The House of Favourite Newspapers

Straika Al Ahly Awatangazia Vita Simba

0

MSHAMBULIAJI wa Al Ahly, raia wa DR Congo, Walter Bwalya amefunguka kitendo cha timu yake kupangwa kundi moja na Simba ndiyo nafasi yake pekee ya kulipiza kisasi cha msimu wa mwaka 2018/19 alipokuwa akichezea Nkana ya Zambia.

 

Bwalya ambaye kwa sasa anachezea Al Ahly alijiunga nayo mapema mwaka huu kwa mkataba wa miaka minne akitokea El Gouna ya Misri.

 

Kabla ya kujiunga na El Gouna mshambuliaji huyo mwenye uraia wa DR Congo alikuwa akiichezea Nkana ya Zambia ambayo ilitolewa katika hatua ya mtoano Simba kwa kipigo cha mabao 4-3.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Bwalya alisema kuwa imekuwa bahati kubwa kwake kuwa atakutana na Simba ambayo iliacha kumbumbuku mbaya akiwa na Nkana hivyo sasa ni wakati wa kuweza kulipiza kisasi licha ya kuwa na timu nyingine.

“Ukiangalia kundi letu siyo rahisi kwa sababu timu zilizokuwepo zote ni ngumu na zimekuwa na uzoefu wa mashindano ambayo tunashiriki kwa muda mrefu, ukiwaangalia, AS Vita, El Merreikh na hata Simba hivyo lazima maandalizi yawe ya kutosha.

 

“Lakini kwa upande wangu imekuwa furaha kwa sababu napata fursa nyingine ya kuweza kulipiza kisasi dhidi ya Simba ambayo iliniachia kumbukumbu mbaya wakati nikiwa Nkana, naamini nitautumia mchezo huo kwa kuhakikisha tunashinda mechi zote mbili.

 

”Katika michuano hiyo, Simba imepangwa kundi A, ikiwa na AS Vita ya DR Congo, Al Ahly ya Misri na El Merreikh ya Sudan ambapo Simba itacheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya AS Vita, Februari 12, mwaka huu kabla ya kukutana na Al Ahly Februari 23, mwaka huu.

Stori: Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Leave A Reply