Straika Mkongo: Nitafunga Sana
BAADA ya kuanza vizuri maisha yake mapya ndani ya kikosi cha Azam kwa kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-1 walioupata katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Horseed ya Somalia, Straika Mkongomani, Idris Mbombo amefunguka kuwa atafunga mabao mengi zaidi msimu ujao.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa juzi Jumamosi, Mbombo aliifungia Azam bao la pili dakika ya 73 ya mchezo huo ambao Azam walishinda kwa mabao 3-1.
Mbombo alikamilisha usajili wake ndani ya Azam na kutambulishwa rasmi Julai 31, mwaka huu akitokea kwenye kikosi cha klabu ya El Gouna inayoshiriki Ligi Kuu nchini Misri ambapo alisaini mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mbombo alisema: “Kwangu kama mchezaji ni jambo la kushukuru Mungu kuweza kufunga bao ambalo limeisaidia timu yangu kupata ushindi muhimu siku ya Jumamosi dhidi ya Horseed ya Somalia.
“Licha ya kufunga bao hilo lakini binafsi naona bado nina kazi kubwa ya kufanya, ili kurejea katika kiwango changu, hii ni kwa sababu kwa muda mrefu nilikuwa benchi kule El Gouna, hivyo nitapambana mazoezini ili kufunga mabao mengi zaidi kwa kila nafasi nitakayoaminiwa na kocha.”
JOEL THOMAS, DAR ES SALAAM