The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Kusisimua ya Rama Mla Nyama za Watu -2

0
Ramadhani Musa (kushoto) akisimulia mkasa wake.

 

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita tulikuahidi kukuletea mwendelezo wa simulizi ya kusimumua ya motto aliyewahi kuwa gumzo, Ramadhan Seleman Musa aliyekuwa maarufu kwa jina la Rama Mla Nyama za Watu ambaye kwa sasa ametoka jela akiwa ni mtu mzima mwenye umri wa miaka 19.

Siku chache baada ya kuruhusiwa kuwa huru uraiani, alifika kwenye Chumba cha Habari cha Magazeti ya Global Publishers na kueleza mkasa mzima ambapo wiki iliyopita alisimulia jinsi alivyokamatwa mwaka 2008, akiwa na umri wa miaka 11 tu, akishikiliwa na vyombo vya dola nchini Tanzania kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Salome Yohana (3), mkazi wa Tabata jijini Dar, alipokutwa akitafuna kichwa cha mtoto huyo huku kikivuja damu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 

 

SASA ENDELEA… Rama anaendelea kusimulia:

“Nakumbuka hadi ninafika pale Muhimbili bado kile kichwa kilikuwa kinarukaruka kwenye mfuko. Hapo ndipo nilipobanwa na wale askari wa pale getini Muhimbili kisha baadaye nilikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Baada ya kesi ile, mwaka 2013, niliachiwa huru baada ya ripoti ya daktari kuonesha kwamba nilifanya tukio hilo nikiwa sijitambui, lakini sikuachiwa nirudi uraiani, nilirudishwa jela Segerea ambako nilikaa kwa takriban miaka sita pamoja na ile miaka ya kuwa mahabusu.

Pale Segerea nilikaa miaka sita kisha nikapelekwa hospitalini kule Mirembe (Dodoma) kwa ajili ya matibabu ambako nilikaa miaka mitatu. Jumla ikawa miaka tisa hadi hivi nilivyoruhusiwa. Kwa hiyo sasa hivi niko freshi kabisa na nimebadilika.

 

 

Nilipotoka nilikwenda pale nyumbani nilipokuwa ninaishi na mama na baba wa kambo, lakini sasa si unajua mazingira?

Zamani wakati tunaishi pale mimi nilijua ile nyumba ni ya kwetu, lakini nilipokwenda sasa hivi nimekuta kuna ghorofa na wanaishi watu wengine kabisa.

 

Nilipofika pale niligonga, lakini hakuna mtu aliyefungua. Nilibaki pale nje nikiwa nimesimama nikiwa sijui nifanyeje.

Baadaye nilijisemea ngoja niende kwa mjumbe au kwa mwenyekiti kwa sababu pale kwetu tulipokuwa tunaishi kwa mjumbe kulikuwa karibu kuliko kwa mwenyekiti.

 

Uzuri nilipofika kwa mjumbe, nilimkuta na alinitambua, akaniambia Rama vipi? Nikamwambia freshi, akaniambia shwari?

Nikamwambia freshi tu.

 

Nikamwambia mbona nimeenda kugonga pale nyumbani kumuulizia mama… kabla sijamalizia akaniambia sikiliza Rama, mama yako hapa alishaondoka muda. Pale mama alikuwa na dada yake alikuwa anakaa mtaa wa pili, naye alishaondoka.

 

Aliniambia cha msingi na anachoniomba nisikae maeneo hayo, niondoke nikatafute maisha mengine na sehemu nyingine ya kuishi, haiwezekani mimi nije kuishi pale wakati ndugu wa yule marehemu nao wanaishi hapohapo.

 

Hapo ndipo nilipoondoka maeneo yale na kwenda kutafuta sehemu nyingine ya kuishi ambayo ni siri. Siwezi kusema ninaishi wapi maana dah…maisha yamebadilika mjomba, siwezi kuficha, naumia sana, acha tu nisije nikaanza kulia (akilengwalengwa na machozi na sauti kukata hivyo mwandishi anambembeleza Rama asilie).

