The House of Favourite Newspapers

Singida BS Jiandaeni… Nabi Ashusha Full Kikosi Cha Caf

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amewaambia wapinzani wake Singida Big Stars kuwa wanalitaka Kombe la FA, hivyo hawatawadharau huku wakipanga kukitumia ‘full’ kikosi wanachokitumia katika Kombe la Shirikisho Afrika ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana leo Jumapili katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Yanga itacheza dhidi ya Singida wakiwa wametoka kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuwaondoa Marumo Gallants ya nchini Afrika Kusini kwa ushindi wa mabao 4-1.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Nabi alisema kuwa hawataudharau mchezo huo dhidi ya Singida Big Stars kwa kuwapumzisha baadhi ya nyota wao tegemeo kwa makusudi huku wakipanga kuwatumia wote.

Nabi alisema kuwa malengo yao msimu huu ni kuhakikisha hawaachi kombe lolote wanalolishindania katika msimu huu, hivyo wataingia katika mchezo huo kwa tahadhari zote za kufuzu kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho.

Aliongeza kuwa wanaliheshimu Kombe la Shirikisho, hivyo atatumia siku mbili jana Ijumaa na leo Jumamosi kukamilisha mbinu za kiufundi mazoezini kabla ya kuwavaa Singida BS kesho Jumapili.

“Mechi ya kwanza ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika tutacheza Mei 28, mwaka huu hivyo hatuoni sababu ya kuwapumzisha wachezaji wetu wote muhimu katika mchezo huu ambao tunahitaji ushindi tufuzu Fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu.

“Kwetu benchi la ufundi tunauchukulia umuhimu mkubwa mchezo huu tofauti na watu wanavyofikiria kuwa huenda tukapumzisha baadhi ya wachezaji wetu muhimu.

“Hivyo tutaweka nguvu nyingi kuelekea mchezo huu, kwani ushindi huu utawawezesha wachezaji wetu kupata muda wa kucheza mechi ya ushindani kuelekea mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika,” alisema Nabi.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply