The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Msamaha wa Mama – 09

1

Mwandishi: SEID BIN SALIM
Wakati wao wanaingia ndani upande wa pili Hamad na Ticha wakiwa njiani wanarudi mjini ghafla walikutana na gari nyeusi imezuia barabara mbele yao, walipata mshangao sana wakapunguza mwendo kisha wakasimama, upande alikokuwa amekaa Ticha alitokea mtu amevaa nguo ya kumfunika uso wake kama gaidi akamtandika risasi Ticha na kutoweka. Alikimbia fasta mpaka kwenye gari hilo jeusi lililokuwa limezuia barabara kwa mbele akaingia ndani na kukanyaga mafuta, tairi zilizungushwa, rami ikasuguliwa vizuri jamaa akatoweka kimuundo huo akimuacha Ticha katika wakati mgumu wa jeraha, risasi ikimpatia maumivu makali mno ya kushindwa kustahimili na kupoteza fahamu.
*****

Seid na mama yake waliingia ndani wakiwa na furaha ya kutembelewa na wageni na kuachiwa chochote kitu, walijua siku hiyo uhakika wa kula vizuri upo.

“Mama leo nadhani tunakula nyama. Alisema Seid akiwa amekaa chini amejiegemiza ukutani na mguu mmoja kuusimamisha, alimuangalia mama yake aliyekuwa anajifuta futa jasho usoni kwa kutumia khanga yake aliyokuwa amejifunga.
“Heee mwanangu unawaza kula tu wewe baba.
“Sasa tufanyie nini hiyo fedha uliyopatiwa?.. elfu 20 chukua kumi lete tule vizuri leo.
” Ila kweli mwanangu, basi hapa itabidi uchukue baiskeli yako uende sokoni uchukue japo nyama na viungo viungo hivi, Mungu ametuona, tunavyoishi yeye ndiye anayejua, ipo siku moja atatuokoa tu na hizi shida tulionazo. Tusiache kumuomba.
” Hilo ndilo la msingi mama yangu, dua kwa sana ndiyo kinachotakiwa, na hasa kuhusu masomo yangu Mungu aweze kuweka wepesi matokeo yangu yarudi, naamini ipo siku mama tutafanikiwa tu inshallah. Alisema Seid na kumalizia kwa neno inshallah akanyanyuka.
“Sasa nipe hiyo pesa niende huko sokoni.

Bi Najma aliposikia mwanaye amesema hivyo aliziangalia pesa alizopewa ziko wapi na kutoa elfu kumi kumpatia, aliichukua Seid na kuangalia kwa kuigeuza geuza akaachia tabasamu.
“Tena hiki chakula nataka nikipike mimi mwenyewe uone nilivyo vizuri kwenye kupika mama.
“Ebu nitokee huko unajua kupika wewe!.
“Sasa mama hutaki au.
“Una miaka 20 mwanangu, mama yako nazeeka tena utoto upunguzege eeh!.
“Mtoto hakui kwa mama, ila si tutampelekea na bibi?.
“Hayo meno anayo?.
“We unayo? ,, Seid alimtupia swali mama yake kama utani baada ya kumuuliza kama bibi yake ana meno
“Ebu nenda huko nina miaka 40 tu sijazeeka kihivyo mwanangu ila bibi yako anaenda kwenye tisini yule sasa hivi.

Seid alitoka na kumuacha mama yake anacheka, akachukua baiskeli na kwenda kwenye soko la Kiwengwa lililoko Pwani Mchangani kwa ajili ya kuchukua mazagazaga ya mapishi ili wale vizuri siku hiyo bila kujua kilichomkuta Hamad na Ticha kipindi wanaondoka.

