SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS(SAA ZA GIZA TOTORO)-30

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

“Mkienda naye kwenye kazi kuwa makini, anaweza kukufanyia makusudi kulipa kisasi, nitajaribu kuzungumza naye kabla hamjaondoka, najua namna ya kumtuliza,” alisema, akaniachia na kuanza kuvaa nguo zake, na mimi nikavaa za kwangu na kuanza kujiandaa kama alivyoniambia.

SASA ENDELEA…

Harakaharaka Kezia alinibusu tena na kwenda kufungua mlango, akatoka na kuniambia anataka kabla hatujaondoka tuonane, nikatingisha kichwa kumkubalia, moyoni nikaanza kuwa na hofu kwa sababu kweli Gamutu angeweza kunifanyizia.

 

Baada ya kumaliza kujiandaa, nilitoka na kuelekea kule kwenye uwanja wa mazoezi, nikawakuta baadhi ya watu wakiwa wameshafika, muda mfupi baadaye Gamutu akaja akiwa ameongozana na Bonta.

 

“Zungumza naye!” alisema Gamutu huku akimuonesha ishata Bonta eti azungumze na mimi, nilishajua kinachoendelea, basi nikawa mpole maana nilijua nikiendelea kuleta ujeuri, kinachoweza kunikuta ni kibaya sana.

 

“Vipi mdogo wangu,” alisema Bonta huku akinishika begani kirafiki kama kawaida yake, tukasogea pembeni ambapo aliniambia kwamba amepelekewa mashtaka na Gamutu kwamba namuingilia kwenye anga zake. Nilikubali kila kitu kwa sababu hata Bonta mwenyewe alikuwa anajua kinachoendelea na yeye ndiye aliyechomekea ishu ya ukaribu kati yangu na Kezia.

 

“Sikia mdogo wangu, huyu jamaa huwa ana visasi sana, we achana na yule msichana, kama unashindwa kumuacha basi fanyeni mambo yenu kwa siri, anaweza kukufanyia kitu kibaya maana siyo mtu mzuri,” alisema Bonta, basi nikawa natingisha kichwa kwa unyenyekevu kumuonesha kwamba nimemuelewa.

 

Kwa kuwa muda wa mazoezi ulishafika, tulianza kupewa maelekezo ya nini cha kufanya na aliyekuwa akitoa maelekezo hayo, alikuwa ni Gamutu, mara kwa mara akawa ananikata jicho baya na mimi nikawa nainamisha kichwa chini kwa sababu sikutaka aone kama ‘namvimbia’.

 

Alitupa mchongo wa kazi nzima, ilikuwa ni kazi ya kwenda kuvamia nyumbani kwa mfanyabiashara mmoja mkubwa jijini Dar es Salaam aliyekuwa akiishi Kunduchi na kulikuwa na taarifa kwamba ameingiza nchini fedha kibao za kigeni lakini ameshindwa kuzipeleka benki akihofiwa kukamatwa kwa kesi ya utakatishaji wa fedha haramu.

 

“Bosi Mute anazitaka fedha zote leoleo na mimi nimeamuahidi kwamba zitapatikana, sasa asitokee kenge yeyote wa kufanya uzembe kutaka kutukwamisha,” alisema Gamutu huku safari hii akiwa amenikazia macho mimi, nikajua kazi imeanza.

 

Ilikuwa ni mapema mno kwangu mimi kuingia kwenye ‘mabifu’ ya kugombea wanawake na wakubwa zangu, moyoni nikajiapiza kwamba kama hilo likipita salama, sitaki tena kuwa karibu na Kezia.

 

Tulielekezwa kila kitu kinachotakiwa kufanyika, tukaoneshwa na ramani ya nyuma yenyewe na jinsi walinzi wanavyojipanga. Tulipewa vifaa muda huohuo, ikiwa ni pamoja na makoti mengine pamoja na silaha, Gamutu akasisitiza kwamba kila mmoja akatulie kwenye chumba chake kusubiri muda wa kazi.

 

Baada ya hapo, tulitawanyika na kila mmoja akaelekea kwenye chumba chake, wakati tukiondoka Bonta alinikonyeza na kunipa ishara fulani, nikamuona akimfuata Gamutu, wakaondoka pamoja.

 

Mle ndani kutembea na silaha halikuwa jambo la ajabu kwa hiyo na mimi nilibeba bunduki yangu na kwenda nayo ndani kwangu pamoja na vile vifaa vingine nilivyopewa. Nikaenda kujitupa kitandani nikiendelea kutafakari mambo mengi ndani ya kichwa changu.

 

Muda uliyoyoma na hatimaye kigiza kikaanza kuingia, Kezia jinsi asivyo muoga, mishale ya kama saa moja hivi, alikuja tena chumbani kwangu huku akiwa amechangamka kama kawaida yake. Akaniambia ameshazungumza na Gamutu ila amemwambia atampa majibu atakaporudi usiku.

 

“Wala usiwe na wasiwasi ila cha msingi ni kuwa naye makini tu mkiwa kwenye kazi,” alisema Kezia, akanibusu na kunitakia kila la heri kisha akaondoka zake. Chakula kilikuja, nikala harakaharaka na baadaye, nilisikia filimbi ikipulizwa, kama Gamutu alivyokuwa ametuelekeza, nilitoka harakaharaka nikiwa nimeshajikoki na kwenda mpaka kule kwenye lile jengo kubwa ambako tuliambiwa ndiyo sehemu ya kuondokea.

 

Nilipofika, nilikuta magari mawili, Toyota Noah yote ya rangi nyeusi yakiwa yameshapaki, wenzangu wakawa wanaingia na mimi nikajichanganya na kuingia. Tuliondoka watu kumi na mbili, sita kwenye kila gari na kati ya wote hao, ni mimi peke yangu ndiye niliyeonekana kuwa mdogo.

