The House of Favourite Newspapers

Siri 5 Mauaji Msikitini!

0

Na Waandishi Wetu, UWAZI

MWANZA: Usiku wa kuamkia Mei 19, mwaka huu ni wa kukumbukwa kwa wakazi wa Ibanda Relini Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana kufuatia watu nane wanaodhaniwa ni magaidi kuvamia Msikiti wa Rahmani na kuua waumini watatu kwa kuwakata mapanga, sasa nyuma ya mauaji hayo kuna siri 5, Uwazi limechimba.

Watu hao walijitambulisha kuwa, wao ni wa kutoka Kundi la Islamic States ‘IS’ huku wakionesha bendera nyeusi yenye maandishi ya Kiarabu.

CHANZO CHA MAUAJI

Ilidaiwa kuwa, kundi hilo liliingia msikitini hapo na kuwauliza waumini hao ni kwa nini wanaswali wakati kuna wenzao wamekamatwa na polisi wa jijini Mwanza kwa madai ya ugaidi. Hivyo waumini hao hawakupaswa kuswali bali kwenda kupambana na polisi ili kuwatoa wenzao.

Tayari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Ahmed Msangi alishakiri kushikiliwa kwa watu hao wanaodhaniwa kuwa magaidi, lakini akatoa angalizo kwa wote wanaotaka kutumia nguvu kuwatoa watuhumiwa hao.

NI MKAKATI WA MUDA MREFU

Madai ya kundi moja kutangaza mkakati wa kuwatoa wenzao walio gerezani yalianza muda mrefu ambapo mwaka jana, mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kaisi Bin Abdullah (mtazame ukurasa wa mbele amevaa ninja) alisambaza video akianika mkakati huo kama njia ya kulipa kisasi kwa wenzao wanaoshikiliwa nchini kote kwa madai ya uhalifu.

Katika video hiyo, Kaisi alisikika akisema: Tumeshaungana ili kupambana. Mkoa wa Mtwara zaidi ya wenzetu 17 walikamatwa kwa makosa ya dhuluma, makosa ya kupanga makosa ya ugaidi. 21 wamekamatwa Zanzibar wako katika Gereza la Segerea (Dar). Wenzetu wengine 18 wamekamatwa Mwanza wako katika Gereza la Kisongo, Arusha. Ndugu zangu, wenzetu wengine 17 wameuawa Mtwara kwa amri ya …(anamtaja waziri).

“Subira yetu imefika mwisho na tulichokuwa tunasubiri Mungu ameshatupa. Tunatoa ahadi kilichopo hivi sasa tunatoboa jahazi wote tuzame. Tunatoa rai, wenzetu waliopo Gereza la Kisongo waachiwe huru. Hapa hatumtishi mtu yeyote yule.”

MKUU WA JESHI LA POLISI ALITIA NENO

Baada ya kunaswa kwa video hiyo, waandishi wa Global Publishers walitia timu kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu na kuzungumza naye kuhusu mtu huyo na kumkabidhi video ambapo alisema:

“Nawashukuru sana kwa kuleta video hii. Huu ndiyo ushirikiano unaotakiwa, nawaomba wananchi video za aina hii wazikatae kwa sababu ni kosa kuwa nazo na watu kadhaa wameshakamatwa kwa kuwa nazo.

“Sisi kama jeshi la polisi tunajua kuwa kuna watu wanadhani kufanya uhalifu kama huo kutawasaidia kutimiza matakwa yao, lakini ukweli ni kwamba polisi wapo imara na nina uhakika watuhumiwa watakamatwa kwa kushirikiana na raia wema.”

Amina Salumu mke wa Feruz Ismail akihojiwa na wanahabariUJUMBE WA KUTODHARAULIWA

Kwa mujibu wa chanzo chetu, siri ya kwanza ya mauaji hayo ilitokana na ukatili wa watu hao ambapo walionesha kuwa, endapo wasingemwaga damu, dhamira yao ya kutaka kuwakomboa wenzao polisi isingekuwa na nguvu.

“Wakati wanalazimisha waumini kulala, mmoja alisema; ‘lazima tumwage damu ili watu wajue hatuna utani. Tusipomwaga damu watatudharau hawa,’” alisema mmoja wa walionusurika akiwakariri watu hao huku akiomba hifadhi ya jina lake.

KUITISHA SERIKALI

Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye anasema aliwashuhudia watu wao wakiwa wanaondoka, alimsikia mmoja akisema; ‘serikali si inataka kuambiwa kwa vitendo, hivi ndivyo vitendo sasa. Hakuna kumwabudu Mungu mpaka haki ipatikane.’ (akimaanisha wenzao waachiwe).

Askari Polisi wakiingia ndani ya msikiti kufanya uchunguziWALITOA ONYO

Mmoja wa waumini wa msikiti huo ambaye pia hakupenda kuandikwa jina gazetini, alisema mauaji hayo yalifanywa na watu hao baada ya kuwatumia salamu mapema waumini wasisali lakini walipogundua watu wanasali wakaona wamepuuzwa.

“Tunasikia walituma ujumbe wa onyo tangu awali kwamba waumini wasisali washughulikie kuwatoa wenzao. Sasa walipobaini watu wameingia kuswali wakajikusanya na kuja kufanya mauaji wakiamini ndiyo dawa pekee ya maneno yao kufuatwa.

Naye kiongozi mmoja wa Bakwata Mkoa wa Mwanza ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa, kwa kawaida makundi ya watu wanaotumia mwavuli wa imani ya Kiislam kufanya mauaji, ni ya wale wanaopenda kuabudiwa kwa kile wanachokisema.