Alijikokota na baiskeli akijaribu kuzinyonga pedeli kwa nguvu ili afike haraka sokoni, uso wake ulionekana kuwa wa furaha kutokana na kujua mapema kuwa angekula chakula kizuri siku hiyo tofauti na siku nyingine zote.
Uso wake ukiwa na furaha za kumwaga, upande wa pili kwa Hamad sura yote ilikuwa imeharibika kwa kuchanganyikiwa baada ya Ticha kupigwa risasi, ubongo uliIipuka na kushindwa kujua afanye nini kwa haraka, jasho liliuzunguka uso wake huku na mwili wote ukihisi muwasho.
Hakujua afanye nini licha ya kuweza kutulia sehemu moja na kukosa papara za kuushughulisha moyo, alituliza akili, akijua endapo atakuwa na itikadi za kudata tu kutokana na kile kilichoko mbele ya macho yake hatofanya chochote. Alikuwa akipenda sana kumfuatilia Wiliam shujaa aliyeishi miaka zaidi ya 100 duniani na kufanya mengi ikiwemo kuwakomboa watu zaidi ya mia nne waliokuwa wametekwa katika meli ya uharamia Somalia na kuwarudisha nchini Uingereza bila kukwama katika harakati za uandishi wake. Mawazo ya kuukumbuka ushujaa wa huyu jamaa yalimuingia, alitulia akashusha pumzi japo tayari na machozi ya presha yalishaanza kumlengalenga, alitoa simu na kubonyeza namba za dharura kwenda polisi akapiga, simu haikuita sana ikapokelewa.

“Mahonda Police Station tukusaidie tafadhali” . Ilisema sauti ya upande wa pili iliyosikika kuwa nzito kwenye simu.
” Hal..loo haloo! Naomba mnisaidie haraka iwezekanavyo, tumevamiwa na mtu tusiyemfahamu kipindi tunatoka Kiwengwa, mwenzangu amepigwa risasi mimi ni mtoto wa Mzee Shaibu. Alisema Hamad.
“Umesema uko wapi? Aliuliza polisi, alipoambiwa mtoto wa Mzee Shaibu tu hakuhitaji maelezo mengi zaidi.
“Kiwengwa.
“Naomba nipate maelezo yote na aina ya gari iliyowavamia.
“Ilikuwa ny’e ny’eusi. Alisema pumzi zikikatika na kushindwa kabisa kuongea sentensi ndefu.
“Namba za gari?..
“ZNZ 654 AD.”

Aliweza kujieleza vizuri Hamad japo alishaelemewa na mzigo uliokuwa mbele yake, polisi alimuomba apunguze presha aendeshe gari kwa makini kupitia njia ya Mahonda iendayo mjini atakutana na gari ya wagonjwa na watampeleka Ticha hospitali haraka iwezekanavyo, huku yeye akifanya juu chini kuhakikisha anateua vijana wa kuifanya kazi ya kulitafuta gari lililowafanyia uhalifu.

Simu ilikatika Hamad akafanya vile alivyoambiwa, mikono ilikuwa inatetemeka na kuwa na misisimko isiyoisha, alishika usukani wa gari akakanyaga mafuta na kuanza kulitoa gari taratibu, Huku yule ofisa wa polisi Mahonda aliyejulikana kwa jina la Saleh, aliyepokea taarifa za kuvamiwa kwa Hamad akiteua vikosi makini kutoka katika idara yake, vijana nane, magari manne tofauti waende haraka kufuatilia uhalifu huo uliotokea ikiwezekana kulipata hilo gari.
Bila kupoteza muda vijana hao waliochaguliwa, waliokuwa wakifanya kazi katika Kituo cha Polisi Mahonda waliingia kwenye magari na kuanza safari.

Gari moja lilipita njia inayoelekea Donge na matatu kupita njia iendayo Kinyasini, yalipofika Kinyasini moja lilikata njia ya Kiwengwa, mawili kusonga mbele.
Na yenyewe yalipofika mbele yalijigawa moja likaelekea njia ya Matemwe lingine likanyoosha kuelekea Nungwi wakiamini kufanya hivyo lazima gari lipatikane labda tayari liwe limeingia mafichoni.

Taarifa zilizidi kusambaa ndani ya muda mfupi, Kamdanda Saleh alizisambaza haraka baada ya kujua aliyempatia habari ni mtoto wa mtu mkubwa ndani ya Serikalini ya Zanzibar.
Aliwasiliana na makamanda wenzake mjini ili nao waweze kujiweka sawa kuingia barabarani kulisaka hilo gari.

