The House of Favourite Newspapers

Siri IGP Sirro Kumpigia Saluti Jokate

0

DAR: Hoja moto iliyokuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki iliyopita ilikuwa ni kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, DC Jokate Urban Mwegelo kupigiwa saluti na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro.

 

Mchachua mada mtandaoni aliandika kwenye mtandao mmoja maarufu wa kijamii (jina kapuni) hivi;

“Mhe DC Jokate Mwegelo kupigiwa saluti na CDF (Mkuu wa Majeshi, Venance Mabeyo) na IGP. Kiitifaki imekaaje?”

 

Katika hoja hii kuliambatanishwa pia picha zilizoonesha DC Jokate akiwa anapigiwa saluti na wakuu hao wa vyombo vya usalama nchini hivyo wachangia kuanza kukomenti yao, kila mmoja kwa ufahamu wake na kuzua sintofahamu kwani wengi waliona kitendo hicho kuwa siyo sahihi.

 

Kufuatia mjadala huo kukosa mtu wa kufunga kwa hoja, mwandishi wetu alimtafuta mtaalam wa masuala ya kidiplomasia nchini, Abbas Mwalimu ambaye alifafanua kwa kina jambo hilo kama ifuatavyo;

 

“Ni kweli picha zinawaonesha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jenerali Venance Mabeyo na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro wakimpigia saluti Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mheshimiwa Jokate Mwegelo na mjadala wake niliziona.

 

“Hiyo ilifanyika kwenye sherehe za uzinduzi wa mradi wa maji wa Kibamba-Kisarawe uliofanywa na Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli Jumapili ya Juni 28, mwaka huu kwenye Viwanja vya Shule ya Chanzige, Kisarawe.

 

“Kwenye uwanja wetu wa Diplomasia tulipokea simu na meseji nyingi kutoka kwa wadau mbalimbali wakitaka kufahamu hili lipoje katika muktadha mzima wa itifaki.

 

“Kwa kuona umuhimu wa kutolea ufafanuzi suala hili ilibidi nasi tujipe muda ili kupata maelekezo kutoka kwa mamlaka husika kabla ya kutoa ufafanuzi wa kiitifaki kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” alisema Abbas na kuongeza;

“Hivyo basi ufafanuzi wa suala hilo ni huu,” alisema na kuanza kutiririka hoja kama ifuatavyo;

 

“Mkuu wa Wilaya (DC) ni mteule wa Rais. Ni mamlaka iliyoteuliwa na Rais ambayo inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni, Taratibu na kwa niaba ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye aliyemteua.

 

Ibara ya 35 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza:

35.-(1) Shughuli zote za utendaji za Serikali ya Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na watumishi wa Serikali kwa niaba ya Rais.

 

35.-(2) Amri na maagizo mengine yanayotolewa kwa madhumuni ya ibara hii yatathibitishwa kwa namna itakavyoelezwa katika kanuni zilizowekwa na Rais, kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.

Kwa maelezo hayo ya Katiba tunaona kuwa DC (Mkuu wa Wilaya) ni muwakilishi wa Rais katika ngazi ya wilaya.

 

Hii imeelezwa wazi katika Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake mbalimbali:

 

Ibara ya 36.-(2) Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuzi unaofanywa na Rais.

 

Kwa tafsiri ya kikatiba hapa tunaona kuwa DC ni cheo cha mamlaka au madaraka ya kiuongozi na kwa utaratibu wa jeshi ni kwamba Afisa ama askari hupigia saluti mamlaka ya kiuongozi.

 

SALUTI NI NINI HASA?

Saluti ni salamu ya kijeshi. Ni kuonesha heshima kwa mamlaka iliyo juu yako.

Tufahamu kuwa, katika nchi za kidemokrasia (maana yake siyo za kijeshi) mamlaka za kiraia ndizo zinazoongoza mamlaka nyingine hivyo mamlaka za kiraia zinachukuliwa kuwa zipo juu ya mamlaka nyingine zote.

 

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 148 (1) inamtaja Rais kama “Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi”.

