The House of Favourite Newspapers

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-17

1

ILIPOISHIA IJUMAA:
Kumbe pale simu ilipokata mawasiliano, dada alijaribu kunipigia tena lakini hakunipata, akampigia yule mganga na kumweleza kuwa nilitekwa na yule jini wakati nakwenda kwa mganga huyo.

Mganga akataharuki. Baada ya kuzungumza na mashetani yake akamwambia dada ameshapajua mahali nilipo hivyo atakodi teksi kunifuata. Mganga akachukua vifaa vyake akaenda kukodi teksi.
SASA ENDELEA…

Kilichotokea ni kwamba ghafla tu yule jini aliniruhusu nirudi nyumbani baada ya kunipa onyo lake la mwisho.
Aliniambia: “Hii ni nafasi yako ya mwisho ya kuyasalimisha maisha yako. Kama nafasi hii hutaitumia vizuri, jua kwamba utakuja kujuta.”
Mimi nilijifanya namuitikia huku nimeinamisha kichwa. Akanikodia teksi nyingine na akailipia kabisa. Wakati mimi naondoka na teksi, teksi ya mganga nayo ikasimama nyuma yetu. Hapo nilimsifu yule mganga kwamba alipagundua kweli mahali nilipokuwa.

Lakini alipofika hapo hakunikuta ikabidi anipigie simu. Kwa vile nilikuwa nimeshaachana na yule jini, simu yangu ikaita. Nikaipokea.
“Uko wapi?” Mganga huyo akaniuliza kwa sauti ya wasiwasi.

“Nilikuwa kwenye hoteli moja lakini nimeshaondoka, niko kwenye teksi narudi nyumbani.”
“Si ulikuwa unakuja kwangu?”
“Nilikuwa nakuja kwako lakini ghafla nilikutana na yule jini akanipakia kwenye teksi na kunileta hapo hotelini, akaniambia maneno yake kisha ghafla akaniambia nirudi nyumbani.”
“Ameniogopa mimi, alijua kuwa ninamfuata yeye. Mimi nimefika hapa hotelini mlipokuwa. Lengo langu lilikuwa ni kumkomoa yeye.”
“Mimi nimeshaondoka lakini huyo jini naona bado yupo hapohapo anakunywa pombe.”
“Bila shaka na yeye pia ameshaondoka. Sasa nakuja hukohuko nyumbani kwenu. Nataka nihakikishe kuwa hakufuati tena.”
“Sawa. Wewe njoo nyumbani utanikuta.”
Mganga alipokata tu simu dada naye akanipigia.
“Uko wapi Enjo?” akaniuliza kwa wasiwasi.

“Niko kwenye teksi ninakuja nyumbani.”
“Mbona ulikuwa hupatikani, imekuwaje?”
“Yule Mzungu alinipeleka hotelini akaninunulia soda. Ameniambia yeye haogopi waganga na kama  nitaendelea kumsumbua nitakuja kujuta.”
“Mimi nilipoona hupatikani nilimpigia yule mganga nikamweleza kuwa huyo jini amekutokea na amekuchukua kwenye teksi. Akaniambia ameshapajua alikokupeleka…”
“Huyo mganga amefika hadi hapo hotelini lakini nilikuwa nimeshaondoka, amenipigia simu.”
“Anaonekana ni mganga hodari sana. Sasa sijui itakuwaje?”
“Ameniambia anakuja nyumbani.”
“Itakuwa vizuri, aje akushughulikie hukuhuku.”
Baada ya kuzungumza na dada, kidogo moyo wangu ulipata faraja. Nikawaza kwamba iwapo mganga huyo atafanikiwa kumtokomeza huyu jini, atakuwa amenisaidia sana.
Kufumba na kufumbua teksi ikaingia Sinza. Nilimuelekeza dereva mtaa aliokuwa anaishi dada, akanipeleka hadi nyumbani kwake.

Wakati huo sikujua kwamba teksi iliyompakia yule mganga nayo ilikuwa imeshaingia kwenye mtaa huo. Wakati nashuka kwenye ile teksi mganga huyo akanipigia simu.
“Umeshafika nyumbani?” akaniuliza.
“Ndiyo nimeshafika, wewe uko wapi?”
“Tumeingia kwenye huu mtaa alionitajia dada yako, sasa ninaitafuta nyumba yenu sijui ni ipi?”
Kwa mbali nikaona teksi inakuja.

“Nimeona teksi inakuja iliko nyumba yetu, hebu endeleeni kuja. Mimi nimesimama nje nawasubiri.”
“Nimeshakuona. Umevaa dela la rangi ya njano,” mganga akaniambia.
“Ndiyo ni mimi.”
“Sawa. Nakuja.”
Mganga akakata simu.
Wakati ile teksi inakuja kulikuwa na lori la mchanga ambalo lilitokea upande wa pili wa barabara. Nyuma ya lori hilo kulikuwa na pikipiki iliyokuwa inaendeshwa kwa mwendo wa kasi.

Pikipiki ikalipita lori la mchanga na kukutana uso kwa uso na ile teksi. Teksi ikaikwepa pikipiki na kuelekeana uso kwa uso na lori. Dereva wa teksi alijaribu kulikwepa lori la mchanga lakini alishamchanganya dereva wa lori ambaye alimfuata hukohuko. Lori na teksi zikagongana uso kwa uso. Teksi ilipinduliwa na kulala chali huku tairi zake zikiendelea kuzunguka.

Kishindo kilichosikika hapo pamoja na vumbi lililorushwa vilifanya nitoke mbio na kwenda kugonga kwenye geti la nyumba ya dada.
“Dada! Dada. Hebu fungua!”
“Kumetokea nini Enjo?” dada akaniuliza kwa fadhaa. Kile kishindo na yeye kilimshtua humo ndani.
Nikamsikia anakuja mbio na kufungua geti.

“Nini?” akaniuliza huku akitupa macho barabarani.
Ile ajali ilikuwa imetokea karibu kabisa na nyumba ya dada.
“Ile teksi aliyopanda mganga imegongwa na lori,” nikamwambia.
“Hivi atakuwa amesalimika kweli?”
“Sijui.”
Wakati namjibu dada hivyo, tukaona michirizi ya damu ikivuja chini ya teksi, nikamsikia dada yangu akisema: “Yesu wangu!”
Tayari watu walikuwa wakikimbilia mahali hapo wakiwemo vibaka na wasamaria wema waliokuwa na nia njema ya kutoa msaada.

Je, mganga alisalimika katika ajali hiyo mbaya? Usikose kufuatilia mwendelezo wa mchirizi huu katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.

1 Comment
  1. neema mikey says

    eeh kaz ipo

Leave A Reply