Vituo vingi vya idara ya polisi vilipata kufahamu nini kinaendelea na kuwa tayari kusimama imara ili mtu aliyefanya huo uhalifu akamatwe, walimwagika barabarani na silaha nzito nzito wengine wakipakizana kwenye magari kwa ajili ya kufanya doria. Barabara ya Mfenensini ilifungwa kwa muda pamoja na “round about” ya mjini inayokutanisha magari yatokayo Bububu na kwingine kwenda Bandarini na Stend Kuu ya Darajani, walihakikisha wanafanya kazi kwa makini zaidi, tayari walishajua kama watafanikiwa kwa hilo watatengeneza majina na kupata kuonekana katika vyombo vya habari kutokana na tukio lenyewe japo limetokea ghafla.

Hamad alijitahidi kuendesha gari mpaka kufika Mahonda, miwani ilishajaa mvuke wa joto ilibidi aivue, Ticha alikuwa pembeni yake akiwa hoi hajitambui. Walipofika na gari ya wagonjwa nayo ilikuwa inafika eneo hilo, walifungua milango haraka wakamtoa na kumuingiza ndani na kuanza safari ya kumpeleka Hospitali ya Serikali ya Mnazi Mmoja.

Hamad alichukuliwa mpaka ndani ya kituo, askari watatu walimzunguka wakiwa tayari kuandika ripoti za kile atakachowaambia.
Kabla ya kuanza kumhoji, simu ya mezani ilianza kuita, kamanda akaichomoa na kuiweka sikioni.
“Police Station Mjini no. 886, tunaomba mtoto wa mheshimiwa afike kituo kikuu kwa ajili ya kuandika ripoti haraka. Alisema wa upande wa pili ambaye alikuwa polisi pia anayefanya kazi mjini.
“Sawa mkuu.”

Alitoa simu sikioni na kuirudisha kwenye meza, aliwaangalia vijana wake huku akisema.
“Inabidi akaandike ripoti mjini haraka iwezekanavyo, chukueni gari lililobaki mwende naye mjini, kijana ingia ndani ya gari lako uongozane na vijana hawa ukahojiwe juu ya lililokukuta, ulinzi uko salama, nawaamini sana vijana wangu.”

Hamad hakujibu chochote, aliinuka kwenye kiti alichokuwa amekaa, akatoka nje huku vijana watatu wakiingia katika difenda nyeusi. Alifika kwenye gari akafungua na kuingia ndani, akaliwasha safari ya kwenda mjini ikaanza akiwa hana amani kabisa moyoni mwake.
Gari lake lilitangulia nyuma ikafuata ya polisi. Bado tafutatafuta ya sehemu mbalimbali iliendelea kulitafuta gari lenye usajili wa namba ZNZ 654 AD. huku kukiwepo mawasiliano ya karibu ili kujuzana kuhusu taarifa za kila kinachoendelea kona zote.

Wananchi waliokuwa sehemu mbalimbali za barabara walikuwa wanashangaa kuona polisi wanavyopiga doria jioni hiyo, kitendo kilichosababisha wengi wawe na maswali tofauti tofauti.
“Amy vipi leo kuna nini mbona doria!?.”
Mpemba mmoja aliyekuwa anachoma mahindi alisikika akimuuliza mwenzake aliyekuwa pembeni.
“Itakuwa kuna uhalifu ushafanyika tayari na hivi Zanzibar ilivyoharibika sasa hivi sijui!.
” Au washaiba Wanyamwezi maana haweshi siku hizi kuvamia mabenki yetu, juzi tu hapo People’s Bank of Zanzibar wamevamia wakaondoka na mamilioni.”

Kabla hawajaendelea ghafla waliona linatokea gari jeusi likiwa spidi kali sana barabarani, watu wote waliokuwepo sehemu hiyo iliwabidi watoke mbio kwa woga, walijua tayari kumekucha, hawakukaa sawa wakaziona difenda mbili zikiwa mwendo kasi, risasi nne kwa mkupuo zililia juu kwa juu, baadhi ya akina mama walianguka chini kwa presha huku wengine wakikimbia mbio, mtu mmoja alisikika anasema huku akikimbia:
“Jamani hivi hii Zanzibar yetu ishakuwaje sasa hivi?, kila siku vita! Kila siku vita hatupumui jamani tushachoka siyeee, tushachoka Wallah aaah!.

