visa

Siri Vurugu za Risasi Kwa Aunt, Iyobo

KWA wale wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii, sakata la vurugu zilizoambatana na mirindimo ya risasi kwenye pub (baa) ya staa wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel iitwayo The Luxe maeneo ya Mikocheni jijini Dar, watakuwa wanataka kujua ni nini hasa kilitokea.

Gazeti la Ijumaa limechimba kwa undani sakata hilo na kuibuka na siri kadhaa nyuma ya pazia.

KWA WASOMAJI WAPYA

Wikiendi iliyopita, Aunt aliangusha bonge la pati la siku yake ya kuzaliwa ‘bethidei’ kwenye pub yake hiyo iliyopo maeneo ya Mikocheni A jijini Dar. Majira ya saa tisa za usiku ndipo risasi ziliporindima kwenye baa hiyo na kusababisha taharuki kwa waliokuwa ndani na waishio jirani na eneo hilo.

Mmoja wa waliokuwa eneo la tukio ni shushushu wa Gazeti la Ijumaa ambaye anaeleza kuwa, jamaa mmoja aliyekuwa na bastola, alifyatua risasi mbili hewani, akidai kukerwa na kelele zilizokuwa zinaendelea siku hiyo ambazo zilisababisha Aunt aumalizie usiku wake kwenye kituo cha polisi pamoja na jamaa huyo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.

PUB YAFUNGWA

Kesho yake, pub hiyo ilifungwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukiuka masharti ya uendeshaji na leseni ya biashara kwa kupiga kelele kupita kiasi katika maeneo ya makazi ya watu.

SIRI ZAVUJA

Vyanzo mbalimbali vilivujisha siri kuhusu sababu zilizosababisha pub hiyo ifungwe. Kuna vyanzo vilieleza kuwa ni kwa sababu ya Aunt alitangaza kurudiana na mzazi mwenzake, Moses Iyobo ‘Moze Iyobo’.

“Iyobo ni kama ana gundu vile, maana ile anarudiana tu na Aunt ndipo kikanuka. Nasikia yule jamaa aliyefyatua risasi ndiye aliyekuwa anasimamia shoo wakati Aunt na Iyobo wameachana, sasa alipoona wamerudiana ndipo akakinukisha,” chanzo kimoja kililieleza Gazeti la Ijumaa na kuongeza;

“Kama uliona, jamaa yule alifyatua risasi hizo wakati ambao Aunt anaoneshana mahaba na Iyobo, wakati sherehe ilipokuwa ikiendelea.”

CHANZO KINGINE

Chanzo kingine kilieleza kuwa, sababu nyingine iliyosababisha vurugu hizo hadi pub kufungwa ni kuwepo kwa mgogoro uliomhusisha mmiliki wa nyumba hiyo na mtu mwingine aliyekuwa anadai eneo hilo ni mali yake.

“Nilisikia kuna mgogoro pale wa ile nyumba kwa kipindi kirefu kabla hata Aunt hajapewa kupakarabati na kuifanya iwe pub,” kilisema chanzo hicho.

AUNT MWENYEWE APASUA JIBU

Gazeti la Ijumaa lilimtafuta Aunt na kukaa naye kitako kisha kumuuliza kama kweli Iyobo ana gundu na ndiye aliyesababisha pub hiyo kufungwa? Aunt kwa mshangao mkubwa alisema si kweli kwamba mzazi mwenzake ndiye chanzo au ana gundu kama walivyodai baadhi ya watu mitandaoni.

“Siyo kweli, hayo ni maneno tu ya watu huko mitandaoni na huwezi kuwazuia watu kusema kile wanachojisikia kwani hiyo ndiyo athari mojawapo ya mitandao.

“Ukweli ni kwamba kweli kulitokea vurugu hizo ambazo zilinifikisha polisi, lakini sababu ambazo mimi naamini ni mbili;

MOSI

“Pale pub watu walikuwa hawajui, kulikuwa au kuna mgogoro wa muda mrefu tu na si kwamba Iyobo alivyofika pale ndiyo tatizo likaanza, hapana, ni kitu ambacho kilikuwepo na kilikuwa mahakamani,” alisema Aunt bila kueleza kwa undani kuhusu kesi hiyo.

MBILI

Sababu ya pili ambayo Aunt alikubaliana nayo kwamba ina ukweli ni ile ya watu kukerwa na kelele ya muziki, jambo ambalo alikuwa akikabiliana nalo mara kwa mara.

“Hiyo ya kelele sawa, sikatai maana kiukweli muziki ulikuwa unawakera majirani, lakini hao wanaosema sijui kuna sponsa ambaye alimaindi kuona nimerudiana na Iyobo, ni uzushi tu unaopaswa kupuuzwa,” alimaliza Aunt.

RPC ANASEMAJE?

Gazeti la Ijumaa lilimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Musa Taibu ili kuweza kujua anazungumziaje tukio hilo na hatua ambazo wamezichukua kwa mtu aliyedaiwa kufyatua risasi angani, lakini kwa bahati mbaya simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa. Jitihada za kumtafuta kamanda huyo zinaendelea.

Stori: Waandishi Wetu, Dar
Toa comment