The House of Favourite Newspapers

SKENDO YA UMBEYA MKE WA MTU AFUNGA MTAA

MKE wa mtu aliyefahamika kwa jina la Mama Glory hivi karibuni alifunga mtaa baada ya kumzulia timbwili la aina yake mwanamke mwenzake aliyetajwa kwa jina la Hadija, chanzo kikidaiwa ni mambo ya umbeya.  

 

Timbwili hilo lilitokea maeneo ya Goba Kontena jijini Dar ambapo inadaiwa Mama Glory alimvaa Hadija akimtuhumu kupeleka maneno ya umbeya kwa mume wake na kumsababishia matatizo.

Paparazi wetu akiwa kwenye mishemishe za kusaka habari, alikumbana na tukio hilo saa 8 mchana ambapo wakati mama Glory akishusha kichapo alisikika akisema: “Niachieni nimfunze adabu kidogo huyu (tusi) mmbeya sana huyu, haiwezekani Baba Glory anipige bila sababu, ni yeye tu ndiye aliyempelekea umbeya, lazima nimkomeshe.”

 

Wakati wawili hao wakizichapa kavukavu, baadhi ya raia wapenda ugomvi walionekana kushadadia kwa kusema; ‘piga huyoooo, kazoea huyooooo’ ndipo mwanaume mmoja aliyekuwa eneo hilo alipolazimika kuingilia kati na kuwaamulia.

 

Hata hivyo, Mama Glory alionekana kutokuwa tayari kumuachia mbaya wake ambapo akiwa ameshikilia kanga moja iliyokuwa ikitaka kumvuka alisikika akiporomosha matusi huku akisema; ‘nitamshikisha adabu’. Baadaye wawili hao waliona wasiendelee kuwanufaisha watu, ndipo walipoachiana na kila mmoja kuchukua hamsini zake na kuwaacha watu waliokuwa wamekusanyika wakitawanyika.

 

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Mama Sakina alisema kuwa, Mama Glory alikuwa shosti wa Hadija lakini kuna siku Hadija alipeleka maneno ya umbeya kwa mume wa mwenzake, jambo lililosababisha amani kuvunjika. “Yule Hadija inasemekana kapeleka maneno ya umbeya kwa mume wa mama Glory na ndiyo chanzo cha huo ugomvi,” alisema shuhuda huyo.

Comments are closed.