The House of Favourite Newspapers

Solid Ground Family: Maisha Yalikuwa na Changamoto, Tukashindwa Kuendelea

0

 

ZAMANI Bongo Fleva ilitawaliwa na makundi mengi mno. Pengine ni kutokana na wasanii hao kutokuwa na uwezo wa kipesa wa kwenda studio mmojammoja, basi njia nzuri ilikuwa ni kujikusanya kwenye makundi huku wakichanga pesa mpaka zilipofika senti za kwenda kuwaona akina Master Jay, Mika Mwamba au P Funk Majani.

 

Kipindi cha nyuma kwenye tasnia ya muziki wa Bongo fleva makundi bora yaliyowahi kufanya vizuri kwenye muziki wa Bongo Fleva ni pamoja na Daz Nundaz Family, Berry, Park Lane, Gangwe Mobb, Solid Ground Family na mengine kama TMK, East Cost Team.

 

Leo kwenye IJUMAA SHOWBIZ tunakusogezea moja ya makundi ambayo yaliweza kufanya poa enzi hizo. Hawa si wengine bali ni Solid Ground Family.

 

Unaikumbuka Ngoma ya Bush Party? Ile pati ambayo mwigizaji Muhogo Mchungu alicheza na mbuzi? Yeah ile pati ambayo jamaa aliingia na ngedere na kuzua kitimtim kikubwa humo mpaka walipomtoa na ngedere wake ndipo utulivu uliporejea mahali pake?

Achana na Mechi Kali kati ya timu ya kifo na timu ya uhai; mechi ambayo timu ya kifo ikiongozwa na straika wao mkali, Ukimwi alipomtungua kwa ufundi mkubwa kipa Panadol wa timu ya uhai.

 

Hawa jamaa pia walitupa stori kali kama Athumani Akishalewa anavyoshindwa kujielewa.Ilikuwa ngoma kali yenye ujumbe kuhusu matumizi ya pombe kupitiliza yalivyo na madhara.

 

Hawakuishia hapo, walileta pia ngoma hatari mno ya Baba Jeni alivyopata mafao tabia yake ilivyobadilika kuwa kituko mtaani.

Kichaa cha Jerry ilikuwa ngoma nyingine kali kutoka kwao ambao ulielezea kwa kirefu ubaya wa matumizi ya bangi ambayo ilimsababishia mshkaji wao Jerry kupata ukichaa kama utani.

 

Ghafla Jerry alivaa shuka na kujiita shetani na wakati mwingine alivaa majani na kujiita yeye nyani.

Solid Ground Family walikuja na staili f’lani ambayo ilikuwa na visa vingi ndani yake vilivyokuwa vinaiasa jamii kujiepusha na starehe zisizo na lazima.

 

Haikujulikana nini kilitokea, kilichojulikana ni kwamba jamaa walipotea kama utani huku ngoma zao zikiendelea kuwa na mafunzo mengi na makubwa hadi kesho. Hakuna yeyote kati yao alieweza kutisha nje ya kundi.

 

Katika mahojiano maalum (exclusive interview) na IJUMAA SHOWBIZ, jamaa wamefunguka mambo mengine ikiwemo sababu za ukimya wao kwa muda mrefu;

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi wazee?

SOLID GROUND FAMILY: Mambo ni poa sana kama unavyoona Solid Ground family tupo na afya tele!

IJUMAA SHOWBIZ: Habari za kupotea kwa muda mrefu kwenye gemu?

 

SOLID GROUND FAMILY: Ni salama kabisa ila tuliamua kwanza kupoa kutokana na gemu la muziki kuvamiwa.

IJUMAA SHOWBIZ: Naona mmeamua kurudi mjini…

 

SOLID GROUND FAMILY: Ndiyo maana tunaona kama gemu la muziki halifanywi kama linavyotakiwa.

IJUMAA SHOWBIZ: Tunasikia stori kwamba kwenye ile video Bush Party ni kama hatukumuona vizuri, lakini aliyeingia na nyani alikuwa ni Hasheem Thabeet, je, kuna ukweli?

SOLID GROUND FAMILY: Hapana, hakuwa yeye isipokuwa watu walichanganya stori. Hasheem Thabeet tulipanda naye kwenye tamasha kubwa sana 2003, lilikuwa ni Fiesta na jamaa alikuwa anatuzimia kwa muda mrefu sana na sisi tulikuwa kama hatujashtukia kile kitu, ila ilipofika siku ya Fiesta ndiyo akatufuata na kuomba kufanya naye kazi.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Uhalisia wa jina lenu la Solid Ground Family lilitokana na nini?

SOLID GROUND FAMILY: Ni kutokana na miaka hiyo kila mtu alikuwa akija, anakuja na jina la kundi lake na kipindi hicho kila kundi lilikuwa na majina ya Kingereza kwa hiyo tulikuwa tunakopi kupitia mabraza ambao tumewakuta ndiyo na sisi tukajiita Solid Ground Family.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Kabla ya kujiita jina hilo kwanza muwaeleze mashabiki mlikutanaje watatu?

SOLID GROUND FAMILY: Tulikuwa tunakaa mtaa mmoja na kulikuwa na harakati za kuweza kuonesha vipaji, tulikuwa kama madansa, lakini tuliweza kuachia ngoma yetu iliyokwenda kwa jina la Pilikapilika.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mmewahi kufikiria kuwa na projekti ya viapji endelevu?

SOLID GROUND FAMILY: Tuliwahi kufikiria zamani sana ila si unajua maisha haya, leo yanakuwa mazuri kesho yanabadilika; yaani kifupi maisha yalikuwa na changamoto sana kwetu hivyo tukashindwa kuendelea.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Lakini ninyi ndiyo mliwahi kabla hata ya akina Harmonize na Diamond kwa nini mshidwe?

SOLID GROUND FAMILY: Kwa kweli sisi tuliwahi sema muda wa biashara ndiyo ulikuwa siyo rafiki na sisi kama ilivyokuwa kwa sasa hivi muziki unalipa tofauti na mwanzo kabisa.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mmeamua kurudi mjini, vipi mnawaahidi nini mashabiki wenu?

SOLID GROUND FAMILY: Mambo ni mazuri kabisa na pia tunaaambia kwamba tunataka kuja na kile kitu ambacho walikitamani kwa muda mrefu, lakini hawakukipata.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Unasema kweli mtaweza kuwateka na wakati wamezoea muziki wa sasa?

SOLID GROUND FAMILY: Najua kuna ambao hawawezi hata kusikiliza muziki wa sasa hivi kutokana na maudhui na mashairi yaliyokuwa ndani ya ngoma hizo za kisasa.

Leave A Reply