The House of Favourite Newspapers

Suala la Nyosso laibuliwa upya TFF

0

Nyosso2Beki Juma Nyosso.

Na Hans Mloli

ISHU ya beki Juma Nyosso aliyefungiwa miaka miwili kutocheza soka, imeibuliwa upya baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa na mchakato wa kupitia upya na kujiridhisha kama hukumu hiyo ni halali au itenguliwe.

Hiyo imekuja baada ya Chama cha Wacheza Soka Tanzania (Sputanza) kuwasilisha ombi lao la kufanyika upya kwa zoezi hilo takriban wiki moja iliyopita na TFF kupitia Bodi ya Ligi iliyo chini ya Mtendaji Mkuu, Boniface Wambura tayari imekubaliana na suala hilo.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Katibu Mkuu wa Sputanza, Abeid Kasabalala amesema kwamba ombi hilo waliliwasilisha pamoja na ada ya Sh 500,000 kulingana na mwongozo uliotolewa huku akisisItiza kuwa hiyo si rufaa bali ni kutaka kuona haki ikitendeka kwa mujibu wa tukio lenyewe na adhabu iliyotolewa.

“Hii adhabu iliyotolewa na kamati ya masaa 72 tunaona haijakaa sawa kwa mchezaji, kipindi alichofungiwa ni kirefu mno kwa hiyo tumewasilisha kupitia upya tukio na hata vifungu vya adhabu na kuhakikisha haki inatendeka.

“Imeshapokelewa na majibu yametoka kutoka Bodi ya Ligi kuwa muda si mrefu tutakutana pande zote ikiwezekana na mchezaji mwenyewe (Nyosso) awepo na tuangalie upya,” alisema Kasabalala.

Akiwa anaitumikia Mbeya City, Nyosso alipewa adhabu hiyo baada ya kuingia hatiani kwa kumdhalilisha nahodha wa Azam FC, John Bocco, katika moja ya mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu iliyopigwa Uwanja wa Chamazi, Dar na Azam ilishinda 2-1.

Leave A Reply