The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Mrisho mpoto: Afanya harusi ya ajabu, keki boga, shampeni dafu

0

????????????????????????????????????

MPENZI msomaji wiki iliyopita katika simulizi hii ya Mrisho Mpoto tuliishia pale alipopata shavu la kwenda nchi nyingi kama vile Marekani, Sweden, Norway, Scotland na sasa amefikia chuo cha Marketing Theatre.

Tambaa nayo mwenyewe…

“Hicho chuo kilikuwa ni moja kati ya vyuo vikuu vya sanaa pale Johannesburg, Afrika Kusini ambapo nilipofikia hapo nilianza kujifunza jinsi ya kutohoa na kughani, jinsi ya kuzingatia vitu gani unapotaka kuandika mashairi na mengine mengi.”

Hongera yako mkubwa kwa kupata mashavu yote hayo, ikawaje sasa, hukurudi Bongo mapema?

(Anacheka kidogo)

“Nilianza kujitambua rasmi kwa kuwa zile safari zote nilizokuwa nikienda kwanza zilikuwa kama semina na zilinifunza mengi ambapo hata nilivyotua Bongo nikaendelea na kundi langu la Parapanda na kurekodi ule Wimbo wa Nenda Mwalimu tukiwa na Irene sanga.

Hapohapo Mrisho, embu niambie huyo Irene Sanga na wewe yupi alianza kuwepo Parapanda?

“Irene alikuwa akisoma mwanzoni chuo cha sanaa Bagamoyo na alipomaliza alijiunga na Kundi la Parapanda moja kwa moja na kunikuta.

(Namsikiliza kwa makini lakini nahisi kuna kitu kinanitatiza, namsimamisha maongezi na kumtupia swali.)

Kwa hiyo Mrisho, hapo ndipo ukaanza kujulikana rasmi, si ndiyo?

“Bado kwani kuanzia hapo nikaanza kurekodi sasa ile siriazi mashairi yangu yote. Wimbo ulionitambulisha rasmi ni ule wa Salamu Zangu Kwako Mjomba.

Hakukua na matukio ya ajabu tena baada ya kuambiwa hapo awali na mama yako usirudi Songea?

“Matukio hayakuwepo kwani kila ikipita muda fulani mama alikuwa akinisisitizia nisifike Songea tena na endapo nitakiuka naweza kuhatarisha maisha yangu.”

Uliishia vipi uhusiano na Mariamu yule ambaye ulikuwa ukipenda kufuatana naye kwenye mikutano ya Kiislamu?

“Wakati nikiwa Kundi la Parapanda nilikuwa naishi maeneo ya Mabibo, Dar kwenye nyumba ya ofisi kama mlinzi ambapo nilipewa kachumba kadogo uani.

“Nikiwa hapo Mariamu alikuwa akitoka shule anapitiliza kwangu.”

Dah, inasisimua kweli hii, kwani Mariamu alikuwa akisoma wapi na mlikuja kuachana au?

“Mariamu alikuwa akisoma Shule ya Sekondari Kisutu, Dar na alipomaliza kidato cha nne tu nikaoa hapohapo kama unakumbuka mimi ndiyo nilifanya harusi ya ajabu Dar ambapo watu walikuwa wakikaa kwenye mikeka, shampeni dafu, keki boga.”

Idea ya kufanya harusi hiyo ya ajabu ilikujaje?

“Ujue miongoni mwa vitu vilivyopo ndani ya moyo wangu ni pamoja na kupenda vitu vya nyumbani yaani vile vya asiliasili, Kiswahiliswahili.

“Nilipeleka wazo hilo kituo cha utamaduni cha nchini Urusi kilichopo nchini (Russian Culture Centre), kwa kuwa nilishawahi kwenda nchini mwao nikawaambia nataka kufanya harusi ya ajabu ambayo haijawahi kufanywa popote Tanzania.

“Nikawaambia sitaki kuwe na vijiko, sitaki kuwe na meza kuu, sitaki kuwe na MC mmoja wawe wengi na mimi niwe mmoja wapo, sitaki ile kawaida kwamba bwana harusi awe wa mwisho kuingia na wa kwanza kutoka, sitaki kuwe na meza kuu, watu wakae chini kwenye mikeka na kila mtu na sahani yake, nikatafuta baiskeli zaidi ya 200 za madafu kutoka Kigamboni zikapangwa nje kila anayeingia.

“Nikawapa hiyo idea wakaipenda na kunipa ukumbi ambapo wasanii wenzangu kina Monalisa, Joti, Tyson, Mpoki kipindi hicho hawajawa maarufu wakakubali kuwa ma MC tukawa ma-MC kama tisa hivi na mimi nikiwepo, waandishi wa habari walikuja wengi wakakaa chini.

“Nilikuwa wa kwanza kufika katika ukumbi na kufungua milango, nikazungukwa na machifu huku wameshikilia mikuki na mwisho wa harusi nikafunga mlango na kuurudisha ufunguo.

Je, nini kiliendelea? Tukutane wiki ijayo.

Leave A Reply