The House of Favourite Newspapers

Siri Ya Mafanikio Ni Kujituma Kwa Bidii

TUMEANZA mwaka mpya wa 2018. Hili ni jambo jema na kila mmoja wetu aliyebahatika kuona mwaka huu ni vizuri kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Ni muhimu kufanya hivyo kwa sababu ndiye anatusaidia kujua leo na kesho inakwendaje, lakini pia kusimamia shughuli zetu mbalimbali.

 

Baada ya kusema hivyo napenda kutilia mkazo mambo ambayo viongozi wa dini waligusia hususan suala la kutunza amani ya nchi yetu.

Pia nitagusia namna viongozi hao walivyotoa ushauri kwa Watanzania kuhusu kumsaidia rais ili atimize majukumu yake inavyotakiwa.

Jambo la msingi hapa ni kuhakikisha amani yetu inalindwa kwa gharama yoyote kwa sababu ikivurugika wote tutakuwa tumeharibikiwa.

 

Kwa hiyo tusikubali kamwe amani yetu icheze kwani huo ndiyo usalama wa kila mmoja wetu na nchi kwa ujumla wake. Tuitunze kweli kweli.

Hata kama nchi ina utajiri mkubwa kiasi gani, bila amani ni kazi bure. Bila amani hatuwezi kufanya siasa. Bila amani kila kitu kinakwenda ovyo ovyo.

Kwa hiyo ndugu zangu bila kuangalia vyama, dini au makabila tunayotoka, tuhakikishe amani yetu inalindwa kama mboni ya jicho.

 

Watoto waambiwe hivyo, vijana waambiwe hivyo, wanafunzi waambiwe hivyo, wafanyakazi waambiwe hivyo na makundi mengine yaambiwe hivyo.

Tunafahamu nchi ambazo hazina amani watu wake wanavyosumbuka na serikali inavyohangaika kuirejesha baada ya kutoweka.

Tuangalia nchi jirani zilizotuzunguka. Wanakesha usiku na mchana kutafuta amani na watu wao kukimbilia kwetu, wanaacha nyumba zao, mifugo yao, mashamba yao na kila kitu chao. Kwa lugha nyingine ni kwamba sisi Mwenyezi Mungu anatupenda ndiyo maana anatulindia amani yetu.

 

Kuhusu kumsaidia rais ni lazima tuhakikishe tunafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuharakisha maendeleo yetu na nchi kwa ujumla.

Suala hili amelisisitiza vizuri Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Mwadhama Pengo aliwataka Watanzania kuutumia mwaka 2018, kufanyakazi kwa bidii usiku na mchana ili kuharakisha maendeleo.

“Ninachowaomba ni kufanya kazi tena zile zinazompendeza Mungu na kulinda utu wa watu. Kwa kufanya hivyo lazima jamii itabadilika na kuwa na jamii ya amani zaidi,” anasema Pengo.

Hoja kama hiyo ilitiliwa mkazo pia na viongozi wengine wa dini, hivyo ninachotaka kusisitiza hapa Watanzania tunahitaji kujituma zaidi.

 

Ni lazima tunapoanza mwaka mpya tuhakikishe tunabadilika, tuache kufanya vitu kwa mazoea na badala yake tufanyie kwa vitendo.

Tukiishia kulalamika kwamba kuna tatizo hili na lile, haitasaidia, muhimu ni kutafuta majibu ya matatizo yetu kwa kujiwekea mikakati ya kuyakabili.

Kama ni tatizo la ajira ni lazima kila mmoja wetu aumize kichwa namna ya kubuni mradi au shughuli inayoweza kumkwamua na umaskini.

Hili linahusu kila moja, ambapo serikali inatakiwa ijitahidi kuweka mazingira rafiki zaidi ya watu kufanya shughuli zao hususan kwa sekta binafsi.

Ni muhimu serikali iwekeze nguvu kubwa kunyanyua sekta binafsi kwani inaonekana ni mkombozi wa ajira nchini kwetu.

 

Hii ikiwa na maana kama ni mikopo sekta binafsi ipatiwe kwa masharti nafuu ili iwe rahisi kwa sekta hiyo kupanua wigo wa shughuli zao.

Katika hili Rais Dk. John Magufuli anatakiwa kuingilia kati ili taasisi za kifedha zinazotoa mkopo zisaidie zaidi sekta binafsi ili ipige hatua zaidi.

Endapo sekta hiyo itawezeshwa vizuri pamoja na kuboresha sekta ya kilimo kuna uwezekano mkubwa wa kufungua fursa za ajira.

Si hivyo tu, kuna umuhimu zaidi wa kuboresha sekta ya viwanda kama serikali ya Rais Magufuli ilivyodhamiria kwani itasaidia pia kwenye ajira.

Kwa hiyo katika mwaka huu mpya wa 2018 kama nilivyotangulia kusema awali, nguvu zetu kubwa ni pamoja na kulinda amani yetu.

Pia kuhakikisha kila mwenye uwezo wa kufanyakazi halali anafanya ili kupiga vita nchini kwetu na kuondokana na utegemezi.

Tukiamua inawezekani kwani waliofanikiwa walianzia mahali na kufikia hapo walipo.

Kama alivyowahi kusema kiongozi mmoja wa Marekani, Colin Powell kwamba, “hakuna siri ya mafanikio, ni matokeo ya maandalizi, kufanyakazi kwa bidii na kujifunza kutokana na kushindwa.”

Ni imani yangu kuwa pale tulipojisahau mwaka jana tupafanyie kazi mwaka huu ili kuhakikisha tunaleta mabadiliko chanya kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla wake.

Jipu limepasuka, siwezi

kuwa adui kwa kusema ukweli

NAPASUA JIPU ERIC SHIGONGO, DAR ES SALAAM

Comments are closed.