The House of Favourite Newspapers

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (19)

0

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (19)

 

ILIPOISHIA JANA…

Ndani ya mtumbwi alikuwamo mzee mmoja mwenye nywele nyeupe, nyusi nyeupe na ndevu nyeupe. Haikutosha kumuita mzee, lilikuwa pande la mzee. Nilifurahi nikatamka kwa sauti Samikeeeeeeeeeeh!

 

ENDELEA KUISOMA…

ALINITAZAMA nikagundua alilitambua jina lake. Alitia nanga haraka, kisha akasema: “We kijana unayeniita jina langu hovyo, njoo tusaidiane kushusha hawa samaki.”

 

Sikutaka kuipoteza nafasi hii adimu niliyopewa na mzee niliyemtafuta kwa muda mrefu. Nilifika kunako mtumbwi.

 

“Mzee wewe ni galacha… samaki wote hawa?” nilisema nikiwashikashika samaki. Wachache walikuwa hai, baadhi walikuwa katika kipindi cha kukata roho na wengi walikufa.

 

“Usu! Acha ulumbi wa maneno… bahari kubwa hii!” alijibu. Nikakaa kimya nikifuata maelekezo.

 

Hata kabla sijajua namna ya kuwashusha wale samaki kama alivyoomba yule mzee nimsaidie, wachuuzi walituvamia, wakawanunua samaki wale kwa pupa. Mwisho mtumbwi ulibaki na samaki wawili walionona. Inaonekana mzee alipenda samaki kuliko pesa, kwa sababu hata alipobembelezwa awauze alikataa.

 

Mzee alimwita kijana mmoja ambaye dalili zilionyesha waziwazi kuwa naye alijihusisha na masuala ya uvuvi, akamkabidhi mtumbwi wake. Baada ya hapo, akaanza kuondoka taratibu. Alinisahau.

 

“Mzee! Mzee! Mzee!” nilimwita kwa mtindo wa ‘takriri’ kuonyesha msisitizo. Aligeuka, nikazungumza, “Mzee umenisahau!”

 

“Tulipanga biashara gani?” aliuliza.

 

“Uliniambia nikusaidie kushusha samaki.”

 

“Ulinisaidia kuwashusha hao samaki?”

 

“Hapana, wachuuzi walikuja kuwanunua.”

 

“Umesahaulika kwa lipi?”

 

“Basi mzee nakutafuta muda mrefu sana! Nina shida.”

 

Mzee alicheka, akanitazama usoni kisha akasema: “Kwa sasa sisikilizi shida ya mtu, nimechoshwa na bahari, nahitaji kwenda kupumzika katika jumba langu la upweke!”

 

“Basi mzee niruhusu niongozane na wewe mpaka nyumbani kwako!” niliomba. Sikuwa tayari kumwacha mzee huyu niliyemtafuta kwa muda mrefu. Ni heri nimfuate kokote aendako ili niweze kupata tiba dhidi ya gonjwa la  kufukuzwa hovyo na mtu yule wa ajabu.

 

“Twende!” alijibu. Tukaenda.

 

Tulitembea hatua kubwakubwa mpaka tukafika alipoishi mzee. Aliishi mtaa wa sarakasi. Nyumba yake ilikuwa peke yake juu ya kilima kidogo. Mbele kiasi kama cha hatua 140, kulijengwa nyumba saba zilizokaa katika msitari mmoja. Kwa mpangilio huo, nyumba ilisimama kama askari anayeamrisha askari saba katika gwaride.

 

“Karibu mpaka ndani bwana mdogo,” mzee alinikaribisha. Nami nikajimwaga katika kiti kimoja cha mbao, huku nikiliacha jicho liichunguze nyumba ile.

 

Hatimaye Popo kampata Mzee Samike… atakubali kumsaidia?

Tukutane kesho…

 

Na: DAUD MAKOBA| GPL

Leave A Reply