 

Hata kabla ya kuambiwa chochote, nilijua kwamba lazima kazi itakuwa ngumu na ndiyo maana wanaondoka wakongwe watupu, isipokuwa mimi tu. Nilifarijika sana kugundua kwamba Bonta naye ni miongoni mwa tunaoenda nao.

 

Kutoka Kibaha mpaka Kunduchi, tulitumia muda wa kama dakika arobaini tu, tukawa tumeshafika kwani madereva walikuwa wakiendesha kwa kasi utafikiri tupo kwenye mashindano.

 

Tulienda kupaki kwenye eneo moja la wazi lililopo ufukweni kabisa mwa bahari, upande wa kushoto kulikuwa na makaburi ambayo baadaye niliambiwa kwamba ni makaburi ya Wagiriki.

 

Tulipofika, wote tulishuka kwenye magari, gamutu akarudia tena kutupa maelekezo ya mwishomwisho, akasema inabidi tuvutevute muda kidogo maana ilikuwa bado mapema. Muda huo ilikuwa ni karibu saa tano za usiku.

 

Basi wengine walianza kuvuta ‘mibange’ pale ufukweni, wengine wakawa wanakunywa pombe kali lakini mimi sikutaka kutumia kilevi chochote, tishio la Gamutu lilinifanya nitamani muda wote kuwa timamu.

 

Tulivutavuta muda mpaka ilipofika saa saba, Gamutu akatoa ishara na wote tukaingia kwenye magari, tukatoka na safari hii magari yalikuwa yakienda mwendo wa taratibu, tukielekea kwenye makazi ya mfanyabiashara huyo ambaye baadaye nilikuja kugundua kwamba anaitwa Subash, ana asili ya India.

 

Tulipokaribia kwenye hekalu lake, tuliteremka kwenye magari, Gamutu akaanza kutupanga namna ya kuingia, cha ajabu eti alinipanga mimi na yeye tupite njia moja, hofu ikazidi kutanda kwenye moyo wangu.

 

Mle kwenye magari tuliwaacha madereva tu ambao nao walikuwa wameyawasha magari na kuyaweka ‘silensa’, kwa wanaojua kuendesha magari watakuwa wananielewa.

 

Tulitawanyika na kuanza kusonga mbele kwa tahadhari kubwa kuelekea kwenye jengo hilo, tukiwa tumelizunguka, wakati tunakaribia, niliamua kuikoki bunduki yangu ili kuzijaza risasi katika ‘chemba’, tayari kwa chochote.

 

Katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa ikigoma kuikoki, nikahisi labda nilikuwa sijatoa ‘safety lock’, nikahakikisha lakini hakukuwa na tatizo, nikajaribu tena kuikoki lakini wapi. Kijasho kikaanza kunitoka, muda huohuo Gamutu alitoa amri ya kuanza kushambulia, milio ya risasi ikaanza kurindima lakini ya kwangu ilishindwa kabisa kutoa risasi hata moja.

 

Walinzi waliokuwa wamejipanga, nao wakiwa na silaha za moto, walianza kujibu mashambulizi, mimi nikawa bado nahangaika na bunduki yangu huku Gamutu akiwa ametangulia na kuniacha nyuma nikihangaika, akili ikanituma kuchomoa ‘magazini’ ili niichomeke vizuri.

 

Nilishtuka sana kugundua kwamba ‘magazini’ yangu ilikuwa tupu, haikuwa na risasi hata moja, nikajua lazima aliyenifanyia mchezo huo ni Gamutu kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akigawa bunduki.

 

Nilijiona mzembe sana kwa kushindwa kuikagua tangu tukiwa kule kambini, nikiwa bado sielewi nini cha kufanya, nilishtukia tukimulikwa na taa kali iliyokuwa kwenye mnara wa mbele wa lile jengo, kisha risasi zikaanza kumiminwa kwa kasi kuelekea pale tulipokuwepo, nikazidi kuchanganyikiwa huku nikiwa sijui nini cha kufanya.

 

Akili zilinituma kulala chini maana sikuwa na ujanja tena, bunduki haina risasi halafu tunashambuliwa. Basi nilibinuka kikomando na kuangukia pembeni ya maua, mahali ambapo nilijua hata wakipiga risasi vipi hawawezi kunipata.

 

Kwa kuwa wenzangu walikuwa wakisonga mbele, na mimi niliamua kusonga mbele lakini kwa mfumo tofauti, nilianza ku-craw kama tulivyojifunza kule kambini lakini nilijitahidi kuwa makini nisionekane, nikawa natambaa kufuata mstari wa maua.

 

Mvua ya risasi iliendelea kumiminika kwa kasi, Gamutu akawa anaendelea kupambana kwelikweli huku akisonga mbele. Alichokisema Kezia kweli nilijionea mwenyewe, Gamutu hakuwa na masihara kwenye kazi, alikuwa anatisha kama jinamizi.

 

Muda mfupi baadaye, wale walinzi waliacha kujibu mashambulizi, nadhani waliona hawawezi kupambana na moto wetu. Tayari tulikuwa tumeshafika kwenye lango la kuingilia na ile mbinu tuliyotumia ya kutokea pande tofauti, naona ilisaidia sana kuwachanganya wale walinzi.

 

Huku kila mmoja akihema, Gamutu alitugawa tena, akachagua wanaotakiwa kuingia ndani kisha mimi na wenzangu wawili, tulitakiwa kubaki pale nje. Hakukuwa na muda wa kupoteza, akafyatua risasi kwenye kitasa kisha geti likaachia na kufunguka, akageuka na kunitazama usoni.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

 

 2176
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment