SUFURIA YA KUAZIMA HAIUNGUZI MBOGA

KAMA nakuona vile, unaringia gauni la dukani unasahau kama umevaa viatu vya mtumba, heeee heeeeiyaaa! Unalo mwaka huu shoga! Wanakwambia ukiona maharage yameiva jua mkaa umeteketea!  

 

Ulifikiri mi wa kijijini nimekuja nanuka moshi kumbe wa mjini sitoki nje mpaka nijioshe! Halooo eeeehhhh! Ukitaka kujua ugumu wa kudai kopesha ukweni, mbona roho itakutokaaa!

 

Shoga baada ya udambwidambwi huo nikupe sasa kile kilichonileta, tena usifikiri ninacheka ukajua nina furaha shoga! Ifike mahali tusikaushane uzazi basi! Kila siku nikisema jambo lina maana yake ati! Haiwezekani we mtu mmoja utufanye wanawake wote tuonekane sawa…hivi jamani lini tutaacha tabia ya kukubali kila ofa!

 

Utakuta mwanamke mzima ameolewa na watoto juu cha ajabu akiambiwa neno ofa anakuwa na kimuhemuhe, kwanza hakatai! Wajanja wa leo wanakwambia ukiona choo ndotoni wala usithubutu ukitumie, mwanamke unatakiwa ujiheshimu siyo kila unachoambiwa unakubali mwisho wa siku unaingia katika matatizo, upo nyonyo?

 

Juzi shosti wangu kaja kunilalamikia alichofanyiwa baada ya kukubali ofa kutoka kwa mwanaume ambaye naye ana mke. Anasema kuwa alianza kuzoeana naye kupitia simu, baada ya kukosea namba. Baada ya muda wakahamishia WhatsApp na mwisho wa siku wakawa wanaonana bila mumewe kujua. Sasa kimbembe juzi jamaa alitaka kumtoa ‘out’ mtoto wa kike wala hakujiuliza akajiandaa na kwenda tena mbaya zaidi akamdanganya hadi mumewe! Kufika jamaa akampa bia wee hadi akalewa na kushindwa kujitambua.

 

Alichofanyiwa ni kupelekwa nyumba ya wageni na kufanya michezo yao michafu mbaya zaidi akiwa hajitambui na mwishowe akatelekezwa karibu na nyumbani kwao! Aibu ilioje mbele ya mumewe! Maana kila akiulizwa anaropoka tu, kuangalia simu yake ina mawasiliano ya yule mwanaume! Hivi ninavyoongea mbona palichimbika.

Nikugeukie na wewe shoga yangu, siyo unajifanya fundi bomba wakati umevaa suti inahu? Na kama ulijua kila usafiri unahitaji konda basi umenoa, kwa taarifa yako bodaboda na bajaj wala hazihitaji konda! Kwani ni lazima kuwa karibu na mwanaume ambaye unajua kabisa analeta uhusiano wa kimapenzi wakati una mume na watoto! Tubadilike jamani tangu lini mguu wa bandia ukawa na vinyweleo?

 

Shoga eeehhh, mchafu hachafuki na akichafuka basi alikuwa msafi huyo! Wote tunakubaliana kuwa sufuria ya kuazima haiunguzi mboga! Kama kweli unataka kwenda kunywa kwa nini ukubali vya bure wakati mumeo yupo! Ulimuomba pesa akakataa? Wanawake tuna ujanja mwingi, je, ulishajibana ukashindwa kupata japo ka elfu tano ka bia mbili?

 

Sitaki kuongea sana ukasema leo Anti Naa amemeza betri la gari aku! Tukutane tena wiki ijayo, ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu!

Loading...

Toa comment