 

Ninachohofia kutaja sehemu ninayoishi, watu wananiogopa, hata nikipita mtaani watu wakishanijua wananiogopa. Wanasema Rama huyo…na kila mtu ananiogopa.

 

Mimi nimekulia sana maeneo ya Buguruni (Dar) lakini nikipita tu watu wote unasikia huyo, wananinyooshea vidole. Hivyo nimekuwa tu mtu wa kujificha na siyo mtu wa kujiachia mtaani. Asikwambie mtu watu wanaogopa hata kunisogelea!

 

Hakuna anayekubali kuishi na mimi. Asilimia kubwa ya maisha yangu nimekuwa mtu wa kukaa peke yangu mpaka hapo Mungu atakapotoa mwanga maana sasa hivi mwanga siuoni!

 

ANA MIPANGO GANI KWA SASA?

Kwa hivi sasa sina mipango. Labda niseme nataka kufanya biashara yoyote tu lakini sina pa kuanzia labda mtu tu aniambie, labda ananisaidia nifanye biashara hii au hii lakini hakuna mtu yeyote mpaka sasa amejitokeza kunisaidia hivyo mimi nipo tu hivihivi. Kwanza kama nilivyosema, mtu akishanijua tu ni mimi, ananikimbia muda huohuo.

 

MAISHA YA JELA YALIKUWAJE?

Yeah! Nikirudi nyuma kwenye maisha ya mle jela, kwanza kabisa niliambiwa watu walipopata tu taarifa kuwa ninapelekwa mle jela (Segerea), watu waligoma, wakasema nisipelekwe kule au nifungiwe kwenye chumba changu.

 

Kweli nilipofika kule nilijua kabisa kuwa kulikuwa na siri au unyanyapaa lakini siwezi kusema moja kwa ni unyanyapaa bali ni watu kuniogopa. Hata nilipoingia kule ndani nilifungiwa kwenye selo ya peke yangu na nikapewa godoro langu peke yangu nilalie.

 

Sasa wakati nimejifunika hivi, nikawa ninakung’uta godoro na blanketi maana kulikuwa na chawa, nikaona kila mtu ananichungulia, sikupata hata mtu wa kuongea naye maana kila nikikung’uta kila mtu anaamka.

 

Nikaona kama watu wananichora, nikaona nijifunike, sasa lile blanketi lilikuwa lina vumbi, nikaanza kukohoa, kitendo cha kukohoa na kujifunua, watu wote walinyanyuka wakaenda chooni na mimi sikujua ni nini.

 

Nikajua labda kwa sababu nimekung’uta lile blanketi, labda kulikuwa na ng’e hivyo na mimi nikakimbilia mle chooni, kila mtu alianza kukimbia na kupiga kelele mpaka mkuu wa gereza akaja. Alipokuja mimi nilikuwa sijui ni nini, nikashangaa kila mtu anamwambia kuwa Rama ameshaanza mambo yake.

 

Nikamwambia mkuu wa gereza hapana, siko kiivyo. Baadaye nilipewa chumba, nikawa ninalala peke yangu hadi waliponizoea japokuwa bado waliendelea kuniogopa.

 

Je, nini kiliendelea? Mkasa huu wa Rama una visa vingi vya kusisimua na kutisha juu ya namna alivyojihusisha na mambo ya ushirikina na kusababisha ajali za magari. Usikose wiki ijayokwenye gazeti hilihili la Risasi Jumamosi.

 

Ili kuona live simulizi hii tembelea Global TV Online kuanzia leo kwa kubofya www.globaltvtz.com.

Simulizi: Mwandishi Maalum

Msimuliaji: Ramadhan Seleman Musa

 

Simulizi ya Kusisimua ya Rama Mla Nyama za Watu

Leave A Reply