visa

SIRI UTAJIRI WA JUX YAVUJA!

DAR ES SALAAM: Kama ulikuwa hujui, habari ikufikie kwamba staa mwingine wa Bongo Fleva, Juma Mussa ‘Jux’ ana ukwasi wa kutosha, Gazeti la Ijumaa limeingia mzigoni na kuibuka na siri nyuma ya mafanikio yake!

MTANDAO YA KENYA YAMTAJA

Kwa mujibu wa mitandao maarufu habari za mastaa nchini Kenya, Jux ni miongoni mwa wasanii ambao kwa sasa wamekuja kwa kasi kwa mafanikio na ana utajiri unaokadiriwa kufikia shilingi bilioni 2 za Kitanzania. Kwa mujibu wa mitandao hiyo, utajiri huo unatajwa kujumuishwa na mali anazomiliki ikiwemo ghorofa moja lililopo jijini Dar.

MAGARI YA KIFAHARI…

Mitandao hiyo imeeleza kwamba, mbali na kumiliki ghorofa hilo, Jux pia anamiliki magari ya kifahari likiwemo Nissan Fuga, toleo la mwaka 2010 lenye thamani ya kati ya shilingi milioni 20 hadi 40. Gari lingine analoonekana akilisukuma ni Toyota Prado lenye thamani ya kuanzia shilingi milioni 21.

Mengine ni Mercedes Benz C-Class lenye thamani ya kuanzia shilingi milioni 20 na Toyota Mark X lenye thamani ya kati ya shilingi milioni 22 hadi 36 ambayo yote ameyapata kutokana na kazi yake ya muziki. “Mtu ukishakuwa na ghorofa mjini, ukawa na magari yako ya kifahari kama hivi, kuna nini tena? “Jux mambo yanamuendea vizuri, kwa kweli anapaswa kumshukuru sana Mungu,” kilisema chanzo.

SIRI YA MAFANIKIO

Vyanzo mbalimbali vilivyozungumza na Gazeti la Ijumaa vimeweka wazi kuwa, siri kubwa ya utajiri wake ni biashara ya mavazi pamoja na muziki. “Yuko vizuri, kijana unajua tangu ameanza kufanya muziki wa kimataifa, amekuwa akifanya shoo zake huku pia akifanya biashara ikiwemo lebo yake ya mavazi inayoitwa African Boy. Wewe unavyoona mtu anashusha ghorofa ujue kabisa kwenye akaunti yake kuna shilingi bilioni kadhaa, siyo kitu cha ajabu.

 

“Lile ghorofa analolijenga hadi likikamilika linaweza kufika hata shilingi bilioni moja, sasa unaweza kuona ni jinsi gani bwa’mdogo yuko vizuri,” kilieleza chanzo kilicho karibu na Jux. Gazeti la Ijumaa liliingia mzigoni na kuweza kunasa picha za ghorofa la Jux pamoja na baadhi ya maduka yake ya Sinza, Kinondoni na Kariakoo jijini Dar bila kusahau magari yake.

MWENYEWE ANASEMAJE?

Gazeti la Ijumaa lilipomtafuta Jux ili kuweza kupata ukweli na kumaliza manenomaneno kuhusu ghorofa na magari anayomiliki alisema hawezi kutaja kwa sbababu kuna wengine hawana kwa hiyo si vizuri kutaja, lakini anamshukuru Mungu kwa kile alichomjalia.

“Ni kweli mafanikio yangu yanatokana na biashara, lakini muziki ni biashara nyingine pia inayojitegemea.

“Idea ya bishara ya mavazi niliipata kwa sababu mimi napenda fasheni na watu wengine wanavyopenda ninavyovaa ndiyo maana nikaamua kufanya kitu kama hicho, lakini kwa upande wa shoo siyo kwamba sipati, zinakuja shoo, lakini kuliko kufanya shoo tu ni lazima ufanye shoo bora.

UTAJIRI JE?

“Kuhusu utajiri siwezi kuongea, lakini nashukuru Mungu ninapata riziki ingawa ni siri siyo vizuri kutaja na pia ninamiliki magari tofautitofauti, lakini huwa sipendi kuzungumzia kuhusu mali kwa sababu kuna mtu mwingine hana hata gari halafu mimi nitaje magari na kuna mwingine hana nyumba ya kuishi mimi nikataja pia kikubwa nashukuru Mungu tu na pia watu waendelee kunisapoti kwa African Boy,” alisema Jux aliyedumu kwenye penzi miaka kadhaa na mwanadada Vanessa Mdee ‘V-Money’ kabla ya kutengana hivi karibuni.

Jux mwenye umri wa miaka 30, kwa sasa yupo kwenye mahusiano na mwanadada mrembo Nayika, raia wa nchini Malaysia.

NYIMBO ZAKE

Miongoni mwa nyimbo zake kali ni pamoja na Nimedata, Mwambie, Uzuri Wako, Nitasubiri, Sisikii, Juu na Utaniua.

ALBAMU MPYA

Juzikati, Jux alizindua albam yake mpya inayokwenda kwa jina la The Love kwenye Mgahawa wa Akemi uliopo Posta jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wasanii wengi akiwemo Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ ambaye alipafomu kwa mara ya kwanza tangu augue kwa muda mrefu.

Uzinduzi wa albam hiyo yenye takriban nyimbo 17, uliambatana na uzinduzi wa bidhaa mpya za Jux zenye nembo ya African Boy ambazo ni pafyumu, raba, boxer na matoleo mapya ya bidhaa zake za zamani kama vile T-Shirt, kofia pamoja na vingine kibao.

Stori: Neema Adrian, Ijumaa
Toa comment