Taarifa Kuhusu Alikopelekwa Dereva wa Lissu

Mbowe akiwa na dereva wa Lissu siku ya tukio.

WAKATI Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto akimtaka dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki kufika katika Ofisi za Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Mkoa wa Dar es Salaam au Dodoma, CHADEMA wameeleza kuwa dereva huyo yupo jijini Nairobi.

Akizungumza juzi na waandishi wa habari mjini Dodoma, Muroto alisema kuwa dereva huyo anahitajika kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya mahojiano kutokana na yeye kuwapo katika tukio la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu.

Muroto alisema dereva huyo ana taarifa muhimu za sababu alishuhudia tukio zima hivyo ni lazima afike kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo.

Wakati Jeshi la Polisi likisema hayo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema kuwa dereva huyo, Simon Mohamed Bakari yupo jijini Nairobi ambapo naye anapatiwa matibabu.

Katika taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa Facebook wa chama hicho, Mbowe alisema kutokana na dereva huyo kushuhudia tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Lissu, waliona sio vyema kumuacha nchini kutokana na usalama wake, lakini pia alihitaji matibabu ya kisaikolojia ambayo ndiyo anayopatiwa kwa sasa Nairobi.

“Anasumbuliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Naye hatukuona busara kuendelea kumwacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na kiusalama itakapohakikishwa.”

Katika taarifa hiyo, ilielezwa kuwa, nidhahiri kwa aina ya shambulio lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwaua wote, Lissu na hata dereva wake.

Wakati huo huo, viongozi wa CHADEMA leo wamezungumza na waandishi wa habari ambapo wamesema kuwa hawana imani na Jeshi la Polisi na kwamba wanataka wawepo wachunguzi huru katika kuchunguza jaribio la kutaka kumuua Mbunge Tundu Lissu.

Naibu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Prof. Safari amesema kwamba, endapo serikali itashindwa kuleta wachunguzi huru, watakuwa wameweka wazi kwamba wanaogopa kwa sababu wachunguzi wa kimataifa wakija watawaumbua.

Chadema: Lissu Amevunjwa Mguu na Nyonga Lakini Jasiri, Tumuombee!


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Loading...

Toa comment