The House of Favourite Newspapers

Siri Jokate Kuteuliwa Mkuu wa Wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Pwani, Jokate Mwegelo.

 

MTU akipata mafanikio ya kushangaza, imezoeleka na wengi kuuliza: “Hebu nipe siri ya mafanikio yako?” Hata kwa Miss Tanzania Namba 2 2006, Jokate Mwegelo kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Pwani swali linalofaa kuuliza ni hilo, Wikienda linakuchambulia.

 

Haikutarajiwa na wengi kwa Jokate kupewa nafasi hiyo ya kiserikali lakini ni kama ‘mlivyosikia’ ambapo siri iliyompa ukuu huo imevuja.

Uchunguzi na uchambuzi wa wafuatiliaji wa duru za kisiasa umeonesha kuwa sababu za Jokate kupewa nafasi hiyo imetokana na mrembo huyo kuwa na elimu, uwezo wa kufanya kazi hasa za jamii na weledi katika maisha yake.

 

“Mtu hachaguliwi kuwa mkuu wa wilaya kutoka gizani, lazima taarifa zake ziwe wazi na athibitishie anayemteua kuwa uwezo wake hauna shaka.

 

“Kwa Jokate anafaa, ni msomi, ana Shahada ya Sayansi ya Jamii na Falsafa, amefanya kazi nyingi za chama (CCM) pale makao makuu lakini ni mtu anayejiheshimu, sasa hizi ndiyo sifa za msingi za kiongozi,” alisema Omary Hussein mchambuzi wa masuala ya kisiasa aishiye Tegeta jijini Dar.

 

Jokate anatajwa kumsaidia kazi mbalimbali mwenyekiti mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kherry James.

Aidha, uchunguzi unaonesha kuwa maisha ya mrembo huyo aliyajenga katika msingi mzuri tofauti na baadhi ya masupastaa wenzake wa kike na kwamba mara nyingi amekuwa ni mtu mwenye uwezo wa kujitenga na mambo yaliyo kinyume na maadili.

 

Katika siku za hivi karibuni Jokate alionekana kuishi maisha yenye utulivu mkubwa, jambo ambalo linatajwa kuwa limechangia kwa kiasi kikubwa kumuwezesha kupewa nafasi hiyo ya kutumikia wananchi.

 

Baada ya Rais Dk. John Magufuli kufanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya gumzo lilikuwa kwenye uteuzi wa Jokate, Jarry Muro (Arumeru- Arusha), Moses Machali (Nanyumbu -Lindi ), Patrobas Kitambi (Dodoma) na David Kafulila aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa Songwe hiyo ni kwa sababu baadhi yao wametoka kambi ya upinzani isipokuwa Murro na Jokate.

Comments are closed.