The House of Favourite Newspapers

Siyo gari wala pesa, Global sasa kutoa zawadi ya nyumba

4Na Mwandishi Wetu

SIYO runinga, pikipiki, pesa wala gari, safari hii msomaji wa Magazeti ya Global Publishers Ltd ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani na Championi, atamiliki nyumba.

Ataimiliki nyumba hiyo kwa utaratibu uleule wa kununua magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo katika promosheni inayotarajiwa kuanza Desemba 11, 2015, ikiwa ni mara ya kwanza kwa zawadi ya nyumba kutolewa na kampuni inayomiliki vyombo vya habari.

Tangu mwaka 2000 Kampuni ya Global Publishers, imekuwa ikijihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa misaada ya kiutu na zawadi mbalimbali kupitia mashindano na promosheni.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa, michezo ya kubahatisha imekuwa ikichezeshwa na kampuni mbalimbali za habari, lakini hakuna yoyote iliyowahi kutoa zawadi ya nyumba. Zawadi kubwa zaidi kuwahi kutolewa ni magari.

Meneja mkuu wa kampuni hiyo, Abdallah Mrisho, amesema wameamua kutoa zawadi hiyo ya nyumba kwa nia ya kuwarudishia wasomaji wao faida, huku wakiamini shindano hilo litabadili maisha yao hasa kwa atakayebahatika kushinda, ili kuwa na makazi bora.

“Tunaamini maisha bora ni pamoja na nyumba bora, sasa promosheni hii ni changamoto kwa wasomaji wetu lakini lengo kubwa ni kuwarudishia faida kwa sababu tunaamini nao ni sehemu yetu,” alisema.

Mbali ya kutoa misaada kwa jamii, lakini pia kampuni hiyo imekuwa ikienzi mchango wa wasomaji wake kwa kutoa zawadi mbalimbali kupitia mashindano kama hayo.

“Sisi siyo matajiri na hatuna fedha za kutosha, lakini tunaguswa na maisha ya Watanzania wenzetu ndiyo maana tuko tayari kugawana hata kile kidogo tunachopata,” anasema Eric Shigongo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo.

Comments are closed.