu, huku nikijipiga ‘mapichapicha’ nikiwa mle ndani. Japokuwa chakula nilikuwa nimenunua wala sikuwa na haraka, akili zangu zote zilikuwa kwenye simu na TV. Fundi alimaliza kuunganisha ‘dish’ kule juu ya nyumba, nikamlipa fedha zake na kuondoka, akaniacha nikiwa naendelea kujitanua pale sebuleni.

Nilisikiliza muziki, nilitazama runinga, nilichezea simu na kugalagala kwenye masofa, basi ikawa raha tupu. Muda uliyoyoma kwa kasi, giza likaanza kuingia, nikatoka tena na kwenda kununua chakula na kurudi ndani, nikajifungia na kuendelea kuchekelea mafanikio niliyopata. Laiti kama Mungu anetupa binadamu uwezo wa kuona jambo linaloweza kukutokea hata kesho tu, hata sijui ingekuwaje. Nilikuwa nafurahia lakini sikuwa najua ni nini kilichopo mbele yangu.

Basi siku hiyo ilipita, nikalala usingizi mnono pengine kuliko siku yoyote maishani mwangu. Kesho yake asubuhi niliwahi kuamka na kuanza kujiandaa, nikavaa nguo zangu mpya na viatu na kunifanya nipendeze sana.

Muda mfupi baadaye, nilisikia pikipiki la Bonta likinguruma nje ya geti, akapiga honi na harakaharaka nilizima kila kitu na kuiacha nyumba yangu kwenye mazingira salama, nikatoka mpaka nje na kukutana na Bonta.

Alinisifia sana kwa jinsi nilivyokuwa nimependeza, nikapanda kwenye pikipiki na safari ya kuelekea kazini ikaanza. Njiani tulikuwa tukipiga stori za hapa na pale mpaka tulipofika. Tulipoingia tu, tulikuta kuna magari mawili aina ya Landrover Defender kama zile zinazotumiwa na polisi zikiwa zimepaki.

Mwanzo niliogopa lakini nilipoona Bonta wala hashtuki, nilipiga moyo konde. Tuliingia mpaka ndani na muda mfupi baadaye, bosi Mute aliwaita watu wote kwenye chumba cha mikutano. Upande wa chini wa ile gereji kulikuwa na ukumbi mkubwa, wote tukaingia.

Bosi Mute akatueleza kwa kifupi tu kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya kazi, kwa hiyo wote watakaochaguliwa kwa ajili ya kazi, wanatakiwa kuelekea uwanja wa mazoezi kwa ajili ya maandalizi. Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza kwa mafumbo, hata sikuelewa alikuwa akimaanisha nini.

Basi baada ya hapo, Bosi Mute alitoka na kuacha jukumu la kuchagua nani na nani waende kwenye kazi, kwa viongozi wengine. Bado sikuwa najua jinsi ngazi za uongozi zilivyokuwa ila nilichogundua ni kwamba Bonta naye alikuwa ni miongoni mwa viongozi.

Basi watu wote tuliamriwa kukaa katika mistari miwili. Kulikuwa na zaidi ya watu hamsini mle ndani, kuanzia vijana wadogo kama mimi, vijana wakubwa na wenye miili mikubwa kama Bonta na wazee wachache. Basi ilianza kazi ya kuchaguana pale na baada ya muda, watu 12 tulichaguliwa na mimi nikiwa miongoni mwao.

Wale wengine waliruhusiwa kuendelea na kazi, sisi tukaelekezwa kwenda kwenye yale magari pale nje yaliyokuwa yanatusubiri. Mimi niliingia kwenye gari la nyuma, baada ya wote kuingia, msafara wa yale magari mawili na kigari kingine kidogo (carry), vile vinavyotumia kubeba mizigo, uliianza safari ya kuelekea huko mazoezini.

Tulipofika mbele kidogo, magari yaliachana, kila moja likapita njia yake, la kwetu lilipita ile njia ya siku zote na tukaenda kutokezea Mombasa, likakata kona kushoto na kuwa linaelekea Gongo la Mboto. Tulipita Gongo la Mboto, safari ikaendelea mpakakwenye Msitu wa Kazimzumbwi.

“Tumefika guys,” alisema mmoja kati ya watu waliokuwa wamekaa kule mbele wakati akiakata kona na kuiacha barabara ya lami, tukaingia ndani ya msitu huo mpaka ndanindani kabisa. Nilishangaa kugundua kwamba yale magari mengine mawili, yalishafika kabla yetu na kupaki na watu wote kuteremka.

Baada ya wote kuteremka kwenye gari, tulipangwa kwenye mstari mmoja, mwanaume mmoja aliteremka kutoka kwenye lile gari dogo (kirikuu), akatusogelea na kuanza kututazama mmoja baada ya mwingine usoni.
Alikuwa kimya kabisa huku akiwa ‘sirias’ sana, uso wake ukiwa na ndita kibao. Akawa anatutazama mmoja baada ya mwingine usoni na kuhamia kwa mwingine.

