SIMULIZI YA WATOTO HAWA 5… INASIKITISHA

KAMA una uwezo wa kupata angalau mlo mmoja kwa siku, una mahali pa kulala pa kueleweka hata kama ni chini na huna tatizo kubwa la kiafya, basi unapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani simulizi ya maisha ya familia moja huko Bukoba-Vijijini mkoani Kagera inasikitisha mno, Uwazi linayo.  

 

Familia nyingi zinapitia kwenye mateso ya ajabu, lakini hii ya Mzee Godwin Mulokozi, mkazi wa Bukoba-Vijijini, ipo njia panda kutokana na kuwa kwenye wakati mgumu usiosimulika na wenye kuumiza baada ya baba huyo na mkewe kuwa wagonjwa hivyo watoto wao sita kuwa kwenye mateso ya kutisha.

 

Watoto hao wanakabiliwa na njaa ya kutisha ambayo kwa mtu mwenye njaa ya kawaida, ukiwashuhudia, lazima njaa yako itakwisha na kujiona umeshiba. Watoto hao wenye umri wa kufuatana, wanajilea wenyewe bila wazazi wala msaada wowote huku mmoja ambaye ndiye mdogo kuliko wote akishinda hivyo kuokota kinyesi cha mbuzi na kula kutokana na kukosa chakula.

 

Katika mazungumzo na Gazeti la Uwazi, mmoja wa watoto hao aliyejitambulisha kwa jina la Kasheki ambaye ndiye mkubwa na mwenye nguvu kidogo ukilinganisha na wenzake, alisimulia kuwa wamekuwa wakiishi maisha magumu mno kwani wazazi wao kila mara wanaumwa na kulazwa hospitali bila kujua wanasumbuliwa na ugonjwa gani.

Alisema katika hali kama hiyo, wao hujikuta wakiishi wenyewe na yeye kuwa na jukumu la kuwalea wadogo zake wapatao watano.  Kasheki alilieleza Uwazi kuwa, amejikuta kwenye wakati mgumu mno wa kuwalea wadogo zake huku akiwa hajui cha kuwapa hivyo hali zao kuendelea kuwa mbaya.

 

“Kila tunapolala hatujui tukiamka tutakula nini siku nzima. “Mara nyingi mdogo wangu wa mwisho huwa anakula kinyesi cha mbuzi ninapokuwa kwenye mihangaiko ya kutafuta mapapai ili tule,” alisema Kasheki katika hali ya kutia huruma kupita kiasi. Akiendelea kusimulia, mtoto huyo alisema kuwa, hata kulala kwao ni shida mno kwani wana chumba kimoja tu ambacho wanalala wote na wazazi wao ambao ni wagonjwa mno.

 

“Nimesema mdogo wangu anakula kinyesi cha mbuzi, si kwa kupenda kabisa, hapana, ni kwa sababu njaa inakuwa imemshika sana hivyo anatambaa hadi jirani na zizi la mbuzi la jirani kisha anakaa na kuanza kula. Pia mimi ninaweza kumuona na nikamuacha kwa sababu unakuta nyumbani sijapika kitu chochote,” alisema.

Kasheki alisema kuwa, pia wana uhitaji mkubwa wa mavazi kwa sababu hawana hata shuka la kujifunika usiku wanapolala na kuna baridi mno ambapo huwa wanalala chini na hakuna hata godoro.

 

“Ningewaomba sana Watanzania wenzangu watusaidie ili tuweze kupata mahitaji muhimu japokuwa tunamshukuru sana dada Flora Lauo (wa Kipindi cha Nitetee) kwani ameweza kutusaidia mpaka hapo tulipo na sasa tuna uhakika hata wa kula,” alisema Kasheki.

 

Kama umeguswa na habari hii, unaweza kuwasaidia watoto hao kupitia namba 0759 665 555 na tunatoa shukurani za dhati kwa Flora Lauo ambaye ni Mtangazaji wa Kipindi cha Nitetee ambaye amechangia kufanikisha kupatikana kwa habari hii.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

 

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment