The House of Favourite Newspapers

Syria: Wanajeshi 14 Wafariki kwa Shambulio la Bomu

0

Takribani wanajeshi 14 wa Syria wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa, baada ya mabomu kulipuka katika basi walilokuwa wakisafiria, tukio lililotokea Jumatano katikati ya Mji Mkuu wa Damascus.

 

Inaelezwa kuwa tukio hilo ni baya zaidi kuwahi kutokea katika Mji wa Damascus tangu vikosi vya jeshi la serikali vilipoanza kuushikilia mji huo ambao ulikuwa ngome kuu ya wapiganaji wanaoipinga serikali ya nchi hiyo kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

 

Kituo cha runinga ya taifa la nchi hiyo, kimerusha video za tukio hilo, zikilionesha basi lililoteketea baada ya kushambuliwa kwa mabomu, na kueleza kuwa tukio hilo limetokea majira ya asubuhi wakati watu wakiwahi makazini na shuleni.

 

Inaelezwa kuwa mabomu mawili yalilipuka wakati basi hilo likiwa karibu na Daraja la Hafez al-Assad ambapo maafisa wa jeshi wa kitengo cha mabomu, walifanikiwa kulitegua bomu la tatu kabla halijalipuka na kueleza kuwa tukio hilo lilikuwa ni la kigaidi.

 

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Shirika la Habari ya Syria, SANA, mabomu hayo yalikuwa yametegwa ndani ya basi hilo na mpaka sasa hakuna mtu au kikundi chochote kilichodai kuhusika na shambulio hilo.

 

Kamanda wa Polisi wa Damascus, Meja Jenerali Hussein Jumaa, akizungumza na Kituo cha Runinga ya Taifa, amenukuliwa akisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi katika eneo la tukio, ikiwa ni pamoja na kufunga njia zote jirani na eneo hilo na kuhakikisha kuwa hakuna mabomu mengine yanayoweza kuleta madhara.

 

Kamanda huyo ametoa wito kwa raia wa nchi hiyo, kutoa taarifa kwa jeshi la polisi haraka endapo wataona kitu chochote kinachotia mashaka.

 

Dakika chache baada ya kutokea kwa shambulio hilo, shambulio jingine limetokea katika Mji wa Ariha uliopo Kusini mwa Mji wa Idlib unaotajwa kuwa ngome ya upinzani, ambapo watu waliojihami kwa silaha za kivita, walifanya mashambulizi makubwa yaliyosababisha vifo vya watu takribani 10.

 

Inaelezwa kuwa shambulio la Damascus, ni baya zaidi kutokea, tangu lilipotokea shambulio lingine la mabomu, Machi 2017 na kusababisha vifo vya watu 30 ambapo Kundi la Wapiganaji wa IS, lilikiri kuhusika nalo.

 

Tangu wanajeshi wa serikali ya Syria walipopata tena udhibiti wa Mji wa Damascus miaka mitatu iliyopita, hali ya utulivu imetawala na mashambulio kama hayo ni nadra kutokea.

 

Shambulio la mwisho lilitokea mwaka mmoja uliopita, wakati Mufti wa Kisuni wa Mji wa Damascus, Adnane al-Afyouni, alipouawa katika mlipuko wa bomu lililotegwa katika gari lake.

 

Mashambulizi hayo yalipungua baada ya majeshi ya Rais Bashar al-Assad kuteketeza vituo na makundi ya kigaidi ndani ya mji huo kwa msaada wa Jeshi la Urusi na Iran na serikali ya rais huyo imeendelea kuwa na udhibiti katika maeneo mengi nchini humo.

 

Imeandaliwa na Darlya Walwa kwa msaada wa mitandao.

Leave A Reply