The House of Favourite Newspapers

Taarifa za Walio na VVU Zavujishwa

Singapore ilitoa picha ya Mikhy Farrera-Brochez, raia wa Marekani anayehusishwa na kuvujisha taarifa za matibabu za watu binafsi.

 

TAARIFA za siri za watu zaidi ya 14000 walio na virusi vya ukimwi (VVU) wakiwemo raia wa kigeni, zimeibiwa nchini Singapore na kuvujishwa mitandaoni.

 

Udukuzi huo unakuja miezi kadhaa baada ya rekodi za watu milioni 1.5 wa Singapore akiwemo Waziri Mkuu, Lee Hsein Loong, kuibiwa mwaka jana.

 

Taarifa za kibinafsi za Wasingapore 5,400 na raia wa kigeni 8,800 zilizokuwa zimeorodheshwa kutoka Januari 2013 huenda zimevujishwa.

 

Hadi mwaka 2015, raia wa kigeni walio na virusi hivyo hawakuruhusiwa kuzuru nchi hiyo japo kama watalii.

Kwa sasa, mtu yeyote anayetaka kuwa nchini humo kwa zaidi ya siku 90 kikazi, lazima afanyiwe uchunguzi wa kimatibabu kuhakikisha hana virusi hivyo.

 

Mamlaka nchini zinaamini aliyehusika na udukuzi huo huenda ni Mmarekani mmoja aliye na virusi vya ukimwi, ambaye mpenzi wake alikuwa daktari wa ngazi ya juu nchini Singapore

 

Mikhy Farrera-Brochez alishtakiwa na kufungwa baada ya kupatikana na kosa la ubadhirifu wa fedha na makosa mengine yanayohusiana na dawa za kulevya mwaka 2016.

 

Alifurushwa kutoka nchini humo mwaka uliopita. Mpenzi wake, Ler Teck Siang, raia wa Singapore, alishtakiwa kwa kumsaidi Farrera-Brochez kuweka taarifa za uongo katika rekodi zake za matibabu kuficha ukweli kuhusu hali yake ya VVU.

 

 

“Samahani mmoja wa wafanyakazi wetu wa zamani ambaye alikuwa na idhini ya kufikia takwimu za usajili wa taarifa binafsi za watu wenye VVU, huenda hakuzingatia mwongozo wa usalama uliowekwa wa kushughulikia taarifa hizo,” alisema Waziri wa Afya wa Singapore, Gan Kim Yong.

 

Jumatatu wiki hii,  maofisa wa afya walisema kuwa wamejaribu kuwasiliana na watu wote walio kwenye orodha hiyo ambao ni raia wa nchi hiyo lakini walifanikiwa kuzungumza na watu  900 pekee kati ya 5,400.

 

Namba ya dharura ya simu imetolewa kwa wale ambao huenda wameathiriwa na tukio hilo na wanataka  kupewa huduma ya ushauri nasaha.

 

Katibu wa Wizara ya Afya, Chan Heng Kee, amethibitisha hilo na kuongeza kuwa maofisa husika  wanaamini Farrera-Brochez yuko ughaibuni lakini hawajui ni wapi hasa.

 

“Kuna hofu huenda akaendelea kuvujisha taarifa hizo za siri mitandaoni,” alionya Chan.

Comments are closed.