The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Mpoto: Apata umaarufu, arudi Songea-09

0

 

PENZI msomaji wa simulizi hii tamu ya Mrisho Mpoto, wiki iliyopita tuliishia pale Mrisho alipowasili nchini akitokea Marekani ambapo alikutana na Irene Sanga na kuandika mashairi na kukubalika na jina la Mjomba likatokea. Baada ya hapo alipata shoo nyingi lakini kuna jambo lilimtokea.

Tambaa nayo mwenyewe…

“Jambo kubwa la kwanza ni kwamba baada ya kupata shoo nyingi, nikaanza kuwa maarufu, naitwa na kufanya mahojiano mengi kwenye media mbalimbali. Kundi langu la Parapanda likaniita na kuniweka kati kisha wakaniambia kuwa kwa sheria yao, siruhusiwi kuongea kitu chochote. Lakini baada ya kuambiwa hivyo kuna gazeti moja nchini likatoa historia ya maisha yangu, nikaonekana kama sistahiki na kwamba nimekua. Ikanibidi niandike barua ya kuacha kazi kwenye kundi langu rasmi.”

Lakini Mjomba ulikuwa na chochote mfukoni kutokana na umaarufu wako?

“Yaani mpaka napata umaarufu bado nilikuwa sijapata lolote la kuweza kunisababishia kuwa na kipato kikubwa kwani maisha yangu yalikuwa ni yaleyale japo jina langu la Mjomba lilikua kila kona. Lakini nikaja kupata bahati katika shirika la umoja wa kimataifa linaloshughulika na watoto (Unicef) kama mtu wa kufundisha sanaa ambapo kwa mara ya kwanza nilipopata hela nilinunua friji na mke wangu Mariamu akawa anatengeneza askrimu tunauza na kujiongezea kipato. Kipindi hicho tulikuwa hatulali usiku ni kufunga askrimu. Biashara hiyo tukaifanya kwa muda mrefu sana.”

Ulisema una mambo mawili ambayo huwezi kuyasahau, la pili ni lipi Mpoto?

“Jambo la pili ambalo nalo siwezi kulisahau maishani mwangu ni kipindi nilichokuwa nikipata shoo nyingi, kilinisababishia kutokea mgogoro mkubwa kati yangu na mwenzangu Irene, huwa sipendi sana kulizungumzia hili lakini kifupi na kwa sababu ni simulizi ya kweli ya maisha yangu, niseme tu sababu kuwa ilitokana na ule wimbo wa kwanza kufanya vizuri.”

Nahitaji kujua japo tena kwa ufupi muafaka upi ulipatikana?

“Hapo ndipo nikakutana na Eric Shigongo (Mkurugenzi wa Global Publishers) baada ya kuuona ule ugomvi kati yangu na Irene kuwa mkubwa hadi kufikia kwenye media, alinituliza na kuniambia; ‘Mpoto mimi naona una kitu kikubwa sana ndani yako. Kitu unachokifanya ni unique, kitu ambacho kinaweza kukufikisha mbali na kufanya biashara kubwa tu kwa hiyo nakushauri huo wimbo achana nao. Kama unajiamini ulishiriki katika kuuandika tafuta mwingine, prove mtu wrong!’

Dah patamu hapo Mjomba, sasa ukaanza kazi rasmi. Nikamuuliza kichokozi, akaniangalia na kucheka kisha akaendelea…

“Kwa sababu ule wimbo ulikuwa ukizungumzia salamu. (Salamu Zangu Mjomba), ikabidi niandike muendelezo wake ambao ndiyo ule wa Nikipata Nauli na ndiyo wimbo ambao napenda sana kujitambulisha kama wimbo wangu wa kwanza.

“Nikatoa albamu yangu ya kwanza ya Nikipata Nauli yenye nyimbo tano. Niliuza albamu hiyo na kupata kama milioni 52. Baada ya hapo nikawa maarufu mara mbili, nakumbuka siku moja nilipigiwa simu kutoka Songea. Nikaambiwa;  ‘Wewe ni Mrisho Mpoto? Nikamwambia ndiyo, akaniuliza tena; ‘Ni Mpoto gani yule wa Mwanaisha Mpoto?’ Nikamwambia ndiyo, nikamuuliza, naongea na nani? Akaniambia; ‘Unaongea na baba yako, nimekuona kwenye gazeti hapa. Kumbe mwanangu umekua msanii mkubwa. Nakuomba uje unichukue Songea, naumwa na sina hata hela.’

Duh sasa ikawaje, si ulikatazwa kwenda Songea na mama yako na kwamba ukienda huko utakufa?

“Nilikwenda kuongea na mama, nikamueleza ukweli wote kuwa baba ameniambia niende Songea. Mama aligoma kabisa, nilitumia muda mrefu kumuweka sawa, akanikubalia hivyo nikafunga safari ya kwenda Songea. Nilipofika tu…

JE, unajua ni kitu gani kilimtokea Mrisho baada ya kufika Songea? Tukutane tena wiki ijayo hapahapa.

Leave A Reply