Paul Kiongera, raia wa Kenya.
Khadija Mngwai,
Dar es Salaam
UONGOZI wa Klabu ya Simba umeeleza kuwa tayari umeshamtumia tiketi mshambuliaji wake, Paul Kiongera, raia wa Kenya, ili kujiunga na kikosi hicho tayari kwa kumalizia mzunguko wa kwanza.
Awali, Simba ilimsajili Kiongera misimu wa 2013/14 kwa mkataba wa miaka miwili lakini alishindwa kuisaidia timu hiyo baada ya kuumia goti katika mchezo dhidi ya Coastal Union, hivyo kupelekwa nchini India kufanyiwa upasuaji kisha kutolewa kwa mkopo katika timu ya KCB ya Kenya.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mratibu wa Simba, Abass Ally, amesema tayari uongozi wa klabu hiyo umeshamtumia tiketi Kiongera na wakati wowote atatua nchini kwa ajili ya kujiunga na wachezaji wenzake kuanza mazoezi.
“Tunatarajia kuanza mazoezi ya beach leo (jana) kwa ajili ya kujiandaa kumalizia mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ambapo baadhi ya wachezaji wameshawasili akiwemo kipa Vincent Agban na wachezaji wengine waliokuwa wamepewa tiketi za kwenda kwao na kurejea nchini.
“Kuhusu Kiongera, tayari ameshatumiwa tiketi ya kuwasili nchini ambapo wakati wowote kuanzia sasa atatua kwa ajili ya kujiunga na wachezaji wengine kujiandaa na michezo iliyobaki katika mzunguko wa kwanza,” alisema Ally.
Simba imekuwa ikisumbuka kutokana na nafasi ya mshambuliaji kutokuwa na mtu makini wa kutupia mabao na kila mmoja anaamini kuwa Kiongera atakuwa mtu sahihi kwenye nafasi hiyo.
Taarifa zimekuwa zikisema kuwa endapo Kiongera ambaye anatarajiwa kutua hapa nchini wiki hii atakuja, basi kuna uwezekano mkubwa, mshambuliaji Pape Nd’aw akafunguliwa mlango wa kwa heri.
Awali ilielezwa kuwa mshambuliaji huyo raia wa Senegal hatarejea nchini baada ya kwenda mapumzikoni lakini ajabu juzi alikuwa wa kwanza kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.