Ibara ya 148 (2) inamueleza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuteua makamanda wa Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Saluti hutolewa kwa Commissioned Officers (askari mwenye nyota moja na kuendelea) wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwa wameteuliwa na Rais kwa kuapa hivyo.

 

Ufafanuzi wa kina hapa ni kwamba mwenye mamlaka ya kumpa cheo cha nyota askari wa JWTZ ni Rais wa Jamhuri.

Kwa msingi huo wanajeshi huwapigia saluti wateule wote wa Rais yaani Commissioned Officers kwa kuwa waliapa kwa kiapo cha Rais kwa kuwa Rais ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Kwa vyombo vingine vya usalama kama Polisi na Magereza au Uhamiaji wanajeshi huwapigia saluti maafisa wenye kamisheni ya Rais tu yaani Afisa ambaye utendaji kazi wake umeidhinishwa na Rais ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu hapa tunazungumzia ngazi kuanzia Makamishina.

Askari au mpiganaji humsalimia afisa au askari kamanda au afisa humsalimia mteule wa Rais kwa kula kiapo cha Rais.

Askari akiwa kwenye vazi la kiraia na akamsalimia mkuu wake kwa kukakamaa afisa aliye kwenye vazi rasmi la kijeshi (uniform) humpigia saluti askari huyo.

Afisa au kamanda atapokea saluti kwa saluti akiwa kwenye uniform tu.

Ikiwa anaepigiwa saluti ni mamlaka ambayo haijapitia mafunzo yoyote ya kijeshi atapokea salamu kwa namna anayoona yeye inafaa (kama alivyofanya Mheshimiwa Jokate).

 

Lakini kama mamlaka inayopigiwa saluti imepitia mafunzo ya kijeshi, basi mteule huyo ataonesha ukakamavu kama hayupo kwenye vazi la kijeshi.

Kama mamlaka inayopigiwa saluti imepitia mafunzo ya kijeshi basi mteule huyo atapokea saluti kwa kujibu kwa saluti pia kama yupo kwenye vazi la kijeshi.

Raia wa kawaida hatakiwi kujibu saluti kwa namna yoyote ile ya ukakamavu isipokuwa tu kwa kuonesha heshima inayostahili.

 

Kwa mfano wakati wa kuapishwa, DC, RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) RC (Mkuu wa Mkoa) anayeapishwa akiwa amepitia mafunzo ya kijeshi anapaswa kuapishwa akiwa kwenye uniform au sare za kijeshi husika.

Ingawa saluti ya kijeshi hutolewa kwa wateule hao wa Rais, lakini mamlaka ya kutoa amri kwa jeshi au wanajeshi hubaki kwa Rais ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na kwa wateule wengine wa jeshi ambao wamekasimiwa mamlaka na Amiri Jeshi Mkuu.

Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 148 (1) ya Katiba.

Hivyo basi kupigiwa au kupiga saluti kwa DC wa Wilaya ya Kisarawe, Mheshimiwa Jokate Mwegelo kijeshi ni ishara ya kutambua mamlaka iliyosimikwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dk John Pombe Joseph Magufuli.

 

KWA UFUPI SALUTI HUPIGWA KWA:

(1) Afisa wa Jeshi wa ngazi tajwa.

(2) Mteule wa Rais.

(3) Waliotangulia mbele za haki (kufariki dunia) sambamba na wanyama wenye hadhi ya kijeshi.

Kwa waliotangulia mbele za haki wao huhesabiwa kama Wafalme au Malkia.

Kama marehemu ni wa kiume, basi atahesabiwa kama Mfalme na kama marehemu ni wa kike atahesabiwa kama Malkia.

Ni heshima ya pekee kuwaheshimu waliotangulia kwa Mungu kwani wao wanakuwa Seniors (waandamizi) kwa wote walio hai.

 

KUTOKA KWA MHARIRI

Shukrani za kipekee zimuendee Mwanadiplomasia Abbas Mwalimu kwa ufafanuzi huu ambao tunaamini utakuwa umeondoa wingu lililokuwepo kwenye tukio la IGP na CDF kumpigia saluti DC Jokate, litakuwa limeondoka rasmi.

Stori: Mwandishi Maalum, Ijumaa

Leave A Reply