The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Kweli ya Christian Bella: Baba’ke Afukuzwa Kazi

0

Christian Bella & Malaika Band - AmerudiMachozi, jasho na damu vimemtoka kufika hapo alipo.

Abeba mchanga, ametengeneza mikate ili kujisomesha. Ametimuliwa nyumbani kwao kisa muziki. Ni mapenzi ya Mungu tu kufikia mafanikio aliyonayo, huyo ndiye Christian Bella ‘Obama’. Amesimulia mengi magumu aliyoyapitia maishani.

UNGANA NAMI HAPA CHINI…

JUMAPILI f’lani hivi ‘amaizing’, majira ya saa mbili kuelekea na robo za usiku nikiwa mahali nimetulia kwenye maduka ya biashara ya Mlimani City, muda mfupi tu baada ya simu ya mkuu wangu wa kazi Erick Evarist kukatika aliyekuwa ananipa maelekezo f’lani juu ya kazi,  mara simu yangu inapokea SMS, kucheki ni Christian Bella ‘Obama’;

“Kaka nimeshafika” aliandika.

“Uko upande gani?” nilimuuliza.

“Samaki Samaki hapa.”

“Poa nakuibukia.”

Baada ya SMS hiyo nikainuka nilipokuwa nimekaa tayari kujisogeza aliponielekeza ili niweze kufanikisha zoezi la kufanya naye mahojiano ambayo ndiyo yalikuwa yametukutanisha mahali pale.

Kwa mwendo wa ‘kiandishi’ nikipepesa macho huku na huko kama naweza kuambulia lingine lolote tofauti na lililonipeleka pale, nilielekea mpaka aliponielekeza, baada ya kufika tulisalimiana, nikaketi kwenye kiti cha mbao mbele yake.

“Samahi kwa kukuweka mkuu,” aliniambia akitabasamu, tuliahidiana kukutana saa moja hiyo ilikuwa saa 8:19, saa 1:19 mbele baada ya muda wa mihadi kupita.

“Usijali, kikubwa ni kwamba hatimaye tumekutana,” nilimwambia.

“Ni kweli.”

Tayari mhudumu alikuwa mbele yetu, Bella aliagiza kinywaji, mimi pia mhudumu aliweka mbele yangu juisi ya embe (mango juice), alipoondoka tu kazi ikaanza, Bella akaanza kufungukia maisha yake, harakati za muziki na mambo mengine mengi mpaka anafika hapo alipo leo…

“Jina langu halisi ni Christian  Kwete ni mtoto wa nane kati ya kumi na tatu wa baba yangu Kwete Mboeey na Janet Okashanga, nilizaliwa miaka michache kabla ya 1990 katika Hospitali ya Taifa Mamayemo, nimekulia katika mitaa ya Limete huko Kinshasa, Kongo.” Anasema Bella, nikisikiliza kwa makini na kunukuu machache kwenye ‘diary’ yangu.

Anaendelea kueleza kuwa wakati anazaliwa baba yake alikuwa na uwezo kifedha maana alikuwa akifanya kazi akiwa Mkurugenzi Mtendaji kwenye kampuni kubwa ya kufua mawese iitwayo PLZ LTD, jambo lililowafanya waishi maisha ya kitajiri sana.

Bella anaeleza kuwa mambo yalianza kubadilika na kuichachia familia yake alipokuwa na miaka 12, baada ya msimamizi wa kampuni hiyo ya PLZ kufariki dunia na uongozi kuchukuliwa na mtu mwingine aliyebadilisha sura ya kampuni na kufukuza baadhi ya wafanyakazi akiwemo baba yake.

Akitua glasi ya kinywaji chake mezani baada ya kunywa mafunda kadhaa na kushusha pumzi ndefu Bella anaendelea;

“Japo baba yangu kabla ya kufukuzwa kazi alikuwa na cheo kizuri kwenye kampuni hilo, hakuweza kujilimbikizia mali, alikuwa ameokoka, muumini wa Kanisa la Mashahidi wa Yehova, kwa hiyo hakuwa na mradi mwingine wowote ule, maisha yaliyumba mno, ikawalazimu kaka zangu waliokuwa wanasoma shule za kulipia kusimama kimasomo kwa kukosa ada.” Anasema Bella.

“Mama vipi, alikuwa anafanya kazi gani?” namuuliza huku nikianza kuingiwa na huzuni.

“Mama alikuwepo tu nyumbani, mimi nimekuwa nasikia alikatazwa na baba kufanya kazi yoyote, ukweli ni kwamba baada ya uchumi na maisha kubadilika kabisa nyumbani ndugu walianza kumlaumu baba wakidai ujinga wake wa kushika dini ndiyo ulitufikisha tulipokuwa.”

“Ehee, nini kikaendelea?” Namuuliza kwa shauku.

Anazidi kueleza kuwa baba yake hakuwa na jibu zaidi ya kuwaambia kila kitu Mungu ndiye hupanga!

Siku zikazidi kusonga mbele wakiishi kifukara, Bella anasema akiwa na umri wa miaka kumi na sita alilazimika kujichanganya mitaani na vijana wengine wa umri wake, kuchimba mchanga kwenye makorongo na kwenda kuuza kwa wajenzi ili aweze kujilipia ada ya shule.

Anasema hakuishia hapo kuhangaikia ada na mahitaji yake mengine, ilimbidi kuanza kujifunza pia kutengeneza mikate kwenye kiwanda-bubu kilichokuwa nyumbani kwao na rafiki yake Junion Kumbukumbu, alikokuwa analipwa posho kutokana na idadi ya mikate aliyotengeneza.

Je, nini kitaendelea? Bella ndiyo ameanza kusimulia juu ya maisha yake, mapito yake ni zaidi ya hamasisho, usikose wiki ijayo!

 

Leave A Reply