Sonia Aibua Hofu Vita Ukraine

HOFU imeendelea kutanda mitandaoni baada ya mapema jana asubuhi vikosi vya Urusi kuanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi nchini Ukraine, ambako ndiko mtoto wa staa mkobgwe wa Bongo Movies, Yvonne Cherrie almaarufu Monalisa aitwaye Sonia George Otieno au Sonia Monalisa akipata elimu yake ya ngazi za juu.
Jana iliripotiwa kuwa, ilisikika milipuko katika miji mikubwa nchini humo hivyo ili kupata undani wa usalama wa binti huyo, Gazeti la IJUMAA ilimtafuta Monalisa kwa njia ya simu na baada ya kupokea na kuulizwa hali ya mwanaye huko nchini Ukraine, aliomba apigiwe baadaye kwa sababu yupo kwenye kikao.
Hata hivyo, baadaye, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mona aliandika; “Tumbo linanicheza kama mzazi. Ukraine! Hakuna ndege, nampataje mwanangu?
Mungu wasimamie watoto wetu.” Katika taarifa iliyopeperushwa kwenye runinga kubwa duniani, kabla ya alfajiri ya jana, Rais wa Urusi, Vladimir Putin alisema Urusi haina mpango wa kuikalia kimabavu Ukraine, lakini akasema jibu la Moscow litakuwa papohapo ikiwa yeyote atajaribu kukomesha hilo.
Muda mfupi baadaye, ripoti zilianza kuibuka kuhusu mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi ya Ukraine. Ukraine ilisema; “Putin alizindua uvamizi kamili wa Ukraine…”
Hadi jana mchana, watu saba waliripotiwa kuuawa katika shambulio la bomu llililofanywa na vikosi vya Urusi. Kwa mujibu wa Polisi wa Ukraine, shambulio dhidi ya kambi ya jeshi ya Podilsk; nje ya Mji wa Odessa liliwaua watu saba na kuwajeruhi wengine huku watu 19 hawakujulikana waliko.
Huku hayo yakijiri Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilinukuliwa na Shirika la Habari la Urusi -Interfax ikisema kuwa;
“Ulinzi wa anga wa vikosi vya jeshi la Ukraine umekandamizwa.” Wizara hiyo iliongeza; “Vikosi vya mpaka vya Ukraine havikupinga vitengo vya Urusi.”
STORI: MEMORISE RICHARD, DAR

