The House of Favourite Newspapers

Sinaloa; Mji Uliojaa Makaburi ya Kifahari!

UTAMADUNI wa kujengea makaburi upo hata hapa kwetu na gharama za ujenzi zinatofautiana.

Ukiwa miongoni mwa watu wanaoshangaa uzuri wa baadhi ya makaburi ya Kinondoni jijini Dar maarufu “VIP” usithubutu kwenda mjini Sinaloa nchini Mexco huko utazimia kwa mashangao.

Sinaloa ni nyumbani kwa mfanyabiashara maarufu na trilionea wa madawa ya kulevya duniani aliyetiwa nguvuni hivi karibuni na Jeshi la Marekani, Joaquin ‘El Chapo’ Guzman.

Ukibahatika kufika kwenye mji huo unaweza kudhani kuwa ni mji uliojaa makanisa ya kifahari yaliyopambwa kwa misalaba, lakini utakapouliza;

“Ni majengo ya ibada haya?” Utajibiwa; “Ni makaburi ya matajiri.” Ndipo utakapoachama mdomo na kushangaa.

Kibaya zaidi matajiri wanaotajwa kufanya kufuru hiyo ni wafanyabiashara wakubwa wa madawa ya kulevya ambao kwao suala la mtu kuzikwa kifahari ni utamaduni kama huku kwetu maiti kuchimbiwa mwanandani.

Kama wewe unaona ni gharama mtu kutumia shilingi laki tano kujengea kaburi, jamii ya Wasinaloa kutumia zaidi ya pauni 230,000 (takriban shilingi milioni 650) kujengea kaburi moja, si ishu kabisa.

Wakati Serikali ya Mexco ikiwa katika vita kubwa ya kupambana na wauzaji wa madawa ya kulevya, kazi nyingine nzito ni kuwajenga watu na hasa vijana kisaikolojia ili waichukie biashara hiyo ambayo baadhi ya Wamexco wanaiona kama biashara ‘inayolipa’ na kumpa mtu heshima.

“Kila binadamu anapenda kuishi vizuri na hata akifa azikwe vizuri, jambo hili ndilo jamii yetu hapa inaliamini na kulitekeleza,” alisema Juan Carlos Ayala, profesa katika Chuo Kikuu cha Sinaloa ambaye amejikita zaidi katika masuala ya utamaduni na sanaa.

Ingawa hadhi ya makaburi inapishana kutokana na hali, heshima na utajiri wa mtu kama ilivyo huku kwetu, lakini Sinaloa suala la mtu kuzikwa vizuri linazingatiwa na jamii nzima na kwamba inaposhindikana, baadhi ya vigezo vya kaburi kutimizwa, basi jamii iko radhi kutoa michango yao ili tu kuhakikisha kuwa kaburi la ‘kichovu’ hazikiwi Msinaloa.

Baadhi ya vitu ambavyo ni muhimu kuwekwa kwenye makaburi ambayo mengi hujengwa kama nyumba ni pamoja na marumaru, nakshi mbalimbali, kamera za ulinzi na kiyoyozi ambacho ni lazima kifanye kazi muda wote.

Mbali na hilo wenye ‘uwezo wao’ wanapokufa au kupoteza ndugu zao, basi makaburi yao huweza hujengwa kwa madini na vito vya thamani huku vioo na milango yake huwekewa madini yanayoweza kuzuia risasi isipenye ndani.

Si ajabu ukifika kwenye msiba wa Msinaloa ukasikia tenda ya kujenga kaburi ikitangazwa na watu kujitokeza kuomba ambapo makampuni ya nje ya nchi nayo hugombea dili za kujenga makaburi.

“Heshima hii ya kujengea makaburi si tu ni jambo zuri kwa waliokufa, lakini hata kwa wale wanaobaki hai, wanapoona makaburi ya gharama na heshima namna hii huhamasika kufanya kazi kwa bidii.

“Lakini pia wakiona makaburi yenye hadhi huwakumbuka ndugu zao kuwa waliishi maisha bora katika jamii,” alisema Ayala.

Hata hivyo, tofauti na hapa kwetu ambapo ujenzi wa makaburi huambatana na uadishi wa majina kwenye makaburi; Sinaloa ni nadra jambo hilo kufanywa.

Ukifika utakuta eneo la makaburi kama mji uliojengwa kifahari na wenye makaburi au wenyeji ndiyo wanaojua nani kazikwa wapi na si lazima kuweka utambulisho.

Mexco ni nchi maarufu kwa biashara ya madawa ya kulevya ambapo majina kama; Joaquin Guzman, Pablo Escober, Frank Lucas, Ismai Zambaga Garcia, Amado Carrilo Fueten na mwanamama Griselda Blanco yamepata kutikisha dunia kwa biashara hiyo haramu.

MAKALA: RICHARD MANYOTA NA MITANDAO

Comments are closed.