The House of Favourite Newspapers

SIRI YAFICHUKA KILIO CHA DIMPOZI

SIRI imefichuka juu ya kilio kizito cha staa wa Bongo Fleva, Faraja Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ alipojikuta akilia kwa kunung’unika wakati wa kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba. 

 

Ijumaa lilimshuhudia Dimpoz ambaye alijumuika na waombolezaji wengine waliofurika kwenye ibada ya kumuaga Ruge kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar ambapo baada ya kuuona mwili huo alianza kuangulia kilio kilichosababisha wasanii wenzake akiwemo Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ waanze kumbembeleza.

 

Paparazi wetu alizungumza na Dimpoz ili kutaka kujua alivyoguswa na msiba huo ambapo mwanamuziki huyo aliomba aachwe kwani hana la kusema.

 

Kufuatia tukio hilo mwanahabari wetu alizungumza na mmoja wa watu wa karibu walioambatana naye ambaye alikuwa na haya ya kusema; “Ilikuwa ni lazima alie sana kwa kuwa ukiachana na kutoka naye mbali, Ruge alimsaidia sana katika harakati za kimuziki mpaka kufikia hapo alipofikia.

“Jambo lingine ambalo lilikuwa ni lazima limlize wawili hao kuna kipindi walikuwa ni mastaa waliokuwa wakiuguzwa nchini Afrika Kusini tena wote katika jiji moja la Johannesburg ambapo Watanzania walikuwa wakiwaombea kwa pamoja.

 

Katika maombi hayo ndipo yeye akafanikiwa kuinuka na mwenzake ndiyo kama unavyoona amefariki dunia hivyo ni lazima alie sana. “Maana kuna kipindi watu wengi waliokuwa wakienda  kumjulia hali hospitalini walimwambia wametoka kumtembelea Ruge na wengine baada ya kumuona yeye walimwambia wanakwenda kumjulia hali na Ruge.

“Hivyo hata wenyewe walikuwa wakiombeana baada ya kugundua kuwa Watanzania walikuwa wakifuatilia hali zao kwa pamoja,” alisema mtu huyo. Baada ya kuaga, Dimpoz alishindwa kutembea ambapo MwanaFA alipata kazi ya ziada ya kumtuliza na kumuweka chini ili atulie kidogo.

 

Mashuhuda wa tukio hilo waliokuwa wakizungumza mambo mbalimbali wakihusisha tukio la kuugua pamoja naye kupata nafuu ya kuweza hata kuhudhuria mazishi ya mwenzake. “Ilikuwa ni lazima alie kwa kuwa hata yeye mwenyewe hali yake ilikuwa mbaya sana, lakini Mungu amemsaidia kuweza kupata nafuu,” alisikika mmoja wa mashuhuda hao.

 

Hata hivyo, kitendo cha kuhudhuria mazishi hayo ni kwa ajili ya upendo wake kwa marehemu kwa kuwa hata mwenyewe bado afya yake haijaimarika vizuri. Katikati ya mwaka jana, Dimpoz aliripotiwa kuwa na hali tete baada ya kufanyiwa operesheni ya koo nchini Afrika Kusini kisha kurejea nchini na baadaye tena kukimbizwa nchini Ujerumani.

Comments are closed.