The House of Favourite Newspapers

Sitta hajui alikotoka, atajuaje anakokwenda?

0

NA RICHARD MANYOTA

www.richmanyota.blogspot.com

+255 714 895555

UKIMTAFAKARI Samuel Sitta unaweza kumfananisha na mtu anayepiga yowe kuomba msaada baada ya kupotea njia. Mapito yake kisiasa yanaonesha hiki ninachokiandika.

Sitta ni mwanasiasa mkongwe na maarufu; mwenye historia ndefu ya uongozi aliyehudumu katika awamu nne tofauti za urais wa Tanzania kwa nyadhifa mbalimbali. Hakuna ubishi kwamba mwanasiasa huyu amevuma sana tangu alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966 ambapo historia inamuonesha kuwa aliwahi kukumbwa na kadhia ya kuongoza mgomo wa wanachuo akiwa na mwenzake Wilfred Mwabulambo kiasi cha kupewa adhabu ya kucharazwa bakora na Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere. Sitta si mtu wa kubeza katika msimamo; ni hodari wa kusimamia anachokiamini.

Siyo mwepesi wa kusema ‘ndiyo’ katika jambo analodhani linameza utu na heshima yake hata kama limeletwa na mtu mkubwa. Aliwashangaza wengi Februari, 2008 wakati alipomwambia rais mstaafu, Jakaya Kikwete ‘awe mkali kidogo’ katika kuwashughulikia watendaji wabovu.

Hii ni sifa njema lakini pengine ameshindwa kuitumia kupata heshima anayoipigania mbele ya jamii kwa miaka nenda-rudi. Kosa ni usahaulifu. Mara nyingi anguko la kisiasa analokumbana nalo, mfano wa hili la kukatwa jina lake katika uteuzi, ni kusherehesha mchakato wa kumpata spika kupitia chama chake cha CCM uliofanyika mwaka 2010 na 2015, ambapo jina lake lilikatwa kimizengwe kutokana na kasoro ya kukosa kumbukumbu.

Sitta ni mwepesi mno wa kusahau alikotoka; ni mtu wa aina yake, aliyetindikiwa sifa za kujua aendako kisiasa. Kwa upande mwingine ni hodari sana wa ‘kulia’ akipoteza mwelekeo. Niweke akiba ya maneno nisimhukumu sana. Hata hivyo, sisiti kumuona kiongozi huyu kama mwanasiasa ambaye si hodari wa kusoma alama za nyakati na kuamua vitu sahihi. Alipotangaza kuwania tena nafasi ya uspika kupitia chama chake mwaka huu, nilijiridhisha kuhusu mtazamo wangu juu yake.

Sitta, ambaye alikuwa spika kati ya mwaka 2005 -2010 na kufanikiwa kuandika historia ya kuongoza bunge lililomng’oa Edward Lowassa aliyekuwa waziri mkuu kutokana na kashfa ya Richmond, alijaribu kugombea tena kiti hicho mwaka 2010 lakini chama chake kilimkataa. Alipokosa nafasi hiyo alisikika akilaumu kuwa mtandao wa kifisadi alioung’oa kupitia Richmond na wakubwa ndani ya chama chake ndiyo waliomhujumu.

Akapuuza kuwa Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete alikuwa sehemu ya uamuzi huo wa kumuengua na kumpa nafasi Anne Makinda kuweza kushinda. Wote aliwaweka fungu moja la waliomtengenezea zengwe. Baada ya mchakato wa mwaka huo kuwa katika sura isiyomfurahisha Sitta; wengi walitarajia kuwa amejifunza kuwa ‘system’ haimtaki, hivyo anapaswa kuitazama upya hatima ya maisha yake ya kisiasa.

Wahenga husema, kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa ndiyo kosa. Kwa mshangao, Sitta alirejea kosa alilolifanya mwaka 2010, ‘mamba’ aliowatusi aliwaomba eti wamvushe mto aende kuwa spika wa bunge la 11. Bila shaka huu haukuwa uamuzi sahihi! Maana haiwezekani watu walewale, chama kilekile na mazingira yaleyale yaliyokupa matokeo hasi kutegemea kuwa yataleta matokea chanya.

Mimi nawaza tofauti katika hili; pengine Sitta ameshajua kuwa amepoteza mvuto na mwelekeo wa kisiasa hapa nchini na kwamba analazimika kutumia mfumo wa kulalamika kuonewa hata pale anaponyimwa jambo asiloliweza, lengo likiwa ni kutafuta nafasi ya uongozi utokanao na kuhurumiwa. Mwaka 2010, alipoambiwa hawezi kuwa spika; alilialia weee kiasi cha kutishia kuhama chama. Waungwana ndani ya CCM wakashauriana kwamba wamfute machozi kwa kumpa uwaziri ili asiaibike. Hata kama hakusema hadharani ‘asante’ lakini ni wazi kwamba Sitta alishukuru; maana isingekuwa huruma ya Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete kumzawadia uwaziri wa Afrika Mashariki, nyota ya mwanasiasa huyu mkongwe ingekuwa imegeuka kimondo.

Wanyamwezi husema; “Ulipoulia mnyama aitwaye korongo ndipo pa kuwindia”. Namuona Sitta anauwinda tena uwaziri kwa kutumia staili ileile ya kugombea uspika huku akilialia ili avute hisia za wakubwa ili wamteue awe mkubwa. Maana kabla hata ya mchakato wa uspika kuanza ndani ya chama chake historia ya kukatwa jina lake ilimjia kichwani; lakini kwa kuwa kukatwa na kulia amekugeuza mtaji, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwaka huu anagombea tena uspika; akikatwa tu, atalia kwa kwenda mahakamani.

Ulichopanda ndicho uvunacho; Sitta kama ana nyota ya mkasi vile; kunusa tu akakatwa! Sasa anasubiriwa kuangua kilio, safari hii sijui ataliaje, na kipi atafutwa nacho machozi.

Yote kwa yote nauona mfumo huu wa kuwafuta machozi watu kama akina Sitta wanaolilia uongozi si njia sahihi ya kukuza demokrasia na utumishi mwema uliotukuka mbele ya jamii. Dunia ya sasa ni sayari tofauti, ni vyema wenye mamlaka za uteuzi nao wakafikiri tofauti kwa lengo la kupata matokeo tofauti na haya tuliyonayo kama taifa.

Wasiojua tulikotoka watajuaje tuendako? Hebu tuwaache watu kama akina Sitta wapumzike utumishi wa umma kwa amani ili wengine nao wapate nafasi ya kulisukuma gurudumu la maendeleo ya nchi, huenda likasogea mbele na uchumi wetu ukakua!

Leave A Reply