Sisi tumeifanyia nini Tanzania?

RAIS wa 35 wa Marekani, John Fitzgerald Kennedy aliwataka wananchi wake wajiulize wao wameifanyia nini nchi yao, wasiishie kuuliza taifa limewafanyia nini?

Ni msamiati mpana hasa kwenye jamii inayotaka kufanyiwa kila kitu ilhali yenyewe imebweteka; naliacha hili vichwani mwa Watanzania wenzangu ili kulipembua.

Ipo wazi kuwa wengi wetu tulipokuwa tukipima siku 100 za utawala wa Rais John Magufuli tulikuwa tukihoji ametufanyia nini? Tukasahau kujiuliza, sisi tumefanya nini katika siku hizo kwa ajili ya taifa letu?
Kwa kurejea kauli ya John mwenzake katika hotuba yake, Rais Magufuli alitukumbusha wajibu wetu wananchi wa kuhakikisha jukumu la kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi si lake pekee bali ni la kila mmoja wetu. Kifupi kazi ya kutumbua majipu tunayompongeza nayo ni yetu sote, tulipaswa kuifanya tangu zamani.

Siku tatu kabla ya hotuba ya Rais Magufuli kwa wazee wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, niliandika dokezo kwenye kundi la mtandao wa kijamii kuwaeleza rafiki zangu majuto yangu ya kutolitumikia taifa langu ipasavyo.

Majuto yangu yalitokana na kufukuliwa kwa uozo na ufisadi wa kutisha serikalini, kazi inayofanywa chini ya uongozi wa Rais Magufuli, jambo lililonifanya nijiulize kwa nini yeye na nisiwe mimi?
Ni wazi kuwa taaluma yangu inaniruhusu kufukua madudu yaliyokuwa yakifanywa na utawala uliopita hata kama yalisimamiwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, (pichani).
Pengine kinachoniumiza ni kwa nini sikufanya wajibu wangu wa kulinda mali za umma; sikuwafokea wezi wa rasilimali za taifa kwa sababu gani?
Je, nilipenda makontena zaidi ya 2,000 yatoroshwe bila kulipiwa ushuru? Niliridhia mabwanyenye wanyonye mapato ya bandari ili wanone matumbo yao na familia zao?
Wakati natafakari majibu ya maswali yangu, Rais Magufuli alinitaka nijiulize; mimi nimeifanyia nini Tanzania? Si mimi tu, rais ametutaka sote tujiulize tumeifanyia nini nchi yetu?
Maana anajua wakati wahuni wanahujumu mita za kupimia mafuta pale bandarini kwa zaidi ya miaka mitano, kuna wafanyakazi waliona hujuma hiyo lakini hawakusema; waliacha wanene waneemeke kwa kuliua taifa letu ambalo ni mali ya Watanzania wakiwemo wafanyakazi wa bandari walioona na kuunyamazia ufisadi huo.

Usiulize Magufuli amefanya nini katika siku 100, jiulize wewe umeifanyia nini Tanzania yako? Maana si jambo zuri kwa Mtanzania mzalendo kuacha nchi ikiharibiwa mbele ya macho yako halafu usubiri kumhesabia ufanisi wa siku 100 mtu ambaye hakuona tukio.
Kama taifa tumefika mahali pa kushirikiana kupambana na ufisadi kwa nguvu zetu sote. Ni wakati wa kila Mtanzania kuwajibika siyo tu kulinda rasilimali za nchi bali pia kuzalisha na kutoa mchango wa hali na mali ili kuliinua taifa letu.

Jambo la kufurahia katika awamu hii ya tano ni kwamba tumepata rais msikivu, tuna mawaziri wawajibikaji na viongozi wafuatiliaji ambao tunaweza kushirikiana nao katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuondokana na ufukara uliotutesa kwa miaka nenda rudi.
Nawaomba waandishi wenzangu tutimize wajibu wetu wa kitaaluma; madudu yanayofukuliwa si aibu kwa utawala uliopita tu; ni aibu yetu pia kwa sababu hatukuyaona na kama tuliyaona hatukuyakemea.

Nawasihi wananchi wenzangu; tusikubali kuwalea wezi wa mali zetu, nyakati za woga zimekwisha sasa ni muda wa mapambano. Ni heri kufa tukitetea taifa letu kuliko kupona huku tukiliangamiza.

Tanzania ni yetu; rasilimali zote ni zetu; tunao wajibu wa kuilinda nchi yetu na kusimamia utajiri wetu usiwanufaishe watu wachache na sisi tuishie kupiga miayo kwa njaa inayotokana na woga wetu wa kuwafichua wanaotuhujumu. Nachochea tu!

Loading...

Toa comment