“Guys, kutaneni na Mamba, huyu ndiyo mwalimu wa somo letu la leo,” alisema Bonta huku mara kwa mara akinitazama. Yule mwanaume alisogea mbele na kwa muda wa kama dakika mbili hivi, alikuwa kimya kama anayefikiria aanzie wapi.

“Naitwa Mamba! Hapa tumekuja kazini, ambaye anajiona hawezi kazi ni bora aseme mapema, vinginevyo ataliwa na mamba,” alisema kwa sauti nzito na kavu.

Baada ya kusema maneno hayo, alitoa ishara kwa watu waliokuwa ndani ya like gari dogo, wanaume wanne wakateremka, nikawa najiuliza walitoshaje kwenye kigari kidogo kama kile?
Waliteremsha masanduku mawili ya chuma kutoka kwenye kile kigari, wakayasogeza mpaka pale tulipokuwa tumejipanga.

 

Yule mwanaume aliyejitambulisha kama Mamba, japokuwa sijui kama lilikuwa jina lake halisi au la, alifungua sanduku la kwanza, akainama huku akitutazama usoni, akawa ni kama ameshika kitu ndani ya lile sanduku lakini anatupima kuona tutafanya nini atakapokitoa.

Lahaula! Aliinuka na bunduki, zile ndefu kama zinazotumika vitani, akaikoki na kuikamata kama anayetaka kufyatua risasi. Hofu niliyoipata ilikuwa kubwa mno, bado kidogo nitokwe na haja ndogo, bunduki inatisha sana, isikieni tu.
“Hiki ndiyo kifaa cha wanaume! Nikisema wanaumee, wote mnaitikia eeeh! Wanaumee!”
“Eeeh!” wote tuliitikia. Sijui kama na wenzangu walikuwa na hofu kama yangu kwa sababu nakumbuka hata hiyo itikia yangu yenyewe, ilikuwa ni ya sauti ya kutetemeka.

“Wanaumeee!”
“Eeeh!”
“Nimewaambia kwamba hapa tumekuja kazini! Kama kuna mtu anamkumbuka mama yake bora aondoke sasa hivi akamsaidie kuchambua matembele,” alisema Mamba. Nilichojifunza ni kwamba alikuwa na maneno ya shombo sana, ambayo yanaweza kukufanya ukajikuta unapatwa na ujasiri kuliko kawaida.

Mpaka muda huo, niliona kama nikiendelea kutetemeka, naweza kuambiwa mimi ni mtoto wa mama, kwa hiyo nikawa najikaza huku nikiwa makini kufuatilia kila kitu.

“Hii inaitwa manati ya mzungu! Wangapi wamewahi kuitumia?” alisema, wachache kati yetu wakainua mikono juu. Kumbe miongoni mwetu kuna watu walishawahi kutumia bunduki, nikawa najiuliza walizitumia wapi, ilikuwaje, inafananaje ukiibeba? Ni kweli niliona bunduki kule kwa Bonta lakini yenyewe ilikuwa ndogo siyo kama ile aliyoishika Mamba.

“Unapoishika, kwanza hutakiwi kuchekacheka kama mtoto wa kike, lakini pia unatakiwa kuwa makini sana kwa sababu uzembe kidogo tu, tena wa sekunde moja tu, unatosha kukubadilisha jina, ukaitwa marehemu,” alisema huku akitembea nayo, safari hii akiwa ameinyanyua na kuielekeza juu, akawa anatusogelea mmojammoja.
Baada ya kuzungukazunguka, alirudi pale kwenye yale masanduku, akaikoki na kutoa risasi ambazo alizikinga kwenye mkono wake, akairudisha kwenye lile sanduku.

“Ili manati ifanye kazi inatakiwa kuwa na nini?”
“Jiweee!” tulijibu wote, akazichambua zile risasi na kuishika moja, akaiinua juu, akatwambia manati ya mzungu haitumii mawe ya kawaida, bali inatumia mawe ya dukani.

“Hii moja inatosha kabisa kuyakatisha maisha yako! Lakini pia inatosha kuyalinda maisha yako,” alisema Mamba na kuanza kutufundisha jinsi bunduki inavyofanya kazi.

Alitufundisha kwanza kwa maneno huku akituonesha, akatufundisha namna ya kuweka risasi kwenye bunduki na kuzitoa, pia akatufundisha namna ya kuikoki, yaani kuzitoa risasi kwenye ‘magazini’ na kuziweka kwenye ‘chemba’, waliowahi kutumia bunduki watakuwa wananielewa.

Ili risasi ifyatuke, lazima kwanza uikoki bunduki na kile kitendo cha kukoki ndiyo kinachozitoa risasi kwenye ‘magazini’ na kuziweka kwenye ‘chemba’, tayari kwa kufyatua.

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Kwa shilingi 6,000 tu unaweza kupata simulizi yote kwa mfumo wa softcopy, piga 0719401968. Pia ukitaka kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

 

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply