The House of Favourite Newspapers

SKENDO YA NGONO KANISANI

SKENDO ya ngono kuingia kwenye nyumba ya Mungu haipendezi; lakini kwa kuwa shetani yu kazini imedaiwa kufika ndani ya Kanisa la Mlimani la Waadventista Wasabato (SDA), lililopo Mtaa wa Majengo Mapya Nyakato, Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.  

 

 

Imefikafikaje kanisani habari hiyo mbaya? Chanzo chetu kinadai eti mzee wa kanisa hilo aitwaye Opi Msafiri anatuhumiwa kuchepuka na mke wa muumini mwenzake.

Chanzo hicho kinaeleza kwamba, hivi karibuni wakati waumini wa kanisa hilo wakiwa katika ibada ya Meza ya Bwana wakiendelea na ibada aliingia mtu mmoja akiwa amevalia kofia pana (pama) na mavazi chakavu, koti na suruali huku akiwa na mkongojo mkononi kama vle ni kikongwe. “Wengi tulivyomtazama tulijua ni mzee na kwamba amekuja kwenye ibada, hatukumtilia maanani,” chanzo kilisema na kuomba hifadhi ya jina.

 

Inaelezwa kwamba, baada ya mtu huyo kuingia na muonekano huo pia alikuwa akichechemea jambo lililozidi kuwaaminisha wengi kwamba mtu huyo alikuwa ni mzee. Hata ungekuwa wewe pengine ungeshtuka mara baada ya kumuona mtu uliyedhani ni mzee akiimarika afya ghafla na kuanza kumwanzishia timbwili mzee wa kanisa.

 

Kasheshe zito lililoletwa na mtu huyo ziliondoa utulivu wa ibada ambapo inadaiwa kuwa baadhi ya waumini waliweka kando mambo ya sala na kugeuka waamuzi wa ugomvi. Mpaka hayo yote yanafanyika hakuna aliyekuwa anafahamu sababu za mtu huyo kumletea vurugu Opi ambaye kwa kiasi fulani ni mtu anayeheshimika kanisani hapo.

 

Hata hivyo, dakika zilivyozidi kwenda na nguvu nyingi kutumika kumtuliza yule mtu aliyeanzisha timbwili, tuhuma zilianza kuwekwa wazi. Inaelezwa kuwa huku akiwa anatweta kutokana na purukushani alizokuwa akizianzisha ndipo alipoanza kummwagia tuhuma Opi kuwa anatembea na mke wake.

 

“Niacheni, huyu anatembea na mke wangu, ushahidi ninao mimi siyo mjinga kuchukua uamuzi kama huu,”alisema mtu huyo. Sekunde chache baadaye waumini wote walipigwa butwaa baada ya kutambua kuwa mtu yule alikuwa ni muumini mwenzao ajulikanaye kwa jina la Dokta Magawa.

 

“Hee kumbe Dokta Magawa!” Kila mtu alishangaa kutokana na awali kutoweza kumfahamu kwa jinsi alivyokuwa amevaa.Cha kushangaza zaidi hata mke wa Dokta Magawa aitwaye Sheba ambaye naye alikuwa kwenye ibada hiyo hakuweza kumtambua mumewe alipoingia kanisani kumwanzishia kasheshe mzee Opi.

 

Hata hivyo, Dk. Magawa alipobanwa juu ya ushahidi upi unaomhakikisha kuwa Opi anajiachia na mkewe, dokta huyo alisema ana sms nyingi za alizodai ni za mapenzi za mzee huyo wa kanisa (Opi) alizokuwa akimtumia mkewe. Inaelezwa kuwa watu katika kubishabisha ikabidi dokta Magawa awaoneshe viongozi wa kanisa sms hizo zinazotajwa kutoka kwa Opi kwenda kwa Sheba.

 

“Alipowaonesha sms hizo ikabidi wajaribu kuipiga ile namba, ikaita kwenye simu ya Opi,” chanzo chetu kilidai. Aidha, Dk. Magawa alidai kuwa Opi ametumia mwanya wa uhamisho alioupata wa kituo cha kazi kutoka Mwanza kwenda Mpanda mkoani Katavi, kujisogeza kwa mke wake.

 

Uwazi lilipomtafuta Opi ili ajibu kadhia hiyo ya kusumbuliwa na Dokta Magawa kanisani kwa tuhuma ya aibu; alipopatikana kwa njia ya simu alisema: “Mheshimiwa sasa niko kwenye kikao na kitanichukua muda mrefu ila unaweza kunitafuta muda mwingine uniambie maudhui ya jambo hilo kwa kuwa hii ni taasisi ina wasemaji wake.”

 

Majira ya usiku mzee huyo wa kanisa alimpigia simu mwandishi wetu, lakini alipoelezwa tuhuma za kujivinjari na mke wa mtu kiasi cha kusababisha sintofahamu kanisani tena siku ya Meza ya Bwana aling’aka kuwa halifahamu jambo hilo.

 

“Jambo hilo silijui na halikuwahi kunitokea kama unavyosema. Labda nikutumie namba ya mwenzangu umuulize yeye,”alisema Opi na baadaye kutuma namba ya mtu aliyetakiwa kuulizwa. Aidha, baada ya mwandishi wetu kuipiga namba aliyopewa alipokea mtu aliyejitambulisha kuwa ndiye Mchungaji wa Kanisa hilo aitwaye Ray Wankyo, ambapo alipoulizwa juu ya tukio hilo la aibu kutokea kanisani kwake alisema:

 

“Kila kitu kina utaratibu wake na siwezi kuwa msemaji na hata kanisa lina utaratibu wake na msemaji ni kiongozi mkuu wa makao makuu (Conference). Halafu kama unamsaidia mtu kiroho huwezi kusema mambo yake nje.” Mchungaji Wankyo alisema bila kufafanua ni mambo gani ya Opi asiyoweza kuyasema nje na kuongeza:

 

“Labda tungekutana ningependa kujua uliipataje hiyo habari na nadhani aliyekupa atakuwa analifahamu suala hilo kwa undani zaidi lakini pia ndani ya kanisa hiyo siyo habari na jambo hilo halipaswi kwenda nje.”

 

Mchungaji huyo alisema kuwa hata Yesu alikuja kwa ajili ya watu wenye dhambi na alikula nao chakula na kushindwa tena kuweka wazi kwamba maneno hayo yanamhusu Opi na kwamba ni mwenye dhambi asiyetakiwa kutengwa ama la! Habari kutoka chanzo chetu zinaeleza kuwa siku hiyo ya tukio mwenyekiti wa mtaa aliitwa kutuliza vurugu jambo ambalo Uwazi liliona ni vema naye atafutwe ili azungumze anachofahamu kuhusu tuhuma hizo za ngono kuingia kanisani.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo Mapya, Deus Malunde alikiri kuitwa kanisani hapo siku ya tukio kushuhudia timbili hizo ambapo anadai alipofika alikuta waumini wamemshikilia mtu mmoja ambaye walikuwa wakimwita kwa jina la Dokta wakimtuhumu kutaka kumpiga mzee wa kanisa hilo Opi kwa nondo.

 

Alieleza kuwa alipotaka kuchukua hatua viongozi wa kanisa hilo walimzuia kwa madai ya kulishughulikia na kulimaliza kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kanisa lao ingawa alishuhudia ujumbe mfupi (sms) wa simu uliotolewa na Dk. Magawa ambao unadaiwa ulitumwa na mzee huyo wa kanisa kwenda kwa mke wa daktari huyo wa binadamu.

 

Malunde alieleza zaidi kuwa alipomuuliza mzee wa kanisa kuhusu ukweli wa meseji hizo alijitetea kuwa alituma ili kumkumbusha mwanamke huyo amlipe deni la fedha alizomkopesha bila kufafanua alimkopesha lini na kwa masharti gani. Hadi tunakwenda mtambo inaelezwa kuwa Dokta Magawa amesharejea kwenye kituo chake cha kazi na kwamba ameacha fukuto kanisa hapo linalohusiana na skendo hiyo ya ngono.

 

“Bado kuna waumini wanalalamika kwamba hatua za kulisafisha kanisa hazijachukuliwa na kwamba kuna hali ya kulindana,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kanisa hilo la SDA.

Comments are closed.