The House of Favourite Newspapers

Sipungii tena wadada mkono!

0

Kuna mambo mengine mtu unafanya kisha yanageuka maana na kukuweka katika hali ya sintofahamu. Lakini lililonikuta juzi mpaka sasa nacheka huku nalia peke yangu hata usiku wa manane. Unajua kama wiki tatu zilizopita yule mchumba wangu niliyewatambulisha kwenu  si kaamua kuniacha baada ya kukutana na jamaa mmoja mwongo wa kutisha.

Jamaa kampiga fiksi mchumba wangu kuwa yeye ni mtoto wa mmoja wapo wa wagombea urais wa awamu ya tano, na kuwa baba yake amehakikishiwa kuwa atashinda uchaguzi kwa kishindo na pia mataifa yote makubwa ulimwenguni yako nyuma yake, pia mganga mmoja toka Afrika Kusini, mtaalam wa madawa ya kushinda uchaguzi kwa sasa amehamia nyumbani kwao, hivyo ni wazi kuwa baba yake njia ya ikulu ni nyeupe.

Mchumba wangu ameona hiyo ni fursa ya wazi ya kuwa na mkwe rais na kaniacha kwa vimbwanga ambavyo bado vinaniuma. Mchumba wangu siku hizi ni kada wa nguvu, anampigia debe baba mkwe mtarajiwa. Kwenye mambo haya ya siasa watu tuna sababu mbalimbali za ajabu sana kwa nini unamtaka huyu awe rais na kwa nini humtaki yule mwingine.

Binafsi nataka kumkomoa mchumba wangu tu, akose baba mkwe rais. Lakini hayo yote tisa, katika kipindi hiki kigumu nimechukua uamuzi wa kutafuta mchumba mwingine, na nimepania lazima awe bomba kuliko huyu aliyenitoroka. Ukinikuta barabarani usishangae ninapoonekana kila mdada namuangalia kwa makini, ni kuwa tu akili yangu iko bize kutathmini nani zaidi.

Juzi katika pitatapita yangu nikawa kwenye uwanja wa kuegesha magari wa maduka maarufu, hapa ni kitovu cha wadada bomba kufika wakiwa katika mipango yao ya kununua vitu mbalimbali. Kama kawaida nikiwa katika tathmini ya mchumba bomba, kwa mbali akatokea binti mmoja akiwa anaelekea kwangu, aise yaani roho yangu ikashtuka.

Sijawahi kuona binti kaumbika kama yule, palepale nikaamua huyu ndiye niliyekuwa namtafuta. Akawa anaelekea nilikokuwa, akatabasamu, ilikuwa kama kwenye sinema, mambo yote yalikuwa slow moshen, akanyanyua mkono kunipungia, nami nikanyanyua mkono na kumpungia, huku  kimoyomoyo nikishukuru Mungu kwa kunichagulia kiumbe kama huyu kuwa wangu wa maisha tena bila mimi kusema hata neno moja.

Tukasogeleana tukipungiana mikono, tulipokaribiana kama hatua kumi, nikashangaa, kumbe alikuwa anampungia mkono mtu aliyekuwa nyuma yangu, tulipopishana nikabaki mkono hewani, sikujua niushushe au ubaki juu. Nikauteremesha taratibu na kujidai nilikuwa najikuna kichwa. Machozi yakanilengalenga.

Leave A Reply