Sistinho: Simba Queens Haivutii Kiuchezaji Hata Kama Inashinda
MCHAMBUZI wa soka kupitia vipindi vya michezo vya Global TV na +255 Global Radio, Sistinho wakati akitoa tathmini yake kuhusiana na michuano ya kuwania kufuzu ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake inayoendelea nchini, amesema licha ya kuwa Simba Queens inashinda mechi zake lakini haivutii aina yake ya uchezaji
“Ni ukweli mgumu kusema kwa kipindi hiki timu inashinda mabao mengi, lakini ukweli ni kwamba aina ya uchezaji ya Simba Queens haivutii hata kidogo badala yake uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja ndio umekua ukionekana kusaidia”
“Kwenye michuano hii kila timu inaonekana kuwa na utambulisho wake kiuchezaji, CBE wao husifika kwa soka la pasi fupi na la kuvutia huku pia walishinda nyingi, As Kigali na Fofila PF wao wanasifika soka la kasi na pasi ndefu pia wanashinda nyingi, hizo zote nilizotaja zimeonakana kuwa na muunganiko kiuchezaji lakini Simba Queens wao wanatambulishwa na Staili gani?”
“Hata wachezaji kadhaa ambao walikua nyota kwasasa ni rahisi sana kubezwa kwasababu hiyo, muunganiko wa kiuchezaji ni mdogo sana na ni vizuri kuyasema haya mapema ili iwe sehemu ya maboresho kuelekea Morocco kwasababu kwa asilimia kubwa najua wana uwezo wa kuwashinda As Kigali fainali kwasababu ya wachezaji wenye viwango vizuri kuamua mechi”