The House of Favourite Newspapers

Sun-El Aachia Ngoma Mpya ‘Fire’

0

 

MSANII mwenye tuzo kibao kutoka nchini Afrika Kusini, Sun-El ameachia kazi yake mpya, inayokwenda kwa jina la ‘Fire’ akiwa ameshirikiana na kundi mahiri kutoka nchini Kenya, Sauti Sol.

 

Wimbo huo mpya utakuwa miongini mwa nyimbo zitakazokuwepo kwenye albamu yake ya TO THE WORLD AND BEYOND, inayotarajiwa kutoka kesho, Desemba 4, 2020.

 

 

Wimbo wa ‘Fire’ uliotengenezwa na maprodyuza Claudio na Kenza ambao wapo kwenye project ya ElWorld Music, ni wa tano kuachiwa na msanii huyo, baada ya Never Never aliyomshirikisha Nobulhe, Madinaye alioshirikiana na Ami Faku, Ubomu Abumanga alioshirikiana na Msaki na Uhuru alioshirikiana na Azana.

 

Akizungumzia kazi hiyo aliyoshirikiana na wasanii hao wakubwa kutoka Afrika Mashariki, Sun-El anasema: “Ni furaha kubwa kufanya kazi na watu ambao nimekuwa nikiwaheshimu sana kwenye sanaa. Nimekuwa nikioneshwa mapenzi makubwa kutoka kwa watu wa Afrika Mashariki, hususan Kenya kwa hiyo ilikuwa furaha kubwa kwangu kufanya nao kazi.”

 

Chimano, msanii kutoka Kundi la Sauti Sol, akizungumzia kazi hiyo waliyoshirikiana na Sun-El, anasema ilikuwa ni nafasi ya kipekee sana kwake kupewa kazi ya kuandika mashairi ya wimbo huo na kushirikiana na Sun- EL.

“Tumependa sana hii kazi tuliyofanya naye. Kilikuwa ni kitu cha kufurahisha mno na tulichokuwa tukisubiri, ni kazi hiyo kuzinduliwa rasmi. Sun-El ni msanii mkubwa, tunayo furaha kubwa kufanya naye kazi hii, huu ni mwanzo tu, kuna project nyingine nyingi zinakuja.”

 

Wimbo wa Fire unakuwa wa kwanza kwa msanii huyo anayeheshimika sana nchini Afrika Kusini, kushirikiana na wasanii wakubwa kutoka Afrika Mashariki, tangu alipoachia wimbo wake wa Akanamali, Sun-EL amejizolea mashabiki wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Kuelekea kwenye uzinduzi wa albamu yake, Sun-EL atafanya tamasha la dakika 45 kwa njia ya mtandao, lililopewa jina la Uhuru Spaceforce, linalotarajiwa kufanyika leo,  Desemba 3, mwka huu, ambapo ataungana na wasanii wengine kama Msaki, Azana, Ami Faku, Simmy, Mthunzi na wasanii wengine wengi ambao wataalikwa kuwaburudisha mashabiki katika kipengele cha El-World RedBox.

 

Baada tu ya kumalizika kwa tamasha hilo, albamu itazinduliwa rasmi.

Neno lake kwa mashabiki wake kuelekea kwenye uzinduzi huo, Sun-EL anasema: “Nawashukuru sana mashabiki wangu wa Afrika Mashariki ambao wameendelea kuonesha mapenzi makubwa kwangu na kuniunga mkono. Natarajia katika siku za usoni kushirikiana na wasanii wengi wakubwa kutoka Afrika Mashariki ili wanitambulishe zaidi katika ukanda huo.”

 

Albamu hii ya Sun-EL, inakuja baada ya mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye albamu yake ya awali, Africa To The World, ambayo iliingia kwenye chati ya Albamu Bora 200 za Muziki wa Electronic duniani, huku ikipata kusikilizwa zaidi ya mara milioni 50 kupitia Apple Music na majukwaa mengine ya mtandaoni

Leave A Reply