The House of Favourite Newspapers

Spika Wa Bunge Atoa Onyo kwa Gazeti la Mtanzania, Nipashe na Mwananchi (Video)

0

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametoa onyo kali kwa waandishi na wahariri wa magazeti ya Mtanzania,  Mwananchi na Nipashe kwa kuvunja sheria ya haki na kinga za bunge, kwa kuchapisha mwenendo wa shauri lililokuwa likimhusu Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini.

 

Akizungumza bungeni kabla ya kuahirishwa kwa vikao vya bunge, Spika Ndugai alisema kwamba Septemba 21, 2017, Zitto alikuwa akihojiwa na kamati ya maadili ya bunge kuhusu madai ya kudharau mamlaka ya spika wa bunge, ambapo alipotoka, kwa kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, alichapisha kila alichohojiwa kwenye kamati hiyo.

 

Siku iliyofuata, Septemba 22, 2017, magazeti hayo yaliandika kuhusu shauri hilo, jambo ambalo ni kinyume na sheria za haki na kinga za bunge, hivyo Spika Ndugai akaagiza wahariri na waandishi wa habari hizo, waitwe na kuhojiwa, jambo ambalo lilifanyika.

 

Spika Ndugai ameongeza kwamba, baada ya kuhojiwa kwa waandishi na wahariri wa magazeti hayo, wamejiridhisha kwamba walifanya makosa hivyo wamepewa onyo kali na kutakiwa kuchapisha habari za kuomba radhi kwenye kurasa za mbele za magazeti yao ndani ya muda wa siku tano kuanzia Novemba 17, 2017 na kwamba atakayekiuka, ameshamwagiza mwanasheria mkuu kumpeleka mahakamani.

 

Kuhusu Zitto, Spika Ndugai amesema hajafika kwenye kamati ya maadili hivyo suala lake bado linashughulikiwa na litakapokamilika, hatua stahiki zitachukuliwa.

Stori: Sweetbert Lukonge | Championi Ijumaa

Leave A Reply