The House of Favourite Newspapers

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (8)

0

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (8)

ILIPOISHIA IJUMAA…

 

“Mzee Samike kwa sababu ya uchawi wake, alikwishatengwa na jamii. Watu wote walimwogopa na hawakuthubutu kwenda msibani. Japo alisimama juu ya paa la nyumba  kutangaza kwa sauti kuwa alifiwa na mjukuu, watu waliziba masikio, msiba wakaupa kisogo.

 

ENDELEA KUISOMA…

 

“Sikitiko likaingia katika moyo wa Mzee Samike. Msiba wote aliufanya peke yake. Alilia, akajibembeleza, akanyamaza na kujifariji. Akabeba maiti ya mjukuu wake kwenda kuizika katika makaburi yaliyokuletea kasheshe. Alipofika kwa sababu hakuwahi kuchimba kaburi maishani mwake, akachanganya mambo, japo ulikuwa msiba wa mtoto mchanga, alichimba kaburi la mtu mzima! Alipomaliza kuchimba, akamzika Chimota akiwa kamshikisha uchawi wa kumlinda. Apumzike kwa amani, asitokee bazazi yeyote akafukua kaburi lile au kufanya ushenzi wowote, hata kama ni kulikanyaga kwa kishindo.”

 

Mzee alimaliza kusimulia, akaweka kiko chini. Nilikuwa na maswali mengi ya kumuuliza. Nikaitumia nafasi hiyo.

 

“Nitampata wapi mzee huyu?” niliuliza.

 

“Swali zuri, ni lazima umpate ili umwombe msamaha. Akuepushe na hilo dubwana linalokukimbiza. Kwa bahati mbaya Samike alihama Chisanza miaka miwili iliyopita.”

 

“Alihamia wapi?”

 

“Kigoma!”

 

“Lazima niende huko. Nikipuuzia mtu wake wa ajabu atanimaliza.”

 

“Safi! Hakuna namna nyingine ya kupambana, ila kumwomba radhi kwa ufuska ulioufanya.”

 

“Nitawezaje kumpata nikifika huko Kigoma?”

 

“Oooh… ni rahisi sana, Mzee Samike ana muonekano wa pekee, waliowahi kupishana naye waligeuza shingo kwa sababu ya ule utofauti alionao. Ana nywele nyeupe isivyo kawaida. Ndevu nyeupe, sharubu nyeupe, kope nyeupe na uso mrefu wenye rangi ya maji ya kunde. Kwa sababu alitumia ujana wake katika kubeba tunguli za kuwangia, ana misuli minene. Samike siyo mzee, ni pande la mzee!”

 

Niliyaelewa maneno ya mzee. Nikataka kumuuliza jina lake, lakini kabla sijachomoa maneno, mlango ukasukumwa kwa kishindo, mtu wa ajabu akaingia akiwa kashika upanga uleule. Akasimama kama mwalimu anayemtafuta mwanafunzi mpiga kelele.

 

“Mtu wako kakufuata. Kimbia haraka katokee mlango wa nyuma,” mzee alinishauri.

 

Nilikimbia kuelekea ushoroba finyu uliozitenganisha kuta mbili ndefu. Sikuvisikia vishindo vya mtu wa ajabu, lakini alinikimbiza. Mlango wa nyuma niliupita kwa mwendo wa farasi wa mashindano. Nikaingia katika barabara ya mwendo kasi. Mwanadamu aendaye mbio, nikakimbia sambamba na magari yaendayo kasi. Abiria wakashika vichwa! Madereva wakaporomosha matusi.

 

Mtu wa ajabu aliendelea kunikimbiza nami nikakimbia kwa bidii ya kuyaokoa maisha. Kwa kuwa watu waliniangalia na kushangaa jinsi nilivyokuwa nakimbia, nikang’amua  kwamba, mtu yule wa ajabu hawakumwona. Ulikuwa mchezo wa mauzauza.

 

Nini hatma ya mchakamchaka huu? Tukutane kesho…

 

NA: DAUD MAKOBA| GPL

Leave A Reply