The House of Favourite Newspapers

Spoti Xtra: Asanteni Kwa Kutukubali, Tunawaahidi Makubwa Zaidi Kila Jumapili

LEO ni toleo la 15 tangu Spoti Xtra tuingie mtaani Desemba 17 mwaka jana. Tunashukuru kwa kutuunga mkono tangu siku ya kwanza mpaka sasa.

 

Muitikio wenu umekuwa mkubwa kutuunga mkono kama tulivyotarajia, jambo ambalo limedhihirisha kwamba tathmini yetu tuliyoifanya sokoni kabla ya kuliingiza Spoti Xtra ilikuwa sahihi na ya kisayansi.

 

Tumejitahidi tangu siku ya kwanza kuimarisha yaliyomo ndani ya gazeti lenu la Spoti Xtra, tumekuja kukata kiu ya habari za michezo na burudani ambayo ilikuwa tatizo kubwa kwa wasomaji haswa wa wikiendi.

 

Kabla ya kuingia sokoni tulifanya tathmini na kubaini kwamba mlichokuwa mkikipata kwenye magazeti mengi kilikuwa chepesi sana, ndipo tukaamua kujipanga ili kuja na vitu vya ziada ambavyo tunafurahia muitikio wenu wa kununua gazeti kwa wingi kila Jumapili ambao unamaanisha kwamba mmekubali.

Mpangilio wetu wa kurasa 24 pamoja na usanifu wa kurasa umekuwa kivutio kwa wasomaji na tunaahidi kuuimarisha zaidi kwa kiwango cha kimataifa.

 

Tumekuwa tukipokea pia maoni yenu kila siku na kuyafanyia kazi kwa kadri inavyowezekana ili kuendelea kuboresha zaidi kwa vile nyie ndio watumiaji wa bidhaa yetu na ili kwenda na wakati lazima kujua uhalisia ulioko mtaani.

 

Kwa muda mfupi Spoti Xtra imefanya vizuri na kuwa gazeti linalouzika na kusomwa zaidi siku ya Jumapili, tunazidi kusisitiza kwamba tunashukuru sana kwa sapoti yenu wasomaji na wadau wa michezo, mmetupa heshima ya aina yake ambayo inatufanya tuzidi kuwaboreshea zaidi na kuwapa mambo mazuri.

 

Tunaelewa kwamba kuna baadhi yenu mmetuma maoni mkiomba tuongeze siku ya kulitoa gazeti hili, tunawaahidi tunalifanyia kazi kwa kuimarisha miundombinu yetu na punde ndani ya kipindi kifupi tutawapa taarifa rasmi kuhusu hilo.

 

Spoti Xtra tunawaahidi kwamba tutazidi kuboresha yaliyomo kuanzia habari za Kitaifa na Kimataifa, chambuzi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunazidi kuwapa heshima na thamani ya fedha yenu.

Tutaendelea kuwapa zaidi ya kile mnachokitaka, tuna timu yenye uzoefu unaojitosheleza hivyo endeleeni kutuunga mkono na mtapata mambo matamu zaidi.

 

Heshima mliotupa ya kuongoza soko la magazeti ya siku ya Jumapili ni kubwa na tunawaahidi hamtajuta kuendelea kununua Spoti Xtra kwa vile kwa misemo sahihi ya lugha za wanamichezo ni kwamba ndio kwanza gari limepata moto, tegemeeeni mambo makubwa.

 

Ni katika kutambua hilo la kutuunga mkono, tumewaletea zawadi mbalimbali za kushindaniwa ndani ya Spoti Xtra ikiwemo Headphone Orijino za Beats by Dre kutoka Marekani.

 

Si hizo tu kuna zawadi mbalimbali za jezi orijino za timu za Ligi Kuu ya England, kila Jumapili, mashabiki watajishindia zawadi hizo kirahisi kabla kwa kushiriki shindano lilipo kwenye ukurasa wa pili.

 

Mambo makubwa yanakuja wasomaji wetu kaeni mkao wa kula, tumejidhatiti na tumeingia mtaani kuwapa mambo mnayoyahitaji. Hatukuja kubahatisha ndio maana muundo wa gazeti hili kwa upande wa yaliyomo ni tofauti kabisa na huwezi kufananisha na yoyote yule ndani ya Afrika Mashariki. Tumejipanga na tutazidi kuwafurahisha wasomaji wetu, asanteni kwa kutuamini na kutupa heshima.

BODI YA UHARIRI – SPOTI XTRA

Comments are closed.