The House of Favourite Newspapers
gunners X

Siri Ya Zuchu Sauzi Yafichuka

0

HIVI karibuni, staa mpya wa kike wa Bongo Fleva anayetumikia Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Zuhura Othman ‘Zuchu’ alisafiri kwenda nchni Afrika Kusini (Sauzi) ambapo siri ya safari hiyo imefichuka, IJUMAA limedokezwa.Habari za ndani ya Wasafi zinadai kwamba, mbali na kwenda kuungana na bosi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye alikuwa nchini humo akiandaa albam yake mpya, lakini kuna mengine yaliyomhusu Zuchu pekee.

 

Imefahamika kwamba, siyo Zuchu peke yake ambaye atasikika kwenye albam hiyo ya Diamond au Mondi, lakini pia kuna mastaa wengine kama Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny ’ wa Wasafi na wengine wakubwa wa nje; yaani ndani na nje ya Afrika.

 

SIRI YA ZUCHU

Imefahamika kwamba, akiwa Sauzi, Zuchu alipata fursa ya kufanya kolabo na mastaa wakuwa wa Afrika waliokwenda kushiriki albam ya Mondi akiwemo Sho Madjozi wa Afrika Kusini.Inasemekana kuwa, wakati akiondoka Bongo, Zuchu alijiandaa vilivyo ambapo anaandaa albam yake na muda siyo mrefu atalipua bomu zito na kuzima kiki zote ambazo zimekuwa zikiendelea mjini.

HUYU HAPA FELA

Mmoja wa mameneja wa Wasafi (WCB), Said Fela ‘Mkubwa Fela’, amefichua kila kitu juu ya msanii huyo anayewika kwa sasa kwenye gemu la Bongo Fleva.

 

Katika mahojiano maalum (exclusive interview) na Gazeti la IJUMAA, Fela anasema kuwa, watu wakae mkao wa kula kwani kuna vitu vizuri vinakuja kutoka kwa mrembo huyo.

 

Fela anasema kuwa, tangu wamemsaini Zuchu katika lebo hiyo, hajawahi kuwaangusha, kwani amekuwa ni mtu wakujituma na kufanya kile ambacho mashabiki wake wanapenda, hivyo safari yake ya nchini Afrika Kusini hivi karibuni haikuwa ya bure, bali ina kishindo kikubwa ambacho kinafuata.

 

“Zuchu ni binti ambaye anajituma sana, amekuwa akifanya hivyo siku zote, sasa hivi huwezi ukataja listi ya mastaa wa kike wanaofanya vizuri kwenye gemu la Bongo Fleva, halafu ukaacha kutaja jina la Zuchu.

 

Sitaki kuongea maneno mengi, naomba mashabiki wake wakae mkao wa kula kwa sababu safari yake ya Afrika Kusini haikuwa ya bure,” anasema Fela.

 

KUZIMA KIKI

Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakidai kwamba, huenda mrembo huyo sasa hivi ataachia bonge la wimbo ambao unaweza kuzima kiki zote mjini.“Ninyi wenyewe si mnamjua Zuchu? Balaa lake huwa siyo la kitoto, binafsi naamini ataachia bonge la ngoma ambayo itakuja kuzima kiki zote zinazoendelea kwa sasa,” alisema shabiki huyo aliyefahamika kwa jina la Allen.

 

TUJIKUMBUSHE

Aprili 8, 2020, Lebo ya WCB ilitangaza kumsaini msanii huyo rasmi ambaye ni mtoto wa Malkia wa Muziki wa Taarab Afrika Mashariki na Kati, Khadija Kopa ‘Bi Khadija’.

 

Licha ya maneno kuwa mengi mitandaoni huku kila mmoja akisema lake, lakini ndani ya kipindi kifupi, mwanadada huyo amefanikiwa kuingia katika kilele cha mafanikio kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike Tanzania kufikisha wasikilizaji milioni tatu kupitia EP yake ya I AM ZUCHU ndani ya Mtandao wa Boomplay pekee ukiachana na mitandao mingine kama YouTube ambako amefunika wasanii wote wa kike ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Mbali na hilo, Desemba 2020, waandaaji wa tuzo kubwa duniani za Grammy walimripoti mrembo huyo kuwa, alifanikiwa kuingia kwenye hatua ya kujadiliwa (consideration) kwa ajili ya kuwania tuzo ya Mwanamuziki Bora Chipukizi.

 

Umaarufu wa kazi zake, kipaji, juhudi na promosheni kubwa anayoipata kutoka kwenye lebo aliyopo kwa sasa, ndivyo vitu vinavyomsaidia kuendelea kukua zaidi na zaidi na kutengeneza mashabiki ambao hawachoki kufuatilia kazi zake kila kukicha

Stori: Memorise Richard, Dar

Leave A Reply