IMG_0023KUCHELEWA KUTII AMRI

Hata hivyo, siri nyingine ya tano ya watu hao kuuawa inadaiwa kuwa ni kuchelewa kutii amri. Inadaiwa kuwa, wakati magaidi hao wakiingia na kuamrisha watu kulala, wapo waliochelewa kutii wakitaka kujua kwanza wanaotoa amri hiyo ni akina nani na wana lengo gani!

“Karibia wote waliokatwa mapanga sana walichelewa kutii amri ya kulala. Walitaka kuwaona wale watu ni akina nani. Kwani lilikuwa tukio la kufumba na kufumbua. Na wao walipoona kuna ambao ni wagumu kulala, wakaanza kutembeza majambia mpaka kuua,” alisema muumini mmoja.

IMG_0027WALIBADILI SAUTI

Muumini mwingine wa msikiti huo alisema kuwa, sauti walizotumia watu hao si za asili kwani alimsikia mmoja wao ambaye huenda ni kiongozi, aliwasisitizia wenzake kuhakikisha wanabadili sauti ili wasibainike.

“Zile sauti hazikuwa zao. Naamini wale watu wanatujua na sisi tunawajua, nilimsikia mmoja akisisitiza kuhusu sauti. Alikuwa akisema; ‘sauti sauti, angalieni sauti zenu.”

SIRI YA KUFICHA SURA

“Ndiyo maana walificha sura kwa kuvaa ninja. Mbona majambazi kibao tu wanaingia benki kuiba bila kuficha sura? Wale sura zao si ngeni kwetu ndiyo maana walificha,” alisema muumini huyo.

WATOTO WAWILI WAZUA UTATA

Muumini mwingine aliyenusurika katika tukio hilo yeye anasimulia kwa kirefu tangu alipoingia kwenye mlango wa msikiti huo.

 “Ilikua saa 2: 35 usiku nilipongia msikitini na kuwakuta watoto wawili wageni. Mmoja aliketi mbele mwingine nyuma. Kwa kawaida Waislam kuwa hatuulizani na kuwa na wageni wa kawaida, kumbe sivyo. Naamini walikuwa kwenye mpango.

“Baada ya muda nikasikia watu wakiingia na kutuamuru tusigeuke na tulale pale tulipo. Walimuulizia imamu wa msikiti, alipokosekana wakampata msaidizi, wakampiga shoka kichwani na kumcharanga sana huku wengine wakiendelea na mauaji, sisi tulifanikiwa kukimbia,” alisema muumini huyo.

MWINGINE HUYU

 “Mimi nilifika msikitini saa 2:40 nikiwa nimechelewa, nikaenda kujipanga mbele. Wakati tunamalizia Rakaa ya mwisho, tukasikia watu wanaingia wakatuambia hapohapo mlipo laleni chini, wakasema wanamtaka imam. Mimi nilijua ni polisi kumbe siyo, wakamchukua Ostadh Feruz wakampiga bapa kwanza, alipopiga kelele wakamkata panga, lakini kumbe vipaza sauti vya msikitini vilikuwa wazi, wakavizima.

“Walizima taa na kuanza kumchinja Ostadhi tukiwa tunaona huku wakisema nyiye badala ya kupigana mnasalisali, mnasali nini kwanza mmetusaliti.

“Kiongozi wa kundi hilo alikuwa mwanamke, akaanza kuamrisha kwa kusema;  ‘chinja na huyu.’ Alipofika mtu wa tatu, yule mwanamke akasema; ‘watoto wasichinjwe.’ Baada ya kusema hivyo mimi nikachoropoka na kuanza kupiga kelele, na wao wakaondoka.”

KISA CHA WALIOKAMATWA

Kutokana na eneo la Ibanda Relini kuwa  nje kidogo ya Jiji la Mwanza, inadaiwa limekuwa likitumiwa kufanya mafunzo ya kigaidi kwa baadhi ya watu wa eneo hilo ambao walikuwa kwenye Kikundi cha Al Shabaab hivyo, baada ya jeshi la polisi kupata taarifa walifanya msako na kuwakamata watu kadhaa ambao ndiyo chanzo cha magaidi hao kuvamia msikitini na kuwaambia wenzao wasisali.

MKE WA MAREHEMU

Amina Salumu ni mke wa marehemu, Ostadh Feruz Ismail Elias, alisema siku ya tukio, mume wake aliondoka nyumbani saa 2:15 kwenda msikitini kuswali lakini baada ya muda mfupi alisikia kelele za watu huku kukiwa na milipuko msikitini hapo.

“Lakini polisi walipofika eneo la tukio tayari mume wangu alikuwa ameshafariki dunia. Naiomba Serikali ijitahidi kuwakamata waliohusika na tukio hili ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Amina.

JESHI LA POLISI

Kutokana na tukio hilo kuvuta hisia za wengi ndani na nje ya Jiji la Mwanza, jeshi la polisi mkoani hapa kupitia kwa Kamanda Msangi, limesema waliouawa katika tukio hilo ni  Feruzi Isamail Eliasi (27) kabila Muha, Imamu wa msikiti huo na mkazi wa Ibanda Relini, Mbwana Rajab (40) kabila Mbondei na Khamis Mponda (28) dereva wa kiwanda cha samaki na mkazi wa Mkolani.

Aliyejeruhiwa vibaya ni Ismail Abeid  (13) mwanafunzi wa  Shule ya Kiislam ya Jabari iliyoko Nyansaka, anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Butimba.

Feruzi Isamail Eliasi (27) na Khamis Mponda (28) walizikwa Mwanza na Mbwana Rajab (40), alizikwa Tanga.

Leave A Reply