The House of Favourite Newspapers

Sinema ya Ebitoke na Mlela Sasa Imenoga

ILE kiki hoti a.k.a Sinema ya Annastazia Exavery ‘Ebitoke’ na Yusuph Mlela inaendelea na sasa imenoga baada ya njemba mmoja kutoka Zanzibar ‘Zenji’ kuibuka na madai ya kuporwa mke; tulia hivyohivyo Risasi likuhabarishe.

 

Njemba huyo kutoka Zenji aitwaye Nassir Vanillah, alitua jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kudai yule mdada anayejulikana kwa jina la Beyonce aliyedaiwa kurithi penzi la Ebitoke kwa Mlela ni mkewe.

 

“Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Beyonce tangu mwaka 2013, lakini juzi nilishtuka kusikia Mlela anatembea naye.

“Jambo hili linaniumiza sana, yaani niko tayari kwenda hata kwa waganga ili kumkomesha Mlela,” alisema njemba huyo.

Kama hilo halitoshi Vanillah alitupia picha kwenye ukurasa wake wa Instagram inayomuonyesha mwanaume akiwa na ujauzito kisha akaandika maneno yafuatayo:

“Nikimfanya hivi @mlelandro (Mlela) nitakuwa nimekosea?”

 

Baadhi ya wafuasi wake mtandaoni walipomuuliza mantiki ya picha na ujumbe huo, Vanillah aliendelea kusisitiza kuwa na uchungu wa kuporwa mke na kwamba anatamani kurudiana naye.

Hata hivyo baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii waliponda madai hayo ya Vanillah kwa kusema inaonekana yanaendeleza kiki ya Mlela na Ebitoke kwa kutoa ‘siriz’ nyingine.

 

“We mke unaweza kumdai kama papai, eti nirudishie mke wangu kirahisirahisi tu, labda kama mimi sijui vizuri uchungu wa mke,” aliandika mchangiaji mmoja mtandaoni kuhusu madai ya Vanillah.

 

Uchokonozi wa mwandishi wetu haukuweza kufanikiwa kuona cheti cha ndoa cha Vanillah na Beyonce zaidi ya kuelezwa kuwa njemba huyo naye ni msanii kutoka Zenji.

Aidha, Risasi Jumamosi lilimtafuta Mlela ili kujibu madai hayo ya kuiba mke wa mtu lakini hakupatikana kwani simu yake iliita bila kupokelewa.

Hivi karibuni Ebitoke alidaiwa kumvamia Mlela hotelini na kumfanyia fujo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alionekana akipigana na Beyonce aliyedaiwa kuwa ni mpenzi mpya wa Mlela.

 

Hata hivyo, baadaye ikavuja habari kuwa mchezo huo ulipangwa kama kiki ya kuwabusti wasanii hao jambo ambalo linayaweka madai ya Vanillah kwenye hisia kuwa huwenda mchezo wa kiki ya Ebitoke na Mlela unaendelea kwa ‘skripti’ nyingine.

STORI:AMMAR MASIMBA

Comments are closed.