Difenda mbili zilizofanikiwa kuliona gari hilo maeneo ya Bumbwini likijaribu kutafuta upenyo wa panya ili kuingia vijijini na kuanza kutimuana nalo mbio, askari wa difenda hizo walipeleka mawasiliano kwa vituo vyote vya polisi vilivyo karibu na barabara, ili vijaribu kuzuia barabara zote hasa barabara inayochomoza Bumbwini kwenda mjini au Kitope, kwani ndiyo sehemu walipokuwa wakilifukuza kwa karibu.

Sekeseke hizo zikiwa zinaendelea, baba yake Hamad, Mzee Shaibu habari zilimfikia, Alichanganyikiwa ghafla kutokana na kumpenda sana mwanaye, alipiga simu haraka kwa maofisa usalama kuuliza usalama wa mtoto wake kwanza.

“Ndugu zangu mimi ni Mzee Shaibu, nimepata habari za Ticha mtu aliyekuwa ameongozana na kijana wangu kupigwa risasi na kuambiwa kuna kashikashi zinaendelea huko vipi mwanangu yuko salama?. Aliuliza.
“Mzee wangu mwanao yuko salama kabisa, tunaomba usiwe na wasiwasi jeshi la polisi linafanya kazi yake.
” Na imetokana na nini hiyo hali.
“Hatujaweza kujua chochote kwa sababu anayejua kila kitu ni Hamad mwanao na bado hajahojiwa.
“Vipi kuhusu Ticha?.”

Kabla ya kumaliza kuongea simu ilikata, alitikisa kichwa.
“Jamani ni nini hiki kinatukuta Zanzibar, mbona amani inatoweka kila siku? tunaishi roho juujuu na familia zetu, wallah kwa nini?!

Hali ilikuwa bado si shwari maeneo tofauti tofauti, watu walilaani hovyo hovyo juu ya hali hiyo, wengine walipata presha na kuzimia hapo papo. Kwa bahati nzuri hakukuwa na magari mengi katika barabara za shamba, askari walishawasiliana kila sehemu kuhakikisha wanaliwinda gari hilo lililoonekana kuwa imara, Risasi kadhaa zilipigwa juu kuangalia kama litasimama lakini wapi, difenda zilizokuwa zinalifukuza zilishakuwa nne.

Baada ya kuchukua muda mrefu wakipiga risasi juu bila kusimama, askari mmoja aliyekuwa na cheo kuliko wengine alisikika akisema “Lengeni gari asituzingue mpumbavu huyo.

Askari walianza kulenga gari, risasi moja ilifanikiwa kulenga tairi. Tairi liliachia pumzi na kuliacha gari likianza kukosa mwelekeo. Risasi nyingine ilipiga tairi la pili kwa nyuma, ndipo gari lilianza kuyumba na kushindwa kutembea kisha kuparamia nguzo ya umeme.

Difenda zililizunguka gari hilo huku askari wakikaa makini kwa ajili ya kushambulia endapo kitatokea kitu tofauti, walishuka na kuanza kutembea taratibu. Mmoja wa askari hao aliushika mlango wa gari lililofanya uhalifu na kuufungua haraka, ndipo alitoka jamaa yule yule aliyemtandika risasi Ticha akiwa ameshikilia bastola mkononi.
” Tulia hivyo hivyo kama unataka salama ya kuishi, na wambie wenzako waweke vikaragosi vyao chini!. Alisema mhalifu akinyoosha bastola yake kumnyooshea askari aliyefungua mlango wa gari, lakini kitendo chake cha kuongea japo alikuwa amejifunga kitambaa usoni, baadhi ya askari waliosikia sauti hiyo walihisi sauti hiyo kuifahamu, haikuwa ngeni masikioni mwao.

Askari huyo hakuwa na silaha alinyoosha mikono juu, askari mwingine aliyekuwa nyuma akasikika akisema:
“Mjinga mkubwa wewe, shusha silaha yako haraka kabla sijamwaga ubongo wako, huna mtu wa kumtisha hapa, uko peke yako tuko zaidi ya kumi, teremsha bastola yako kwa usalama.
“Mnaweza kuwa zaidi ya kumi na bado mkawa mabwana wadogo tu kwangu, endapo utathubutu kushuti na mimi naondoka na huyu mwenzenu kwasababu sishindwi kumshuti kabla nyinyi hamjanishuti. Alisema.

**Tukutane Sehemu ya 10 baadaye…..

1 Comment
  1. ZEBEDAYO says

    very interesting story

Leave A Reply