The House of Favourite Newspapers

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume

1

Nilichozoea kusikia ni kwamba kuna majini wanawake wanaojigeuza binadamu na kuwatongoza wanaume. Wengi wa majini hao hutaka kuishi na binadamu kama mke na mume, jambo ambalo baadhi ya watu linawavutia kutokana na tamaa ya kupata utajiri.

Lakini nimekuja kugundua kuwa hawapo majini wanawake pekee, bali pia wapo majini wanaume ambao huwatongoza wanawake wa kibinadamu na kutaka waishi nao kama mume na mke.

Hilo ndilo lililonitokea mimi na kuniingiza katika mkasa ulioyatatanisha maisha yangu. Nilifikia mahali sasa nikawa natamani kufa.

Jina langu naitwa Enjo. Ni mtoto wa tatu katika familia ya mzee Sabastian Chacha. Wa kwanza ni mwanaume, jina lake ni Raymond au Ray kama marafiki zake walivyozoea kumuita.

Yeye anafanya kazi Uingereza. Ameshaoa na ana watoto wawili. Wa pili alikuwa mwanamke kama mimi, anaitwa Miriam. Anaishi Dar ninapoishi mimi, naye pia ameshaolewa na ana mtoto mmoja.

Kwa wanaomkumbuka mzee Sabastian Chacha aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni kisha akawa Mbunge wa Jimbo la Kibaha iliko nyumba yetu.

Mzee Chacha alifariki dunia miaka michache iliyopita kwa ajali ya gari. Miaka miwili baadaye, mama yetu naye alifariki dunia ghafla katika Hospitali ya Muhimbili kutokana na shinikizo la damu.

Baada ya masomo yangu ya chuo kikuu, nilipata kazi Wizara ya Afya. Haikutimia hata miaka miwili, nilifukuzwa kazi kutokana na sababu ambayo haikuelezwa wazi.
Lakini nilijua kuwa nilitofautiana na bosi wangu aliyekuwa akinitaka kimapenzi nikamkataa. Yeye ndiye aliyenisingizia madai ya kuwa mzembe hadi nikafukuzwa kazi.

Kulikuwa na mwanaume Mzanzibar ambaye nilikuwa na matarajio naye sana kwamba angekuja kunioa. Yeye alikuwa akisoma huko Uingereza. Kwa vile alikuwa na ndugu zake huko ambao walikuwa wakijiweza, alikuwa akinitumia pesa mara kwa mara.

Wakati ule nafanya kazi, nilipanga nyumba huko Sinza. Hiyo nyumba tulichangia watu wawili. Upande mmoja alipanga mtu mmoja aliyekuwa na familia yake na upande mwingine nilipanga mimi lakini tulikuwa tunatumia mlango mmoja.

Siku moja nilikuwa nimealikwa katika hafla iliyokuwa ikifanyika katika hoteli moja kule Masaki.Watu tulikuwa tumekaa kwenye viti tukipata vinywaji.

Katika meza ya pembeni kwangu aliketi mzungu mmoja aliyekuwa akinitazama sana.
Mzungu huyo alikuwa amevaa suti iliyokuwa imempendeza sana na alikuwa amejifunga kikuba cha rangi nyekundu shingoni. Jinsi alivyokuwa amezichonga vyema ndevu zake alionekana kama muungwana na mtu aliyejistahi sana.

Alikuwa akinywa kinywaji chake taratibu huku jicho lake likiwa upande wangu.
Sikuweza kujua ni kwa nini alikuwa akinitazama sana. Kwanza, nilidhania pengine alikuwa amenifananisha na mtu aliyekuwa anamfahamu au aliniona mahali fulani na alikuwa akijaribu kunikumbuka.

Lakini nilipomuangalia ili niweze kumuelewa vyema alikuwa akikwepesha macho yake na kutazama upande mwingine. Na ninapogeuza uso wangu anaanza tena kunitazama bila kujua kuwa nilikuwa nikimtazama kwa pembeni mwa macho yangu.

Kusema kweli alinikosesha raha. “Kama amenipenda angeniambia tu kuliko kunitazama vile,” nikajiambia kimoyomoyo nikiwa nimekasirika.

Kwa vile muda ulikuwa umepita sana, niliona bora niondoke nirudi nyumbani.
Lakini kama aliyekuwa amesoma mawazo yangu, aliinuka haraka akanifuata nilipokuwa nimeketi na kuniambia.

“Samahani dada, kuna kitu nataka kukuomba,” akaniambia kwa Kiswahili fasaha.
Nikahisi alikuwa Mzungu mwenyeji kwani alikuwa akiifahamu vyema lugha yetu.
“Bila samahani, niombe tu,” nikamjibu.

“Lakini natanguliza samahani, sijui kama utaridhika.”
“Niambie tu, ni kitu gani?”
“Naomba namba yako.”

Nilielewa kuwa alikusudia namba yangu ya simu kwa sababu hiyo ni tabia ya wanaume wengi, lakini nikamuuliza.
“Namba yangu ya….?”

“Nilikuwa na maana namba yako ya simu.”
“Kama ni hilo tu, hakuna tatizo,” nikamwambia.

Nikampa namba yangu. Nilimpa ili anipigie na kunieleza kile alichokuwa nacho moyoni mwake.Nilipomtajia namba yangu aliiandika kwenye simu yake kisha akanipigia hapohapo.

Simu yangu ilipoita aliniambia.
“Namba yangu ndiyo hiyo, ahsante sana.”
Hakurudi tena kwenye meza yake, akatoka. Kwa vile mtu aliyefanya niamue kuondoka alishatangulia kutoka nikaona niendelee kukaa kidogo.

Lakini sikutimiza hata nusu saa, nikainuka na kutoka. Nilirudi nyumbani kwa teksi. Nikafikia kuoga na kujilaza kitandani.

Wakati usingizi unataka kunichukua, simu yangu ikaita. Nilipoichukua na kutazama kwenye skrini niliona namba ya yule mzungu. Nikaipokea simu yake.
“Hello!” nikasema kwenye simu.

Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.
Simulizi yangu ya “NILIVYOGEUZWA PAKA” sasa imetoka kwenye kitabu. Kwa mawasiliano ya kupata kitabu hicho piga namba 0712777737

1 Comment
  1. Aisha Chumo says

    Hahaha alifikiri namba viatu ama? Thank god huyu jini wa hadithi hii ni mzungu maana wengine wameshakariri majini ni waarabu.

Leave A Reply